Wapo ndugu zetu tumetegana nao muda mrefu kwa heri na wengine sio kwa heri, wale ambao tumetegana nao kwa njia ambayo sio ya amani sana. Tunahitaji kurejesha mahusiano yetu kwa njia ambayo itakubalika.

Hatupaswi kuzitegemea tu akili zetu katika hili, tunapaswa kumwomba Mungu sana ili tukapate kibali kwao. Bila kupata kibali mioyoni mwao tunaweza kufanya mambo mazuri ila yasipate kupokelewa vizuri.

Tunapomwomba Mungu na akatupa kibali, zawadi inaweza ikawa njia nzuri sana kuwaunganisha tena na rafiki yako, mzazi wako, kaka yako, na dada yako.

Zawadi yako nzuri inaweza kuondoa mpaka aliokuwekea mzazi wako kutokana na jambo ulilolifanya nyumbani.

Hili huwa tunachukulia kawaida sana bila kujua ni moja ya njia ambayo inaweza kuleta suluhisho ambalo lilishindikana kabisa kupatikana.

Tunajifunza kupitia maandiko, tunaona Yakobo akiandaa zawadi ya kumpelekea Esau, na tunakumbuka Yakobo aliwahi ya mzaliwa wa kwanza kupokea baraka za baba yake.

Kitendo hicho hakikikuwa chema kwa Esau, Yakobo kutoonana na ndugu yake kwa muda mrefu. Alimwandalia ndugu yake zawadi nzuri, zawadi ambayo alijipanga nayo kisawasawa.

Rejea: Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng’ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako. MWA. 32:4‭-‬5 SUV.

Ni njia nzuri sana, hasa ukipata bali kutoka kwa Bwana Yesu, inaweza kuwaunganisha tena na ndugu yako ambaye mliwahi kupishana naye kipindi cha nyuma.

Hasa wewe ukiwa mkosa/mkosaji ukitumia njia aliyotumia Yakobo unaweza kufanya jambo la kuwaunganisha tena.

Mtu anaweza kukusamehe kwa kosa ulilomfanyia ila akakuwekea mipaka kwenye maeneo kadhaa, maeneo ambayo hawezi kukuweka kutokana na ulichowahi kumfanyia.

Lakini wewe unapaswa kufanya jambo la kuwaunganisha tena, ukimsikiliza Roho Mtakatifu atakupa wazo zuri sana la kuwaunganisha tena.

Unaweza kuandaa zawadi yako nzuri sana ila ukawa na hofu kubwa, ukashindwa namna ya kuiwasilisha au ukafikiri zawadi yako inaweza kukugharimu utakapoipeleka.

Rejea: Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana. MWA. 32:11 SUV.

Ndicho kilichokuwa kinamtesa Yakobo ambapo kinaweza kukutesa na wewe, lakini tunaona Yakobo alikuwa haachi kumwomba Mungu.

Na wewe ukiona una wasiwasi mwingi wa kudhuliwa vizuri kujipanga kiroho na kimwili, utamwona Mungu akikutetea.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest,
www.chapeotz.com