Eneo hili la kueleweka upo upande gani, watu wengi bado linawashinda sana, hata katika maisha yetu ya kimwili, ukiwa hueleweki upo upande gani watu watashindwa kukuweka katika kundi gani.

Watu wakishaona hueleweki upo upande gani, wanakuwa na mashaka na wewe, na itafika mahali hawatakuwa na imani na wewe, na kuna maeneo hutoshirikishwa mambo ya msingi kutokana na kukosa msimamo wako.

Wengi tunapenda kuonekana hatuegamii upande wowote hata kwa mambo yanayopaswa kuonyesha msimamo wako, kote unataka uonekane mwema, haijalishi hilo jambo linamchukiza Mungu wako. Unachotaka wewe ni kuonekana mzuri, bila kujalisha madhara unayopata kutokana na kutojulikana msimamo wako ni upi.

Tabia hii ya kutotaka kuonekana mbaya, ipo hadi kwenye maisha ya watu wanaosema wameokoka, hawajulikani wanamwabudu Mungu au wanamwabudu shetani.

Kwanini nasema hivyo, ukienda kanisani unawakuta wanamwabudu Mungu na ukiwaangalia kwa macho wanaonekana wanamaanisha kweli kweli. Lakini siku nyingine unawakuta wanafanya mambo yanayompendeza shetani, tena hawana hofu yeyote katika hilo.

Kwa lugha nyingine tunaweza kusema kwa Shetani wapo na kwa Yesu wapo, na kote wanatumika, usiku kwa Shetani na mchana kwa Yesu. Watu kama hawa wangejulikana moja kwa moja wapo kwa Shetani ingekuwa rahisi zaidi kupata msaada.

Unajua unapomwendea mtu ambaye unajua kabisa Shetani amemkamata na yeye haonyeshi kificho kwa hilo ni rahisi kupata msaada kwa wepesi, kuliko yule ambaye anaonyesha hayupo kwa Shetani ila amekamatika kisawasawa.

Heri mtu ajulikane wa baridi sana au wa moto sana, kuliko kuwa wa vuguvugu, hili Yesu Kristo analikataa kabisa. Na Neno lake linatuthibitishia hili ninalokuambia hapa, unachopaswa ni kuchagua kuwa upande gani.

Rejea: Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. UFU. 3:15‭-‬16 SUV.

Kama umeamua kuokoka maanisha basi, ya nini kuendelea kusema umeokoka alafu huku unachanganya wokovu na dhambi? Kuendelea kuchanganya dhambi na wokovu, yaani kuendelea kusema umeokoka alafu huku ukiendelea kufanya dhambi kwa siri huko ni kutafuta kutapikwa siku ya mwisho.

Chagua kufuata njia moja, ya Yesu au ya Shetani, zote unao uhuru wa kuchagua, hakuna mtu atakulazimisha kumfuata Yesu, wala hakuna atakayekulazimisha kumfuata Shetani.

Umeamua kumfuata Yesu Kristo, ishi vile unapaswa kuishi kama mkristo mwaminifu mbele za Mungu, michanganyo kwako iwe mwiko. Uwe mwaminifu siku zote za maisha yako, utamwona Mungu katika maisha yako ya wokovu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081