Kila mmoja wetu hasa sisi tuliolikiri jina la Yesu Kristo, huwa tunasema tunamjua Kristo, pamoja na kuwa matendo yetu yanamkataa Kristo. Huwa hatuachi kusema tunamjua sana Yesu Kristo.

Kusema kwetu hakuwezi kubadilisha huu ukweli kama matendo yetu yatakuwa hayampendezi Mungu, kama matendo yetu yanamkataa Kristo sisi ni waongo. Utasema uongo wangu umetoka wapi? Uongo wako ni kusema unamjua Kristo alafu matendo yako yanamkataa.

Kutozishika amri za Mungu, alafu tunasema tunamjua Kristo, huo ni uongo, tena kweli haimo ndani yetu. Hata kama tunafanya bidii sana kuonyesha kuwa tunamjua Kristo, kama hatuzishiki amri zake huo ni uongo.

Rejea: Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. 1 YOH. 2:4 SUV.

Tunapaswa kuzishika amri zake, kusema nampenda Yesu, alafu matendo yako yanamkataa unayemsema unampenda huko ni kusema uongo, tena kweli ya Mungu haimo ndani yako.

Tuishi maisha ya kumpendeza Mungu, tena hata bila kusema nampenda Yesu Kristo, matendo yako yataonyesha kuwa unampenda Yesu Kristo. Vile unaishi maisha matakatifu, unajitambulisha kwa wengine na mbele za Mungu.

Shika amri zake na kuzitenda, kuepuka kuwa mwongo, ikiwa hutazishika amri zake utakuwa mwongo, na kweli haitakuwa ndani yako. Labda unajiuliza nitawezaje kuzishika amri zake, elewa kwamba yote yanawezekana katika yeye atutiaye nguvu.

Tena neema yake yatutosha, ikiwa ametupa amri zake, anajua kuwa tunaweza kuzifuata na kuziishi katika maisha yetu ya wokovu. Haijalishi watu wanasemaje kuhusu hili, haijalishi watu watakupa shuhuda nyingi za kushindwa, amini unaweza.

Ikiwa umeelewa umhimu wa kuzishika amri za Mungu, usiache kuelewa na umhimu wa kusoma Neno la Mungu, hili ndio mwongozo wako ukiwa kama mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni.

Hakikisha kila siku unajiwekea ratiba ya kusoma Neno la Mungu, hili linawezekana kabisa ukiamua kama tulivyojifunza kuzishika amri. Tena hatuwezi kusema tunamjua Mungu pasipo kusoma Neno lake.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com