
Kinachotia faraja na kuleta amani ya Kristo ndani ya mioyo yetu, ni kujikuta unayemwamini ndiye mwenye uwezo mkubwa wa kuweza kufanya yale yaliyoshindikana na kila mtu au na viumbe vingine vyote vinavyooneka na visivyoonekana kwa macho ya nyama.
Tunachopaswa kujivunia katika maisha yetu hata kama hatuna kitu kizuri sana cha kimwili, kama vile utajiri mkubwa wa mali nyingi. Tunacho kikubwa zaidi cha kujivunia katika maisha yetu ambacho ni Yesu Kristo.
Kama umekosa kabisa jambo la kujivunia katika maisha yako, alafu ukawa umeokoka sawasawa, nakuambia ukweli unacho cha kujivunia, kuwa na Yesu Kristo ni jambo la maana sana. Maana unaye mwanzo na mwisho, yeye awezaye kutenda mambo makubwa sana.
Mambo ambayo hakuna malaika, wala hakuna mtu yeyote duniani aliyeweza kujitokeza kufanya hayo mambo makubwa, ni Yesu Kristo peke yake ndiye aliyeweza kufanya mambo makubwa sana ya kushangaza.
Rejea: Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. UFU. 5:3-4 SUV.
Unaona hapo, hakuna aliyeweza kukitwaa kitabu na kuzifungua muhuri zake, haya ni maono halisi ya Yohana wakati amechukuliwa katika ulimwengu wa roho kuonyeshwa mambo mbalimbali. Mojawapo ni hili tukio la kukosekana mtu wa kukitwaa kitabu.
Baada ya kimya kingi na kusababisha kuibua kilio cha Yohana, baada ya kuona hakuna anayeweza kukitwaa na kuzifungua muhuri zake. Lakini ghafla akajitokeza mwanakondoo.
Rejea: Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, UFU. 5:9 SUV.
Huyu ni simba kabila la Yuda, anayeweza kukitwaa kitabu na kuzifungua muhuri, hakuna yeyote mwenye uwezo huo. Ndio maana tunazo kila sababu za kujivunia huyu Yesu, tuna wokovu wa thamani sana.
Tena tunapaswa kujivunia sana wokovu wetu, tunapaswa kujiona kwa namna ya tofauti na wale ambao bado hawajajua thamani ya yule waliyembeba mioyoni mwao, au ambao hawajampokea kama Bwana na mwokozi wao. Maana anao uwezo ambao hukupatikana mahali pengine zaidi yake yeye.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com