Wapo watu wanaposikia habari za kuokoka wanaona uzito mkubwa sana, wanafikiri hawataweza kuzishika amri za Mungu. Wengine hufika mbali zaidi na kuona waliokoka wanaigiza tu ila hawawezi kuzishika amri za Mungu.

Wanaona kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ni jambo nzito sana lisilowezekana kabisa kwa maisha ya mkristo. Kwahiyo unapomwambia Habari za kuokoka anaona haitawezekana kwake, bora aendelee kuufuata ulimwengu unavyotaka.

Nakumbuka kabla sijaokoka nilikuwa naliona hili, nilikuwa naona kuishi maisha yanayompendeza Mungu haitawezekana kabisa. Kumbe ni mahali ambapo shetani huwabana watu wasiweza kuokoka, wokovu kwao inabakia hadithi kwa kujitia hofu wenyewe.

Na wengine wanaokoka wakiwa na picha ya amri za Mungu ni nzito sana kwao, anaenda na hii picha, asipopata mafundisho sahihi ya Neno la Mungu ya kumwondolea dhana hii potovu. Baada ya muda fulani usishangae kumwona anarudi nyuma tena.

Ndugu yangu ukiwa umeokoka, ama ukiwa hujaokoka, unapaswa kuelewa kuwa amri za Mungu sio nzito kiasi cha kukufanya ushindwe kuzishika na kuzifuata. Tukishampokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yetu, neema yake inatusaidia kuenenda sawasawa na mapenzi yake.

Rejea: Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito. 1 YOH. 5:3 SUV.

Kama ulikuwa na mtazamo hasi juu ya kushindwa kuzishika amri za Mungu, kuanzia sasa badili mtazamo wako hasi, habari njema kwako ni kuwa amri za Mungu zinawezekana kuzishika wala si nzito.

Tena anasema nira yake ni laini na mzigo wake ni mwepesi, ikiwa ni hivyo hofu yako ni nini tena? Enenda kama mkristo anayejua anaweza kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.

Rejea: Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi. Mathayo 11:30.

Umeona neno linavyosema? Kama ilikuwa unaona shaka kuhusu hili la kuweza kuishi maisha yanayompendeza Mungu au ulikuwa huoni kama inawezekana kabisa. Kuanzia sasa anza kuona inawezekana kabisa.

Mungu hawezi kuchukia dhambi zako akiwa anajua huwezi kuzishika amri zake ngumu alizokupa, anasema amri zake si nzito. Unaweza kuishi maisha yanayompendeza yeye ukiwa duniani hapa hapa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com