
Kuna watu wamepewa majina ambayo ni tofauti na ya wazazi wao waliowapa, na kama ndio wazazi wenyewe waliamua kumwita mtoto wao hivyo watakuwa na sababu maalum.
Yapo majina watu wamepewa, majina ambayo yanawatambulisha sifa yao njema, wapo watu wanaitwa makamanda wa Yesu. Ukimwangalia utaona jina lake linafanana na vile matendo yalivyo.
Wapo watu majina yao halisi yamefunikwa na sifa zao mbaya, utasikia yule fulani mlevi, yule kahaba, yule malaya, yule jambazi, yule tapeli, yule muongo na mengine mengi yanayoendana na hayo.
Ukifuatilia sana utakuta asilimia kubwa ya watu wana majina ambayo yanawatambulisha haraka, yanaweza yakawa majina mazuri au yanaweza yakawa mabaya.
Huenda hapo ulipo wamekupa jina la kudharauliwa jamii, badala ya kuitwa jina lako wanakuita jina lisilo lako na lenye sifa mbaya. Bora wangekuita jina lenye sifa nzuri inayokutambulisha matendo yako.
Kama uliitwa jina baya mfano wa yale niliyoyaorodhesha hapo juu, kuanzia sasa na kuendelea hutoitwa tena hilo jina.
Na hili lipo ndani ya uwezo wako, kazi yako ni moja tu, kukataa majina mabaya na kuamua kuchukua maamzi ya kumkiri Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yake.
Jina lako la awali linaweza kubadilika wakati wowote ukiwa umeokoka au ukiwa hujaokoka kabisa ukapachikwa jina lisilo lako.
Hili tunalithibitisha kupitia maandiko ya biblia, tunamwona Yakobo akipewa jina tofauti, jina ambalo lilikuwa jema sana.
Rejea: Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli. MWA. 35:10 SUV.
Chagua kuishi maisha yanayompendeza Mungu ili ujipatie jina zuri sana mbele za Mungu na wanadamu. Utashangaa ukipewa au ukipachikwa jina lenye sifa njema mbele za Mungu.
Usikubali kuendelea kuitwa majina ya hovyo, kataa kuitwa hiyo jina na uitwe jina lingine zuri, ipo gharama kubwa ila unapaswa kufahamu yote yanawezekana kwake.
Walizoea kukuita masikini, hawatakuita hivyo tena maana Mungu atakuwa ameufuta huo umasikini kwa kufanya kwako kazi kwa bidii.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com