
Unaweza kusema kwanini kila kitu mwanamke, jibu lake ni kwamba biblia haijakaa kimya kuhusu mwanamke, nasi hatutaacha kunena hizo habari njema zinazoelezwa kupitia maandiko matakatifu.
Wanaume nao wanazungumzwa sana na biblia ila kutokana na kile ambacho wanawake wametajwa hapa, napenda kukizungumzia vile ambavyo mwanamke anaweza kumsababisha yule asiyeamini aweze kuamini.
Utii wa mwanamke kwa mume wake, yaani ule utii usio na unafiki ndani yake, utii usiomkosea Mungu, utii wenye kuleta utulivu ndani ya nyumba, utii ambao unawafanya na watoto wajifunze kitu kutoka kwa mama yao.
Vile mwanamke huyu anavyomtii mume wake, ndivyo anavyozidi kuwavuta wengine kwa Yesu Kristo, anaweza asione sana kama kuna watu wanazidi kukata shauri kupitia yeye.
Sababu haswa kubwa inayowafanya watu wengine wamwamini Yesu Kristo, ni vile ambavyo mwanamke anamtii mume wake, anawafanya hata wale ambao ndoa zao zilianza kupata shida. Kupitia utii wa mwanamke yule amefanikiwa kuwafanya wanaume wengine wamrudie Kristo.
Mwanamke aliyesimama vizuri na Yesu Kristo na mwenye kumtii mume wake, huyo ni mwanamke ambaye anaweza kuhubiri bila kutoa sauti, wala bila kuandaa mpango wa kuhubiri injili ya nyumba kwa nyumba.
Ule utii tu wa mwanamke kwa mume wake, unawafanya wengine wampende Yesu, kupitia tu utii wake kwa mume wake. Hata kama kulikuwa na mwanaume ambaye haamini habari za Yesu Kristo, kupitia utii wa mwanamke kwa mume wake unamshawishi afanye.
Rejea: Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno. 1 PET. 3:1 SUV.
Watu wavutwe na mwenendo wako mama au dada, vile unavyozidi kumtii mume wako unawafanya na wengine waone kuna jambo la tofauti kabisa. Vile walikuwa wanamfahamu Yesu kwa kiwango kidogo, kupitia utii wa mwanamke watamfuata Yesu Kristo.
Mungu akusaidie sana mwanamke ili uweze kumtii mume wako, utakuwa umeokoa roho nyingi sana zilizopotoa, watakapoona maisha yako yalivyokaa ni ya namna ya tofauti kabisa.
Kumbuka siku zote usije ukasahau hili, ndoa yako ni muhimu sana kuiangalia na kuitunza vile inavyopaswa kutunzwa ili siku moja watu wajifunze kitu cha maana.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com