Ukiyaona majani ya mti vile yanavyopendeza kwa rangi nzuri ya kijani, kama hukuwahi kuona majani yanavyokauka, unaweza ukaona majani hayo yatabaki yalivyo siku zote. Lakini pamoja na uzuri wote wa majani, ukipita baada ya siku kadhaa kupita utakuta majani yale yamebadilika rangi na kukauka, kisha kuanguka chini.

Vile vile maua yake, ukiyaona yanavyopendeza kwa rangi nzuri za kuvutia, unaweza usijue kama yatafika wakati yataharibika na kupoteza ule mwonekano wake mzuri. Lakini ukija kupitia njia ile ile baada ya siku kadhaa kupita utakuta yamekauka, na kupoteza ule mwonekano wake mzuri wa maua.

Miili yetu wakati mwingine huwa inatudanganya sana, huwa tunajiona kama tutakuwepo duniani siku zote, tunajiona kama vile hatuna haja sana na kumpokea Yesu Kristo. Tunaenda mbali zaidi na kuona tuna muda wa kutosha wa kukimbizana na mambo ya dunia hii.

Tunajisahau sisi wanadamu ni kama majani ya mti, na ufahari wote ni kama ua, unaweza ukawa unajiona unao muda wa kutosha kufanya mambo yako yasiyofaa. Ukiwa unafanya hayo yote unapaswa kukumbuka hili andiko;

Rejea: Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka. 1 PET. 1:24 SUV.

Ndugu yangu huna haja kusema hayo ni majani tu, na wewe ni mtu, ndugu hili andiko halijakuwepo kwenye Biblia yako kwa bahati mbaya. Huu ndio ukweli, ukubaliane nao au uukatae, fahamu huu ni ukweli, fahamu kwamba miili yetu ni kama majani.

Vizuri sana kuutumia muda wetu vizuri na kujenga uhusiano wetu mzuri na Mungu, maana tumeshajua kuwa sisi ni watu ambao tunafananishwa na majani. Na sifa ya majani yanakauka, haijalishi yalikuwa mazuri kiasi gani, inafika wakati yanapoteza kabisa rangi yake ya kuvutia.

Majani yanakuja na kupotea, yanapopotea yanaota mengine mapya kabisa, ambayo ni tofauti na ya kwanza. Ukiwa kijana unaweza kujiona huna haja kujiweka vizuri sasa na Mungu, ukiangalia umri ulionao ni mdogo, ukajiona huna haja kujiweka karibu zaidi na Mungu.

Kumbuka siku zote mwili wako ni kama majani, muda wako wa kukauka ukifika unakauka, na unaweza usifike huo muda, akapita mpita njia na kuchuma hilo ua au jani. Maisha yako yapo mikono mwa Mungu, unapaswa kuelewa hili na kujiweka vizuri kwake.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com