Siku unaondoka nyumbani kwenu kwenda kutafuta maisha, uliondoka kwa furaha au kwa huzuni?

Siku unaondoka nyumbani kwenu uliondoka kwa hiari yako au ilikubidi uondoke kwa kulazimishwa na ndugu zako au wazazi wako.

Uliondokaje nyumbani kwenu, hilo ndio somo letu la leo, somo linalotufanya tufikiri tulipotoka huko na tulipo sasa.

Kwanini nimeanza kuuliza swali la uliondokaje nyumbani kwenu, kama uliondoka kwa misukosuko. Umeshasamehe hayo au bado umeshikilia moyoni mwako.

Huenda siku unaondoka nyumbani ulifukuzwa kama mbwa, lakini leo hii una mafanikio makubwa ambayo unaweza kumsaidia mtu.

Inatokea wale ndugu zako wa damu wanakujia kutafuta msaada wa chakula, na wewe unacho cha kutosha kabisa. Je, utaweza kuwasaidia chakula au utakuwa na uchungu nao moyoni mwako?

Tunajifunza kwa Yusuf, pamoja na kufanyiwa mambo mengi mabaya na ndugu zake, ndugu zake wale wale aliwapa chakula cha kutosha.

Sio hilo tu, aliwarudishia pesa zao ndani ya magunia yao, japo kuwa hawakuwa wanajua kama ndio Yusuf.

Rejea: Ikawa, tulipofika nyumba ya wageni, tukafungua magunia yetu, kumbe! Fedha za kila mtu zilikuwako kinywani mwa gunia lake, fedha zetu kwa uzani wake kamili; nasi tumezileta tena mikononi mwetu. MWA. 43:21 SUV.

Huyu ni mtu ambaye alifanyiwa mambo mabaya katika maisha yake, ambapo angeweza kukataa kuwapa chakula.

Wakati mwingine tunaweza kufikiri tulifukuzwa nyumbani vibaya, kumbe ilikuwa mpango wa Mungu tupitie njia hiyo ya kufukuzwa.

Tunaona hata ule upendo wake kwa ndugu zake ulikuwa  bado upo, inaonyesha wazi kabisa pale alipowaona hakuweza kuzuia machozi yake.

Rejea: Yusufu akafanya haraka, kwa sababu moyo wake ulimwonea shauku nduguye, akatafuta pa kulia, akaingia chumbani mwake, akalia humo. MWA. 43:30 SUV.

Haijalishi uliondokaje nyumbani kwenu, hupaswi kujenga chuki kwa wazazi wako, kaka zako, au dada zako.

Mungu kukutenganisha nao, yeye ndiye alijua maisha yako yajayo, huna haja kujenga chuki juu yao. Ukifanya hivyo utafarakana na Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com