Katika maisha yetu ya kila siku yapo mambo ambayo yanaweza kutufanya tukaanza kuingiwa na hofu kubwa kiasi kwamba tukaanza kukosa usingizi mzuri. Mambo ambayo tunayafikiri tu wenyewe kichwani huenda yakatokea na kutuathiri.

Sio kana kwamba vimeshatokea, wala sio kana kwamba tuna uhakika navyo mia kwa mia kuwa vitatupata na sisi, kutokana na maneno ya watu, au kutokana na habari tunazosikia zinatufanya tujawe na wasiwasi mwingi kupitiliza.

Sasa unamkuta mtu anashindwa kula kwa ajili ya hofu yake iliyomjaa ndani yake, hofu ile inampelekesha kiasi kwamba hana amani, usingizi umepotea, hamu ya kula chakula haipo tena. Anaweza akapeleka chakula mdomoni ilimradi apoze tumbo ila kupata ile ladha ya chakula inakuwa haipo.

Yupo mtu anaweza kukumbwa na hofu kubwa ya kufukuzwa kazi, hofu hii ikampelekesha kweli kweli hadi kupelekea kiwango chake cha utendaji kushuka chini. Asipokuwa makini kinachokuja kumfukuzisha kazi sio ile hofu yake, ni kile kiwango cha utendaji kilichoshuka chini kwa kusababishwa na hofu ya kitu ambacho hakikuwepo.

Zipo hofu nyingi sana ambazo zinatutesa watoto wa Mungu, hii yote ni kukosa maarifa sahihi ya kutusaidia kuondakana na kifungo hichi. Wakati mwingine ni kuyawaza sana mambo ya kesho na kumsahau anayeijua kesho yetu, na hata kama hatujamsahau tunakuwa hatuna imani kwake.

Hili la hofu lilimkumba mtumishi wa Mungu Ibrahim, hofu yake ikampelekea kusema Sara ni ndugu yake, kwa maana nyingine sio mke wake. Kitu ambacho hakikikuwa kweli.

Rejea: Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara. MWA. 20:2 SUV.

Jambo hili lilimfanya Mungu aingilie kati mwenyewe, ilibidi Mungu aongee na Abimeleki kwa ndoto, kumwonya kuhusu Sara. Kuwa huyo ni mke wa mtu, na mtu mwenyewe ni Ibrahim.

Rejea: Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. MWA. 20:3 SUV.

Abimeleki akamuuliza Mungu mbona aliniambia ni ndugu yangu? Na Sara mwenyewe alisema vivyo hivyo kuwa ni ndugu yake. Unaweza kumlaumu sana Ibrahim ila ukirudi kwenye uhalisia wa maisha yako utaona haya mambo tunayo sana.

Rejea: Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. MWA. 20:5 SUV.

Abimeleki wa watu hakuwa vile Ibrahim alifikiri, kumbe angemjibu ni mke wake wala asingenyang’anywa mke wake. Kwa Mungu alimjua vizuri Abimeleki, akamwondoa shaka kwa kumjibu kwenye ndoto.

Rejea: Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. MWA. 20:6 SUV.

Unaona hapo, sasa sababu aliyokuja kutoa Ibrahim kwanini alifanya hivyo, ni wasiwasi wake tu kufikiri watu wale hawakuwa na hofu ya Mungu. Kwa hawana hofu ya Mungu wangeweza kumuua kwa ajili ya mke wake.

Rejea: Ibrahimu akasema, Kwa sababu naliona, Yakini hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu. MWA. 20:11 SUV.

Mungu atusaidie sana katika hili, kuna mambo ambayo tunakuwa tunafikiri visivyo kabisa na kusababisha madhara ambayo tungeweza kuepukana nayo mapema.

Ipo haja kumweka Mungu mbele kwa kila hatua ya maisha yako, na kumwamini kuwa anaweza kukuokoa na jambo lolote lile litakalotupata kwenye maisha yetu.

Hofu na wasiwasi mwingi tuwaachie wale ambao hajamkubali Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao, lakini sisi tuliopata neema ya wokovu tuna kila sababu ya kutokuwa na wasiwasi/hofu kwa vitu ambavyo havipo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081