Katika vitu ambavyo hatuwezi kuvikwepa kama wakristo wenye safari ya kwenda mbinguni ni kusingiziwa mambo mabaya, hili linaweza kumtokea mwamini yeyote aliyesimama vizuri na Mungu wake.

Unaweza kujitahidi kuepuka kila namna ya mazingira ambayo hayamtukuzi Mungu ila ukashangaa kutengenezewa kisa kibaya, kisa ambacho ni cha kutengenezwa tu.

Tena ukiwa mwana wa Mungu aliyesimama vizuri, mara nyingi habari mbaya juu yako huwa zinakuwa zina nguvu sana, maana shetani ndio mahali pake pa kujiinua na kuleta maneno ya kejeli kwa mtumishi wa Mungu.

Kama hutojua mbinu mbaya za shetani, unaweza ukaanza kufikiri kutafuta njia mbaya, njia ambayo itakufanya umkosee Mungu wako. Wakati ni jambo ambalo linaweza kumtokea mkristo na kupita, itategemea na vile mtu atalipokea.

Sasa tunapochafuliwa na watu kwa maneno mabaya, njia sahihi na nzuri itakayotufanya tufunike yale maneno mabaya yaliyonenwa juu yetu. Ni yale matendo yetu mazuri, tunavyoendelea kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu. Watu watamkuza Mungu wetu kwa matendo yetu mazuri.

Rejea: Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa. 1 PET. 2:12 SUV.

Ukiona mambo mabaya yanazushwa juu yako, wanakupa sifa mbaya ambazo hukuwa nazo, fahamu kwamba watazamapo matendo yako mema, watamkuza Mungu na kuona yale yaliyonenwa juu yako sio kweli.

Kujitetea kwetu sehemu nyingine ni matendo yetu mazuri, yapo maeneo hatuwezi kujiosha kwa kusema hatukufanya yale tunayoambiwa tumefanya ila kupitia matendo yetu mazuri. Watu wanapata kujua maneno waliyosikia juu yako siyo ya kweli, baada ya kuona matendo yako yanapishana na maneno waliyosikia.

Ishi kwa kumpendeza Mungu wako, zipo kesi ambazo huwezi kuzitatua kwa kuongea sana au kwa kujitetea sana, kesi zingine matendo yako mazuri ndio yatakutetea mbele za watu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com