Katika maeneo ambayo tunakosea pasipo kujua ni kujihakikishia sana juu ya leo yetu au kesho yetu, tena tunajihakikishia uwepo wetu bila kumtanguliza Mungu. Tunaona tutakuwepo tu na mtu anakuwa hana shaka juu ya hilo, uhakika wake atakuwepo vile anavyoona na kupanga.

Hii imesababisha watu wengine waendelee kumtenda Mungu dhambi wakijua wanao muda wa kutosha wa kuishi hapa duniani, wanaona bado umri unaruhusu kufanya yale anayoyaona kufanya wakati huo.

Wengine wamejihakikishia watakuwepo muda waliouona wao wenyewe, pamoja na kujihakikishia huo muda watakaokuwepo wao wenyewe. Wameshindwa kufikia muda waliokuwa wanadhani watakuwa bado wapo hai.

Tunapanga mambo mengi sana na mazuri ila tunapaswa kutambua kwamba tunapaswa kuweka nafasi ya Mungu katika mipango hiyo, tena tunapaswa kuweka neno hili, “Mungu akipenda au Mungu akijalia”

Hii inaonyesha kuwa duniani muda wowote tunaondoka Mungu akitaka tuondoke, tunapopanga mambo mbalimbali na kusahau kuwa muda wowote unaweza ukafa au ukapata jambo la kukufanya ushindwe kufanya kile ulipanga ufanye, unakuwa unakosea sana.

Mipango yetu lazima imhusishe Mungu mwenyewe, na tuwe tunasema Bwana akipenda tutakuwa hai na kufanya moja mbili tatu. Huko ni kujua kuwa duniani tu wapitaji, unaweza ukayeyuka tu na ukabaki kuitwa marehemu.

Haya sio maneno yangu, nakueleza habari ambazo zimeandikwa ndani ya biblia yako, hebu soma mistari hii uone vile tunapaswa kusema. Hii ikufanye uanze kufikiri kwa namna ya tofauti, na ujue namna ya kuzungumza.

Rejea: Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. YAK. 4:13‭-‬15 SUV.

Umeona hayo maandiko, ungeweza kusema ni maneno tu ya watu ila hapa ni kutoka ndani ya biblia takatifu, tena sisi wanadamu tumefananishwa na mvuke unaoonekana kwa kitambo tu. Kisha baadaye hutoweka huo mvuke, kwahiyo unapaswa kuwa makini sana.

Ukiwa unapanga mambo yako ya kesho, wiki, mwezi, mwaka au miaka, hakikisha unaweka kauli ya Mungu akipenda utafanya moja mbili tatu. Sio unapanga mambo yako kama mtu ambaye anajua kesho yake itakuwaje au muda mfupi ujao utakuwaje.

Mungu akusaidie kukumbuka hii, hata kama hukuwahi kujua hili umeshajua kupitia ujumbe huu ulioambatana na maandiko matakatifu. Kazi yako ni kuyaweka katika kumbukumbu zako, na yawe katika matendo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com