
Mafundisho ni mengi sana, tena kila fundisho linamjenga mtu kwa vile lilivyokusudia limjenge, linaweza likawa fundisho zuri au linaweza likawa fundisho baya. Yote yanaitwa mafundisho, mafundisho yanayomfanya mtu awe vile inatakiwa awe.
Katika mafundisho hayo yote, yapo mafundisho ya Kristo, mtu anaweza akawa vizuri katika mafundisho mengine, lakini kama mtu huyo hadumu katika mafundisho ya Kristo. Mtu huyo atakuwa hana Mungu ndani yake.
Anaweza akawa mshirika mzuri kabisa wa kuhudhuria ibada mbalimbali ila kama hadumu katika mafundisho ya Kristo, mtu huyo hana Mungu ndani yake. Hata kama atajitetea kwa namna gani, kitendo cha kuacha kudumu katika mafundisho ya Kristo, huyo hana Mungu ndani yake.
Mtu anaweza kuchukilia hili kawaida ila ukweli ndio huu kuwa hana Mungu ndani yake, lazima mkristo adumu katika mafundisho ya Kristo. Pasipo kudumu katika mafundisho sahihi ya Neno la Mungu, huyo hana Mungu ndani yake.
Sio mimi ninayesema haya, maandiko matakatifu yanatuthibitishia hili ninalokueleza hapa, linaweza likawa jambo ambalo linakupa maswali mengi ila fahamu hivyo. Hebu tusome maandiko haya uone;
Rejea: Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. 2 YOH. 1:9 SUV.
Yule anayedumu katika mafundisho ya Kristo, huyo ana Baba na Mwana, unaweza kuona ni jinsi gani tunaweza kubaki kusema ni wakristo. Na wakati hatudumu katika mafundisho ya Kristo, ama kwa kupuuza au kufuata mafundisho yasiyo sahihi.
Yapo mafundisho yanayompinga Yesu Kristo, hayamtumbui kabisa, wanamtambua tu Mungu ila Mwana hawamtambui kabisa. Wakifikiri wapo sahihi kabisa na Mungu yumo ndani yao.
Maandiko matakatifu yanatuambia yule anayemkana Mwana, huyo hana Baba, na yule anayemkiri Mwana huyo anaye Baba. Sasa asikudanganye mtu kuwa anampenda sana Mungu wakati anamkataa Yesu Kristo.
Rejea: Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia. 1 YOH. 2:23 SUV.
Sijui kama unaelewa ninachokueleza ndugu, hata kama kuna mafundisho mengi umeyapata na yamekuwekea msingi wa kutoamini Mwana wa Mungu. Kuanzia sasa anza kubadili mtazamo wako, mpe nafasi moyoni mwako Yesu Kristo ili ithibitike unaye Baba.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com