Tunapoenda mbele za Mungu tukiwa na mashaka mengi labda tutasamehewa dhambi zetu au hatutasamehewa dhambi zetu, au tutakuwa tumesamehewa baada ya kuomba toba kwake. Ama tutakuwa bado hatujasamehewa dhambi zetu tulizozifanya.

Maswali kama haya wengi wetu huwa tunakuwa nayo vichwani mwetu, pamoja na mtu kutubu mbele za Mungu, pamoja na mtu kuokoka na kuachana na mambo mabaya ya dunia. Bado mtu huyo utamkuta ana mashaka juu ya maisha yake ya wokovu.

Mashaka yake yanakuwa labda atakuwa hajasamehewa dhambi zake alizomtenda Mungu wake, kumbe tangu siku anaziungama dhambi zake alisamehewa siku hiyo hiyo.

Pia wapo watu ambao hawataki kuziungama dhambi zao, bado wanaendelea kumtenda Mungu dhambi, hawajui kuwa wasipookoka hawawezi kuingia mbinguni. Wanaona maisha ya dhambi ni mazuri kwao, lakini ukiangalia sio kweli ni mazuri kwao, bali ni hatari kwao.

Tunapaswa kuziungama dhambi zetu mbele za Mungu, tena yeye ni mwaminifu atuondolea dhambi zetu na kutusafisha kwa damu yake. Tutakuwa viumbe vipya kabisa kwake Bwana Yesu, yale mambo ya kale yatakuwa yamepita.

Rejea: Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. 1 YOH. 1:9 SUV.

Yeye ni mwaminifu kwetu, kazi yetu ni kuchukua hatua ya kuziungama dhambi zetu, kisha yeye atatusamehe na kutusafisha na uchafu wote. Hili sio jambo la kuchukuliwa kawaida kabisa, kila mmoja anapaswa kulichukulia kwa uzito mkubwa.

Nenda mbele za Mungu ukaziungame dhambi zako zote, huna haja ya kuhangaika sana na watu, kila mmoja atapaswa kutoa hesabu yake mbele za Mungu. Ni muhimu sana uelewe kuwa kuna umhimu wa kuziungama dhambi zako zote kwake yeye anayesamehe na kutakasa.

Umekosa mbele za Mungu au ulikosea na ukaziungama dhambi zako zote, usiwe na hofu yeyote, Yesu ameshakusamehe kabisa muda ule ule ulioziungama dhambi zako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com