Kila mmoja wetu anaweza akawa ana kiu kubwa ya kuinuliwa na Mungu katika huduma yake, biashara yake, kazi yake, yapo maeneo mengi ila inategemeana na mtu anataka nini.

Katika kufikiri hivyo kila mtu kutaka Mungu amwinue katika eneo lake, anaweza akajitahidi sana kwenye kumwomba Mungu amwinue katika eneo ambalo analitamani kila wakati Mungu amwinue.

Pamoja na kutamani huko, Mungu ana taratibu zake, bila kujalisha mtu ana kiu kiasi gani cha kutaka Mungu awainue katika maisha yao. Mungu anajua hilo isipokuwa anataka tufuate utaratibu wa kiMungu ili tuweze kufikia lengo letu.

Watu wengi wanatamani Mungu awainue au awakweze katika maisha yao, lakini ukiangalia vile wanavyoenenda katika maisha yao unajua kabisa wataedelea kutamani kitu ambacho wanakosea masharti.

Kuinuliwa na Mungu inawezekana kabisa ukifuata vile unatakiwa kuenenda utaona mabadiliko yakianza kutokea kwako, mabadiliko ambayo yanakufanya Mungu akuinue viwango vya juu.

Rejea: Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 1 PET. 5:6 SUV.

Haleluya, unyenyekevu wako mbele za Mungu ndio utakufanya Mungu akukweze au akuinue kwa wakati unaofaa. Wakati ambao Bwana mwenyewe ameupanga akuinue kwa viwango vya juu.

Jambo la kuzingatia ni kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu, unyenyekevu ambao unakuwa nao wa kumaanisha, sio unyenyekevu wa maigizo. Lazima Bwana atakukweza/atakuinua kwa wakati wake, huna haja ya kuhangaika sana, wewe nyenyekea chini ya mkono wa Mungu.

Unataka Mungu akuinue kwenye huduma yako, nyenyekea kwa Mungu, unyenyekevu usio na unafiki ndani yake, unyenyekevu wenye kumaanisha Kweli. Ukiwa hivyo uwe na uhakika hutabaki kama ulivyo, Mungu lazima akuinue viwango unavyostahili kuinuliwa.

Hadi hapo utakuwa umeelewa ni jinsi gani unaweza kuinuliwa na Mungu katika eneo lolote la maisha yako, ambalo unaliona kwa jicho la tofauti. Ukielewa vizuri kabisa utaendelea kumshukuru Mungu vile anavyozidi kukuinua siku hadi siku.

Soma Neno la Mungu ufahamu mambo ya msingi kama haya, ambayo yatakufanya uishi maisha ya kumpendeza Mungu na kuelewa ni namna gani unaweza kufika eneo fulani?

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com