Unayemwona si kitu wala si chochote, ukamchukulia vile unamwona kutokana na udhaifu wake wa kimwili, unapaswa kuelewa kuwa Mungu alimwona wa pekee sana katika uumbaji wake.

Mungu amejiridhisha mwenyewe kuwa alichokiumba yeye ni chema, ulivyo anakuona kwa namna ambayo mwanadamu hawezi kufanya uwe hivyo ulivyo.

Ukijidharau na kujiona si kitu hiyo ni wewe umeamua, Mungu alishakuona unafaa, Mungu aliona huhitaji kuongezewa uumbaji mwingine. Alishamaliza kuumba na akaona upo vizuri.

Unaweza kujikosoa kutokana na sura yako ilivyo na kuanza kufikiri labda ungekuwa kama fulani ungekuwa na furaha sana, na ungemkutukuza Mungu kwa uumbaji wake mzuri.

Umeshindwa kutambua umeumbwa kwa mfano wa Mungu, umeshindwa kujua Mungu hakuona kibaya kwako, bali aliona kila kitu ni chema kwako. Hili lilipaswa kuwa jambo la kumshukuru Mungu na kumtukuza siku zote za maisha yako.

Rejea: Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. MWA. 1:27 SUV.

Uwe mwanaume, ama uwe mwanamke, Mungu alikuumba kwa mfano wake, hakusema alimuumba mwanaume kwa mfano wake peke yake, wala hakusema alimuumba mwanamke kwa mfano wake peke yake. Kila mmoja wetu kwa jinsia yake aliumbwa kwa mfano wa Mungu.

Tena alivyomaliza kukuumba aliona kila kitu ni chema sana, maana yake naweza kusema hakuona mahali pa kurekebisha chochote, ulivyokuwa yeye aliona unafaa sana kwake. Hili sijui kama unalifahamu kwenye maisha yako, kama hakulifahamu kuanzia sasa anza kufahamu.

Rejea: Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita. MWA. 1:31 SUV.

Muhimu sana kukua kiroho, maana kuna mambo unaweza kunyanyaswa nayo kana kwamba shetani alikuumba, unaweza kujiona una sura mbaya sana. Hebu nikuulize umewahi kushiriki kwa chochote katika uumbaji wa Mungu?

Huenda umekuwa huna raha ya maisha kutokana na watu kukuambia una sura mbaya, ubaya wake umeupima na nini, anayekuambia mbaya yeye aliumbwa na nani na wewe uliumbwa na nani?

Utakuta ni yule yule Mungu, kwanini yeye ajione ni mzuri zaidi na kuanza kuwaambia wenzake wabaya, mtu wa namna hiyo ni mchanga kiroho. Anahitaji atoke kwenye eneo hilo na kwenda eneo lingine atakaloona vitu kwa mtazamo tofauti.

Mungu ana uhakika na alichokifanya kwako, huna sababu ya kujichukulia kawaida, una kila sababu za kujichukulia mtu wa viwango, mtu uliyeumbwa kwa mfano wa Mungu. Hakuna mnyama mwingine aliumbwa kwa mfano wake ni wewe pekee.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081.