
Ukiwa kama mtumishi wa Mungu au ukiwa kama kiongozi mkuu katika ofisi, au ukiwa kiongozi katika mtaa/kijijini/kata yako, au ukiwa kiongozi katika familia yako. Hupaswi kuchoka kuwakumbusha mambo ya msingi wale unaowaongoza.
Zipo kanuni na taratibu unazotaka wale unaowaongoza wazishike na ukawa umetumia nguvu kubwa sana kuwaelewesha, na wakati mwingine inawezekana kabisa umekuwa nao kwenye semina au darasa la muda mrefu. Lakini pamoja na kukaa nao kwa muda wote huo, unapaswa kujua bado watahitaji kufundishwa na kukumbushwa kila wakati.
Unaweza kuwaeleza watu jambo lolote lile unalotaka walifahamu na walifanye au wasilifanye kabisa, wakaonekana kukuelewa na kufanya vile uliwaambia. Usipoendelea kuwakumbusha mara kwa mara, wanaweza wasifanye kama ulivyowaelekeza, na kama walivyoitikia.
Vile tulivyo wanadamu hadi jambo jipya lituingie na lisisahaulike na liwe sehemu ya maisha yetu, tunahitaji kujimbusha mara kwa mara, ama tunahitaji kukumbushwa mara kwa mara. Bila kujalisha hilo jambo tumelielewa sana, bado tunahitaji kuendelea kujimbusha hadi liwe sehemu ya maisha yetu.
Bila shaka umekuwa shahidi wa haya, yapo mambo mengi sana ulijifunza na ukaona ni mazuri kuyaishi au kuwa sehemu ya maisha yako. Lakini baada ya muda uliacha na kurudi kwenye maisha yale yale ya kawaida, au kwenye tabia ile ile ambayo hukupenda kuendelea kuwa nayo.
Kama umejifunza tabia nzuri au kama umefundishwa somo linalogusa maisha yako, na hayo maisha hukuwa ukiyaishi au ndio ulikuwa umeanza kuyaishi muda sio mrefu. Unahitaji kuendelea kujikumbusha kila wakati ili hilo ulilojifunza lijengeke ndani yako.
Ndio maana kila siku nakusisitiza na kukumbusha umhimu wa kusoma Neno la Mungu, najua sio jambo rahisi kukuingia moyoni au akilini mwako mara moja na kuanza kuliishi, kwa sababu tangu utoto wako hadi unakuwa mtu mzima hukuwahi kuwekewa mkazo mkubwa wa kusoma Neno la Mungu.
Ndio maana mafundisho ya neno la Mungu hayaishi kila siku, tunaendelea kuhudhuria mafundisho mbalimbali yenye kutumbusha namna ya kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Hakuna siku tutasema hatuhitaji tena kujifunza chochote.
Haya ninayokueleza hapa biblia imeweka wazi kabisa, huenda ulikuwa hujui au huenda ulikuwa unajua ila ulikuwa umeshasahau, leo nakukumbusha hili andiko uone kuwa kukumbushana ni jambo ambalo lipo kibiblia kabisa.
Rejea: Kwa hiyo nitakuwa tayari kuwakumbusha hayo siku zote, ijapokuwa mnayajua na kuthibitishwa katika kweli mliyo nayo. Nami naona ni haki, maadamu nipo mimi katika maskani hii, kuwaamsha kwa kuwakumbusha. 2 PET. 1:12-13 SUV.
Hapa watumishi wa Mungu tuna kazi ya kusimama katika hili kuhakikisha tunaendelea kuwakumbusha watu yale yawapasayo kuyatenda. Ama yale wasiyopaswa kuyatenda katika maisha yao, ili pale tutakapoondoka duniani wawe wanakumbuka yale tuliyokuwa tunawasisitiza kuyafanya au kutoyafanya.
Tukiacha kuwakumbusha mambo ya msingi na kuona kuwa wameshajua kila kitu au wameshashika kila kitu, tutakuwa tunakosea na wale tunaowaongoza watarudi katika yale ambayo tuliwakataza siku moja wasiyafanya. Tutawakuta wanayafanya kumbe tungekuwa tunawakumbusha kila wakati wasingerudi kufanya.
Unamwona mtoto wako kama mzazi hafanyi vile unataka afanye, au anafanya ila baada ya muda fulani anarudi kwenye hali yake ya unyonge. Usichoke kumwelimisha na kumkumbusha yale mambo muhimu anayopaswa kuyazingatia katika maisha yake.
Siku moja atakumbuka yote uliyokuwa unamsisitiza, wakati huo unaweza uwepo au unaweza usiwepo duniani, lakini yale mambo ya msingi uliyokuwa unamsisitiza kila siku. Yatakuwa sehemu ya maisha yake na hatakaa ayasahau kwenye maisha yake.
Waamshe watu pale unaona wamelala kwenye eneo ambalo hawakupaswa kulala, wakumbushe wajibu wao, wataamka tena na kufanya vizuri kabisa. Wale usije ukajisahau, wala usije ukachoka, maadam umeshajifunza hili kwako itakuwa sio jambo gumu maana tayari una maarifa sahihi.
Nikukumbushe kuwa kusoma Neno la Mungu kila siku ni muhimu sana kwako, kama unaona hili linakuwa gumu kwako, karibu kwenye group la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku. Hili group litakukumbusha kila siku, mwisho wake tabia ya kusoma Neno la Mungu itajengeka ndani yako na hutokaa uache kufanya hivyo.
Ili uweze kujiunga na kundi hili la wasap, tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081, hakikisha hutumi ujumbe wako sehemu yeyote. Tumia wasap tu kuwasiliana nasi kwa ajili ya kuunganishwa na kundi hili la kusoma Neno la Mungu kila siku.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081