Haleluya, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona leo tena. Kwa mazoea ya kila siku unaweza kuona ni jambo la kawaida kuamka na kulala, ila ukweli sio jambo la kawaida kabisa.

Mazoea haya yametufanya kwenda mbele za MUNGU kwa mazoea na desturi zetu ambazo tumejiwekea.

Hali hii imetuua wengi na kushindwa kuona ladha ya kuwa ndani ya WOKOVU, tumeona wokovu ni jambo la kawaida, tumefikia wakati hata tukisikia NENO la Mungu hatushtuki kabisa.

Sio kana kwamba tumeasi, ila ndani yetu tumekuwa sugu, usugu huu umezaliwa na mazoea ya dini/madhehebu yetu. Mtu yupo tayari kutetea na kunadi dhehebu lake, kuliko YESU Kristo.

Tumeona kujifunza NENO la MUNGU ni jambo la kawaida kawaida, hata unapomwambia mtu habari za kusoma NENO. Anakuona umekosa mambo ya kufanya, anakuona umekosa sera za kumweleza.

Ugonjwa huu umeendelea kututafuna kidogokidogo mpaka tumefikia hatua tumejaa hofu za maisha yetu, kwa sababu hatuna NENO la MUNGU mioyoni mwetu.

Tumekuwa watupu ndani ya mioyo yetu kiasi kwamba mtu anaweza kumtenda Mungu dhambi, na asione kwamba ametenda vibaya, kuona ametenda vibaya ungemwona akijuta kumkosea Mungu.

Kushindwa kusoma NENO la MUNGU ni tatizo baya kwa mkristo, lakini watu wamelichukulia kawaida kabisa. Wakati haikupaswa kuchukuliwa kawaida kawaida.

Ahadi zetu nyingi tumeshindwa kuzidai kwa sababu ya kutojua maandiko, hata tukijaribu kusoma NENO hatuzioni kwa sababu tunasoma ili tuonekane kwa wengine. Ila mioyoni mwetu hatuna kabisa nia ya dhati kujifunza NENO la MUNGU.

Utasema ina maana tangu nianze kusoma NENO, sijui ninachofanya? La hasha unaweza kuwa unajiona unajua ila nikupe zoezi moja. Nichunguze ndani yako, unajisikiaje unaposoma NENO la MUNGU, unajisikia kupata kitu cha kubadilisha maisha yako au unasoma kama jarida fulani.

Ingekuwa NENO la MUNGU linakuingia usingeshindwa KUSAMEHE waliokukosea, usingeng’ang’ania na usemi wa hutakaa uwasamehe waliokukosea.

NENO LA MUNGU lingekuwa linakuingia ndani yako; usingekuwa unatumia vilevi kwa kujiachia wakati unajua YESU Kristo amekataza.

NENO LA MUNGU lingekuwa linakuingia vizuri; usingeweza kulala na mume wa mtu ndani kwako ukijua ana mke wake nyumbani, usingeruhusu kabisa.

NENO LA MUNGU lingekuwa linafanya kazi ndani yako; usingekuwa na ujasiri wa kulala na wamama/wadada wa nje wakati umeoa, na umeacha mke wako ndani.

NENO LA MUNGU lingekuwa linafanya kazi ndani yako; usingeendelea kulala na wadada/wakaka kwa ujasiri wakati bado hujaoa. Usingekubali kuingia kwa mwanaume kufanya naye uasherati, usingekubali mwanamke kukuteka akili zako.

Huna NENO la Mungu ndani yako, umebaki na mazoea ya WOKOVU, ndani yako umeoza. Kubali kataa; umeoza, haiwezekani unasoma NENO unaona kila kitu kawaida kawaida.

Moja ya kujua NENO linagusa maisha yako, kuna maeneo utasoma mpaka unasikia kulia machozi. Unaona ulichokuwa unakifanya hakifai kabisa, unaona kanisa lilipofikia sio pa zuri, kwa kuona hivyo unajisikia ndani yako kutubu…ooh! Hata kama hujakosea wewe.

Sijui kama unanielewa ninachokisema hapa; kwanini huna hamu ya kusoma NENO la MUNGU? Kwanini unasoma NENO la MUNGU lakini ndani yako unajisikia mkavu tu wala hushtuki kitu chochote?

Umetekwa ndugu yangu, huna chako tena, umempa shetani nafasi kiasi kwamba amechukua kila kilicho chako, kuonyesha amekunyang’anya haki yako. Ni pale unavyopenda kufanya mabaya kuliko mazuri, huna hamu ya ibada ila una hamu na vitu visivyofaa.

Wengine wameingiziwa ratiba za kuangalia mechi, sijakuambia kuangalia mechi ni dhambi; ila mbona kuangalia mpira kumechukua nafasi ya MUNGU wako.

Utasema nafasi ipi hiyo? Hoja nzuri kabisa; mbona huna uwezo wa kuomba hata nusu saa ila una uwezo wa kuangalia mpira dk 90, nikiwa na maana ya saa moja na dakika 30.

Huna hamu ya kusoma NENO la MUNGU hata dakika 20 au 30, ila una hamu ya kuangalia mpira dakika 120 yaani mpaka zile za nyongeza.

Huwezi kusoma biblia, na huna muda kabisa wa kufanya hivyo ila upo kwenye magroup ya wasap, ukichati mambo yasiyo na faida kwako.

Umetekwa rafiki yangu, lazima ukatae hiyo hali, umeokoka sawa ila umebaki mkristo jina. Ndani yako huna ukristo ila umebaki ukristo wa mdomoni tu.

Unajiona wewe mwenyewe ulipo sio shwari, unaona kabisa wala huhitaji kufanyiwa uchunguzi, ndani yako unashuhudiwa kabisa hali sio hali.

Uamzi unao mwenyewe, unaweza kukataa hali hiyo kwa vitendo, hakuna atakayekuja na fimbo akuchape kama mtoto mdogo.

Mungu afungue ufahamu wako upate kuona biblia ni sehemu yako ya ratiba ya siku kuisoma.

Unapenda kuungana nasi group la Wasap, karibu sana tuwe pamoja kwa kutuma sms yako yenye majina yako kamili, kwenda namba hizo hapo chini. Hakikisha una nia ya kweli kusoma NENO la MUNGU kila siku, yaani ni kila siku isipokuwa jpili tu.

Leo tupo kitabu cha 1 Nyakati 17, tunaenda kusoma sura hii na kupata muda wa kutafakari, na kushirikishana yale tuliyojifunza kutoka kwenye sura hii.

Mungu akubariki sana.

Samson Ernest.

+255759808081.