Kuchukiwa kwa mtu sio mara zote mtu huyo anakuwa anafanya mambo mabaya, ubaya wake unaweza ukawa kutokana na vile Mungu anavyomtumia kufanya mambo yanayoweza kumuumiza yule asiyelitii Neno la Mungu.

Vile Mungu anavyomtumia mtumishi wake kufanya kazi yake, kama vile Kuzuia mvua kwa miaka mitatu na miezi sita, kunaweza kuleta chuki kubwa sana kwa wale ambao walikuwa wanamtenda Mungu dhambi wakasababisha hayo yatokee.

Kwa sababu mtumishi yeyote halali wa Mungu anayo mamlaka ya kuweza kufanya jambo gumu kibinadamu kutokana na maelekezo kutoka kwa Mungu au kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu. Ambapo kwa watu inakuwa ni adhabu au pigo, pigo linaweza kusababisha madhara mengi sana kwa wanadamu na wanyama.

Madhara hayo yanapotokea uwe na uhakika utachukiwa au huyo mtumishi atachukiwa na watu, hasa wale watenda mabaya, sio hivyo anaweza kuchukiwa na ndugu wa wale ndugu wanaopotezwa na ghadhabu ya Mungu.

Hili tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, tunaona manabii wakijitokeza na kuwa watu wasiopendwa kutokana na mamlaka kubwa ya kiMungu waliyopewa.

Rejea: Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo. UFU. 11:6 SUV.

Siku ikatokea hawa manabii wawili wakauawa, watu walifurahia sana na kuwa sherehe ya kununuliana zawadi wenyewe kwa wenyewe. Hii inaonyesha wazi ni jinsi gani hilo tukio la kuawawa hao manabii liliwafurahisha sana.

Rejea: Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi. UFU. 11:10 SUV.

Ilivyo ajabu furaha yao inakuja kukatishwa ghafla baada ya Mungu kurejesha uhai wao, hili halikuwa jambo la kufurahisha kwao, wala hii haikuwa habari njema kwao.

Wale waliokuwa wamepongezana kwa zawadi mbalimbali, wanashuhudia tukio ambalo hawakutamani kuliona machoni pao. Lakini wakati wanaendelea kushangaa hilo waliona tukio lingine jipya kabisa kwao.

Rejea: Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama. Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama. UFU. 11:11‭-‬12 SUV.

Unaona hilo andiko linavyosema, lipo jambo kubwa la kujifunza hapa, kumbe Mungu anaweza kukatisha furaha ya maadui zako walioshangalia wakati umepatwa na shida ngumu.

Wale wale waliofurahia na kununuliana zawadi mbalimbali nzuri kwa ajili ya kushangalia anguko lako, ndio wale wale watakaoshuhudia kuinuliwa kwako. Kama hawa tuliowaona wakinyakuliwa juu mbinguni, na waliobaki wakapatwa na jambo lingine baya.

Rejea: Na katika saa ile palikuwa na tetemeko kuu la nchi, na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka; wanadamu elfu saba wakauawa katika tetemeko lile. Na waliosalia wakaingiwa na hofu, wakamtukuza Mungu wa mbingu. UFU. 11:13 SUV.

Mungu atusaidie sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.