Mtu anaweza akawa na maneno mazuri sana, maneno ambayo ni matamu sana, maneno ambayo yana ushawishi mkubwa, maneno ambayo anayesikiliza anatamani kuendelea kusikiliza zaidi.

Mtu mwingine anaweza akawa na mipango mizuri sana ya mdomoni, mwingine anaweza akawa na ahadi nzuri sana kwa watu.

Mtu mwingine anaweza akawa ni mwema kwa maneno yake, vile anazungumza unaweza ukasema huyu mtu ni mcha Mungu wa kweli haswa.

Wapo wengine ni wachapa kazi wazuri kwenye maneno ya midomo yao, vile anazungumza unaona vile alivyo mchapa kazi haswa.

Pamoja na hayo yote bado hatuwezi kumpitisha moja kwa moja kuwa huyo mtu ndivyo alivyo, maneno yake ya mdomoni hayawezi kutusaidia kumtambua huyo mtu.

Japo mtu hunena yaliyoujaza moyo wake, lakini nafasi ile ile wengine huitumia vibaya. Ukija kufuatilia vizuri utaona aliyokuwa anazungumza ni tofauti kabisa na matendo yake.

Sasa ili uweze kumtambua mtu ana tabia gani, ukiachana na maneno mengi ya kujisifia, au kujinadi, au kujisemea vizuri, au upole wake.

Mtu kama mtu utamtambua kwa matunda yake, matunda yake ni yale matendo yake yanayoonekana kwa watu/jamii.

Rejea: Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? MT. 7:16 SUV.

Vile vitu ambavyo anavifanya na vinaonekana au vinatokea, vile ambavyo anaishi na watu, hiyo ndio picha ya mtu alivyo moyo wake.

Hata kama atajaribu kuigiza, mwisho wa siku tutaona matunda ya yale aliyokuwa anafanya. Ikiwa alikuwa anafanya ubaya ila kwa maneno anaaminisha watu anafanya mazuri, uwe na uhakika kile alichokuwa anakipanda ndicho atakachovuna.

Siku zote mlimau huwezi kutoa matunda ya mapera, wala mti wa pilipili huwezi kutoa hoho, utatoa kile cha asili yake.

Rejea: Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu. YAK. 3:12 SUV.

Hata yule mtu anayesema amejazwa na Roho Mtakatifu, tazama matendo/matunda yake yanayoonekana kwa nje. Utajua huyo mtu amejazwa kweli au ni maneno tu.

Mtu mwaminifu kweli na yule mwaminifu wa kujisema na maneno, lakini kwenye uhalisia sio mwaminifu. Atajulikana kutokana matendo/matunda yake.

Hivyo ndivyo unaweza kumtambua mtu, unaweza kusikia mambo mabaya sana juu ya mtu fulani. Kama ni kweli utamtambua tu kwa matunda/matendo yake, na kama ni uongo napo utamtambua vile vile kwa matendo yake.

Hii ndio faida ya kusoma neno la Mungu kila siku na kutenga muda wa kutafakari yale uliyojifunza, unakuwa na maarifa ya kukusaidia kwenye maisha yako.

Hakikisha siku haipiti bila kusoma Biblia yako, kufanya hivyo inakufanya kiwango chako cha ukuaji kiroho unaongezeka kila siku.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.