Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupea ili kuendelea kumzalia matunda mema, kwa kuitenda kazi yake.

Jambo/kitu chochote kinapoanza kwa siku ya kwanza, huwa kinaanza kwa kasi kubwa sana. Wakati mwingine ukijaribu kukizuia kwa mbele, unaweza kukutana na shida, maana mwendo wake ni wakasi kubwa mno.

Jambo lenyewe ninalotaka kulizungumza hapa, ni usomaji wa NENO la MUNGU, wengi huanza kwa nguvu zote na nidhamu ya hali ya juu sana.

Kadri mtu huyu anavyoendelea kusoma NENO la MUNGU, ule usomaji wake alivyoanza nao mwanzo, huzidi kupungua siku hadi siku. Badala ya kuongeza usomaji wake, unashangaa unapungua kabisa.

Mazoea yamewarudisha wengi nyuma, shida ya mazoea ni hii; utafanya vitu kwa kuwa wewe una uzoefu nacho, na kwa kuwa ni kawaida yako kufanya. Hutokuwa na muda wa kuumiza kichwa namna gani ya kuboresha kile unafanya.

Mazoea hayawezi kukuletea maumivu hata usipofanya hicho unachofanya, wala mazoea hayawezi kukusukuma ufanye kile ulikianzisha kufanya pale unapojisikia kuchoka.

Wakati wale wanaofanya pasipo mazoea ya kawaida, wao hujisukuma zaidi kufanya hata kama mazingira yanakuwa magumu kwao, utawakuta wanafanya.

Naona bado hujanipata vizuri, iko hivi; mazoea ninayozungumza hapa ni yale mabaya yanayopoteza/yanayoua ufanisi wako, na kuchukulia kila jambo kawaida kawaida.

Mazoea yanaua ule msukumo wako wa asili na kuona ufanye, usifanye bado mambo yataenda tu. Unapofika hatua hii unakuwa mtu wa kawaida kawaida.

Ndivyo ilivyo siku za leo, tunashindwa kuwa bora kwa sababu ya kuingiza mazoea au tunaweza kusema ukawaida. Ukawaida huu umeturudisha nyuma wengi sana.

Lisha ya kila jambo unaloanza lina changamoto yake, tena unaweza kukutana na ugumu ambao hukuutengemea. Ila nikuambie kwamba ipo nguvu katika kusoma NENO la MUNGU.

Nguvu hii ndio inayotufanya tusonge mbele, jinsi unavyoongeza umakini na kuondoa mazoea katika usomaji wako wa biblia. Ipo kiu inazidi kuongeza ndani yako, maana unaelewa unachofanya si kwa sababu uonekane na wewe msomaji wa NENO, bali unajua katika kusoma kwako biblia kuna mwongozo wa maisha yako unapata.

Kujua tu hivyo, inakusukuma wewe kuondoa ukawaida kawaida wa kusoma NENO la MUNGU, ukawaida huu ndio unaotufanya tushindwe kuona nguvu za Mungu.

Ukawaida/mazoea yanasababisha tufanye ibada zisizo na uvuvio wa nguvu za Roho Mtakatifu. Maana utayari wetu wa kupokea jambo unakuwa hakuna.

Kuanzia sasa fikiri upya, jiulize kwanini huna msukumo wa kusoma NENO la MUNGU, na wakati siku za mwanzo ulianza vizuri. Na leo usome, usisome NENO wala hujisikii kupungukiwa kitu, jitathimini mwenyewe ni kitu gani hicho kama si mazoea yaliyozaa uvivu.

Kumbuka hakuna mtu atakuja kukushikia fimbo ya kukulazimisha urudishe ile kasi yako ya usomaji NENO, ni wewe pekee ndiye utakayeweza kujisimamia kwa kuamua.

Huenda unasoma ujumbe huu na hujawahi kabisa kutenga muda wako kwa ajili ya kusoma NENO la MUNGU. Hujachelewa, anza sasa, nasema anza sasa hivi, usijiambie ngoja nijipange.

Tumekosa dira ya maisha yetu kwa uzembe wa kutojua maandiko, tumeshindwa kujisimamia kwa kukosa maarifa ya NENO la Mungu, kwa kujipa muda kila siku wa kusogeza siku mbele.

Tumebakisha siku za jpili tu, muda mwingine tunajiona tumechoka sana, tunaamua kupumzika nyumbani siku za ibada.

Jpili yenyewe tunaingia ibadani huku tunaweza kazi zetu, biashara zetu, na familia zetu. Hata ule umakini unakuwa haupo kabisa.

Hebu amua kubadilika mwenyewe, kusoma NENO la MUNGU si kwa faida ya mwingine. Bali ni kwa ajili yako mwenyewe, ukijua NENO alafu likawa taa ya maisha yako, hiyo ni faida yako.

Mpaka hapa utakuwa umebadili mtazamo wako hasi, utakuwa umeondoa ule ukawaida/mazoea, na sasa unaenda kuanza upya usomaji wako wa NENO la MUNGU.

Kwa wale ambao tupo pamoja WASAP group, leo tupo katika kitabu cha 1 Nyakati 20, naamini kuna vitu umeanza kujiona vikibadilika kwako kupitia usomaji wako wa NENO la MUNGU. Usiache kujitathimini, hii itakufanya ujirekebishe pale ambapo unajiona haupo vizuri.

Umetamani na wewe kuwa pamoja na wenzako wanaojifunza NENO la MUNGU kwa kutafakari pamoja na kushirikishana yale waliojifunza. Unakaribishwa sana kwa angalizo hili, uwe umeamua kweli, uwe tayari kutenga muda wako, uwe mtu usiye na sababu sana, na uwe tayari kuwashirikisha wenzako ulichojifunza sura husika.

Umejipima umeona unaweza kufuata hayo yote, wasiliana nasi kwa sms, kwa njia ya wasap tu na si vinginevyo, kwa namba hizo chini.

Mungu ainue zaidi viwango vyako vya uelewa wa NENO LAKE.

Samson Ernest.

+255759808081.