
Maisha ya hapa duniani unaweza ukachagua mwenyewe unataka yaweje kwako, kwanini unaweza kuchagua. Kwa sababu Mungu amekupa uhuru wa kuchagua kuishi maisha ukiwa na Kristo au uamue kuishi bila Kristo.
Hata wahubiri wanaohubiri habari njema za Kristo, hamlazimishi mtu kuokoka, mtu mwenyewe anaokoka kwa hiari ya moyo wake.
Vile vile mtu akiwa hapa duniani anaweza kuchagua ni namna gani anaweza kuweka alama njema mbele za Mungu na watu pia anaoishi nao.
Huyu mtu sio kana kwamba atakuwa na mambo yake mwenyewe aliyoyabuni kutoka kichwani kwake, vile neno la Mungu linataka. Mtu akilijua na akaamua kuliishi kama linavyotaka, mtu huyo lazima afanikiwe.
Leo nataka nikutafakarishe kidogo au sana, umewahi kukaa chini na ukatafakari ni jambo gani mbele za Mungu ni alama kwako ya kukutambulisha kwake.
Sawa umeokoka hakuna anayepinga hilo, yapi ni matunda yako ya kuokoka kwako? Matunda ambayo hata yule asiyemjua Kristo anaweza kuyashuhudia kwako.
Kipi kitakufanya ukumbukwe na jamii inayokuzunguka, achana na watu wengine ambao wapo mbali nawe. Wale unaoishi nao katika mazingira yako, kipi kitakuwa ukumbusho wao kwako.
Wapo watakumbukwa kwa mabaya, huo ndio utakuwa ukumbusho wao kwa watu na mbele za Mungu. Wewe kama mwana wa Mungu aliye hai utakumbukwa kwa lipi mbele za Bwana?
Kornelio tunayemsoma kwenye Biblia yale matendo yake, sala zake na sadaka zake ndizo zilizomfanya awe alama njema.
Rejea: Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Matendo 10:4 SUV.
Kipi kwako kitakuwa ukumbusho wako mwema mbele za Mungu? Unaweza ukajifichia mahali na kusema mimi sina uwezo wa kuweza kumtolea Bwana sadaka kama za Kornelio.
Lakini napenda kukuambia hata kutoa muda wako mbele za Mungu ni sadaka mbele za Mungu, hata kufanya kwako usafi kanisani kwako kwa moyo wako wote ni sadaka yako.
Hata kukarimu wageni, ama watumishi wa Mungu wanaokuja kuhubiri habari za Yesu Kristo hiyo ni sadaka yako kwa Bwana.
Vipo vingi sana vya kukufanya uwe ukumbusho mbele za Mungu, ukumbusho ambao utakuwa duniani na mbinguni.
Bado hujachelewa ndugu yangu unayesoma ujumbe huu, unao muda mzuri wa kujitengenezea hazina yako njema. Ambayo itakutambulisha ukiwa duniani na utakapokuwa haupo duniani.
Hii ndio faida ya kulijua neno la Mungu, neno ambalo linakufanya uishi maisha ya tofauti na kawaida ya ulimwengu huu, maisha ambayo yanalenga mahali ambapo ni kusudi la Mungu kukuleta duniani.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.