
Kama kuna jambo la kujivunia katika maisha yako ni kumwamini Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, lingine la kufurahisha zaidi ni kule kumtumikia Mungu kwenye ule wito aliokupa Mungu.
Mtumishi wa Mungu ana thamani kubwa sana mbele za Mungu, thamani aliyonayo inaweza isionekane sana kwa macho ya kawaida, au inaweza ikawa inafahamika kuwa mtumishi wa Mungu ni mtu wa muhimu ila isiwe imepewa uzito sana.
Tunaposoma biblia tunaona hata nyakati za Sodoma na Gomora, wapo watu ambao walipona na ghadhabu ya Mungu kutokana na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu wao.
Mungu wetu anaweza kuangamiza kabisa ila anapokuwepo mtoto wake mwaminifu kwake, uwe na uhakika huyo mtu hawezi kuangamizwa kamwe na ghadhabu ya Mungu. Mungu lazima amwondoe katikati maangamizo hayo yanayotaka kumwangukia mtoto wake.
Hili tunajifunza kupitia maandiko matakatifu yanavyosema, yanatudhihirishia waziwazi kuwa hili jambo linaeleweka. Ni wewe tu kuendelea kutembea katika njia safi, njia inayokufanya kuendelea kuitwa mwana wa Mungu.
Rejea: Akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao. UFU. 7:3 SUV.
Hili andiko linatuthibitishia wazi kabisa kuwa Mungu hawezi kuachilia watu wake wakaangamizwa na adhabu aliyotoa Mungu mwenyewe. Lazima awatenganishe watu wake kwa kuwaweka alama, ambao anawataka wasipate madhara na pigo litakalokuja.
Huo ndio utaratibu wa Mungu kwa watumishi wake, au watoto wake wanaoishi maisha ya kumpendeza yeye, maisha yenye ushuhuda mzuri mbele za Mungu na mbele za watu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com