
Maisha yana mambo mengi sana, ukianza kufuatilia dunia ilivyo na ukaanza kuangalia watu wake wanavyoishi unaweza ukashindwa kuelewa kabisa baadhi ya mambo.
Wapo watu wanaishi maisha ambayo ukitazama unaweza ukafikiri mwisho wa dunia labda kesho kutokana na matendo yao ya hovyo, pia unaweza kukutana na watu fulani wanavyoishi ukafikiri laiti watu wote wangekuwa hivyo dunia ingekuwa salama sana.
Wakati mtu ni mzima wa afya njema, amekula vizuri au kwa kuungaunga, au amevaa vizuri au kwa ki hivyo hivyo tu, yaani amevaa ilimradi amevaa. Mtu huyo anaweza asiwe na shaka sana kuhusu matendo yake mabaya yanayomkosea Mungu wetu.
Kutokujali kwake na kujiona yupo vizuri kwa matendo yake yale yale mabaya, mtu huyu huyu aliyekuwa anapuuza kuweka njia zake vizuri, mtu huyu huyu aliyekuwa anaona hakuna mwisho wa dunia, mtu yule yule aliyekuwa anawapuuza watumishi wa Mungu.
Mtu yule yule ambaye alikuwa anaona kuishi maisha yanayompendeza Mungu ni kupoteza muda wake, ndiye mtu ambaye anakuja kukutana na pigo la Mungu na kuanza kumtukana Mungu kutokana na maumivu wanayopitia.
Rejea: Wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao. UFU. 16:11 SUV.
Kule kukumbuka kuwa kuna kutubu mbele za Mungu unapokuwa umekosea mahali, ni muda ambao mtu anakuwa hana wakati huo, kinachomtesa ni yale maumivu makali anayoyapata.
Yapo mapigo makali yenye maumivu makali sana, mapigo ambayo akikutana nayo kwenye maisha yake, inaweza ikawa hali ngumu sana, hali ambayo inamfanya amtukane Mungu.
Rejea: Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno. UFU. 16:21 SUV.
Ndugu yangu, inawezekana kabisa usijue sana madhara ya kuishi maisha yasiyompendeza Kristo, lakini itakapofika saa ya mwisho kama hivi tunavyosoma kwenye andiko hilo nililokushirikisha unaweza mbaya.
Dawa ya kuepukana na haya yote yasije yakupata siku ya mwisho ni kupokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, na ukishampokea Yesu ishi maisha ya kumpendeza Mungu.
Mungu akusaidie sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com