Ukiangalia kile kipindi cha mwanzo kabisa ulikuwa na subira na uvumilivu mkubwa Mbele za Mungu, hata pale ulipoomba Mungu akachelewa kujibu maombi yako. Hukuwahi kuacha kuwa na upendo mkubwa mbele za Mungu, ulikuwa unaendelea kumpenda Mungu zaidi na zaidi.

Kimetokea sijui kitu gani, ule uvumilivu wako wa mwanzo mbele za Mungu haupo tena, umefika mahali ambapo huna tena upendo mkubwa mbele za Mungu. Hufurahii tena kuokoka kwako, umefika mahali ambapo unaona kuishi maisha ya wokovu ni mzigo kwako.

Ile ladha ya wokovu wako umeipeleka wapi? Ulikuwa mtu wa subira na uvumilivu kwako ilikuwa ni jambo linalofahamika na marafiki zako wanaokufahamu. Maana ulikuwa sehemu ya kuwatia moyo wengine ambao hawana subira na uvumilivu wowote katika yale waliyomwomba Mungu.

Unaona kabisa umepoteza ule upendo wa kwanza kwa Yesu, sio jambo la kufumbia macho, lazima ukae chini ujue sababu haswa ya kukosa upendo kwa Mungu ni nini. Ukishajua sababu ni nini unapaswa kutubu na kumwambia Bwana akurejeshee furaha ya wokovu wako.

Rejea: Tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu. UFU. 2:3‭-‬5 SUV.

Ukatubu ndugu ukarudi ukayafanye yale matendo yako ya kwanza, vile ulivyokuwa na subira na uvumilivu mwingi mbele za Mungu, na ule upendo wako kwa Mungu urudi tena kwa upya.

Muhimu sana kujichunguza mwenendo wako wa kwanza upo kama ulivyoanza? Maana unaweza ukawa unaenda tu kwa mazoea. Lakini ukawa umepoteza ule upendo wako kwa Mungu kama siku zile ulivyookoka.

Siku za mwanzo wakati unaokoka ulikuwa na bidii sana ya kusoma Neno la Mungu, na sasa hauna kabisa hiyo ratiba ya kusoma Neno la Mungu. Fanya matengenezo na Mungu, na urudi katika ule usomaji wako wa biblia wa awali.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
+255759808081.