Kuna vitu vinaweza kukutokea katika maisha yako ukashindwa kuelewa ni kwanini inakutokea wewe tu na wengine haiwatokei sana wao. Na ukiangalia kosa haswa ulilowakosea unaona halipo sana, lakini unaona unachukiwa tu.

Ndugu yangu kuchukiwa na watu ukiwa umeokoka sawa sawa, hilo halipaswi kuwa jambo geni kwako, wala hupaswi kushangaa kabisa pale utakapoona unachukiwa na majirani zako, ndugu zako baadhi, au rafiki zako.

Usije ukaanza kutafuta sababu ambazo hukuwa nazo moyoni mwako, ukaanza kufikiri huenda kuna mahali umekosea, wakati unajua kabisa hukumkosea lolote yule anayekuchukia.

Kuchukiwa kwa mkristo ambaye njia zake mbele za Mungu ni safi, hilo ni jambo ambalo lipo, tena biblia yenyewe imeliweka wazi kabisa. Uone ni jinsi gani hili jambo lilivyo changamoto kwa wengi ila limetolewa majibu yake.

Rejea: Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia. 1 YOH. 3:13 SUV.

Usije ukastaajabu au ukashangaa watu wa ulimwengu wakikuchukia, yaani wale wasiomjua Yesu Kristo wakikuchukia. Maandiko matakatifu yanatuambia tusije tukastaajabu tukiyaona hayo yakitokea kwetu.

Sababu haswa ni kule kuenda kinyume chao, yale matendo yako na yao hayafanani, kwahiyo ulimwengu huwapenda walio wake. Wale ambao Mungu amewachugua ni adui kwa wana wa ulimwengu huu.

Rejea: Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. YOH. 15:19 SUV.

Umeona neno hilo, limetusaidia kuelewa yale yanayotupata yasitunyime usingizi, maana tayari tumeshajua tunachukiwa kwa sababu gani. Chuki yetu kwa watu wa ulimwengu huu, ni kwa sababu sisi si wa ulimwengu.

Fahamu haya uache kupata shida pale unapoona chuki inainuka juu yako, ukishajua utaelewa sababu za kupatwa na chuki kwa watu. Kuliko kutokuelewa utabaki ukiumia kwa jambo ambalo majibu yake yamo ndani ya biblia yako.

Soma Neno la Mungu upate maarifa sahihi ya kukusaidia katika safari ya maisha yako, utaona mambo mengi sana hupati nayo tabu kabisa. Maana utakuwa unajua kwanini hayo yanakupata.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com