MWONGOZO WA MAISHA YETU YA WOKOVU.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai sasa na hata milele, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa zawadi ya kibali, ili tuendelee kumzalia matunda mema kwa kuitenda kazi yake. Na nafasi nzuri kutengeneza mahusiano yako na Mungu pale ulipokosea ukarudi nyuma.
Yapo mengi tunayapata kupitia usomaji wetu wa NENO la MUNGU, mambo haya tunayoyapata ndio yanakuwa mwongozo wetu wa maisha ya KIROHO na KIMWILI. Hili jambo tunaweza kuliona ni jambo la kawaida na kulichukulia kwa kiwango kidogo sana, kwa kutoelewa kwetu.
Hakuna jipya chini ya jua, yote unayoyaona yanatokea sasa na hata yale yaliyopita miaka ya nyuma, na yatakayotokea miaka kadhaa ijayo. Yameandikwa ndani ya biblia iliyobeba maandiko Matakatifu.
Siku zote binadamu asili yake ni ubishi wa kutoamini mambo/jambo, na hili tunalithibitisha kwa Tomaso, rejea; Yohana 20:27. Ambapo ubishi ule mtu anakuwa nao si kana kwamba kwa sababu anaelewa sana la hasha! Kutojua kwake anataka kujiaminisha kuwa anajua kupita wengine.
Hili swala la kusoma NENO la MUNGU lazima tuambiane ukweli ili tuweze kuzishika amri za Mungu, ili tuweze kuelewa vizuri kwanini Mungu alituumba, ili tuelewe kwanini Mungu ameweka serikali inayoshughulika na mambo ya mwili. Na kwanini ameweka mpangilio wa kanisa linalomwabudu na kulisifu jina lake.
Nguzo iliyo kuu ni Neno la Mungu, vyote unavyoviona duniani vilifanyika kwa NENO, na NENO huyo ni Mungu mwenyewe, na huyohuyo NENO akafanyika mwili ili sisi tupate kukombolewa katika dhambi.
Utajuaje sasa mwongozo wa maisha yako ikiwa hutojua NENO la MUNGU? Utajuaje haki zako za msingi ikiwa huna NENO la MUNGU ndani yako? Utajuaje Mungu ni mwenye pendo kuu juu ya maisha yako ikiwa huna neno moyoni mwako?
Ufike wakati ujihoji ndani ya moyo wako hata pasipo kumshirikisha mtu mwingine yeyote, wakati mwingine tumeshindwa kushinda changamoto ndogo ndogo kwa sababu hatujui tufanye nini. Wakati mwingine tumeingia kwenye dhambi kwa sababu ya ujinga wetu wenyewe.
Pamoja na kujua pasipo Mungu hatuwezi kuenenda sawasawa na mapenzi ya MUNGU, bado tumeendelea kukalia uzembe wetu uleule. Wakati upo uwezekano wa kila mmoja wetu kutenga muda kwa ajili ya kusoma NENO la MUNGU, tukapata muda mzuri wa kutulia mbele za Mungu tukitafakari yale tuliyojifunza.
Tunajiona tupo bize kiasi kwamba hatuwezi kushika biblia, mtu huyuhuyu anayesema yupo bize utamkuta anaongea na simu nusu saa mpaka lisaa limoja, ambapo ukizifuatilia hizo simu hazina matunda yeyote kwake.
Mtu yule yule anayekuambia yupo bize utamkuta kwenye makundi akipiga story, mwingine utamkuta yupo tu anazunguka kwenye mitandao ya kijamii. Kama sio pepo hili, ni nini hili linalomsumbua mtu huyu.
Kile ambacho kinatuongoza maisha yetu KIROHO na KIMWILI, tunakipuuzia, lakini vile ambavyo haviwezi kutuongoza ndio tunavizingatia sana. Tufike wakati tushtuke ni kitu gani kinatufanya tushindwe kusoma NENO la MUNGU.
Siku za jpili tunapitishwa mistari mifupi mno, wakati mwingine unaenda kanisani bila hata biblia. Una baki kumsikiliza tu mchungaji, mchungaji akishuka madhabahuni na wewe unaachana naye pale pale. Mtu akija akakuuliza leo umefundishwa neno kutoka kitabu gani, unabaki unamwangalia tu maana hukumbuki chochote.
Neno la Mungu lina utamu wake ndugu yangu, ukilijua tu hilo haijalishi utakuwa kwenye wakati gani, lazima utapenyeza kila njia upitie maandiko machache ya kuushibisha moyo wako.
Kila utakaposoma NENO la MUNGU utajisikia vizuri sana kwa sababu ipo nguvu ndani ya NENO, neno linaonya, neno linajenga, neno linakuongoza, neno linaleta hekima, neno linakupika kiasi kwamba unatoka umeiva kisawasawa.
Utaachaje kutembea kifua mbele kwa ujasiri ukiwa unajua BABA yako anakuwazia yaliyo mema, utachaje kuwa na furaha wakati unajua wa kumtwisha mizingo yako mizito ambayo inataka kukuelemea, ni yeye Mungu.
Leo hii wanaume wameshindwa kujua wajibu wao kama baba, kwa wake zao na watoto wao, kwa kutojua neno la Mungu, kabisa. Leo hii wanawake wanatafuta haki sawa kwa sababu NENO la MUNGU halimo ndani yao, na waume zao wamekuwa sababu ya hayo yote.
Ndugu zangu tupende Neno la Mungu maana limejaa ahadi zetu, tutakuwa watendaji wa NENO kwa sababu tunalijua. Hatutaweza kuwa watendaji wa NENO ikiwa ndani yetu halimo. Hebu tuamue kubadilika kuanzia sasa hivi, anza kutenga muda wako kwa ajili ya kusoma NENO.
Huwezi kujisimamia peke yako katika azimio hili la usomaji neno la Mungu kila siku, usiogope kuhusu hilo, tumekuandalia utaratibu mzuri wa group la wasap ambalo lina mkusanyiko wa watu wenye nia moja ya kujifunza neno la Mungu kwa bidii sana. Nawe unahitaji watu wa kuambatana nao, basi nikualike katika group letu kwa kuniandikia ujumbe kwa njia ya wasap kwa namba za simu hizo chini.
Tulio pamoja katika hili zoezi la maisha yetu yote hapa duniani ya kulisoma NENO, leo tupo kitabu cha 1 Nyakati 24, tunaenda kusoma na kushirikishana yale tuliyojifunza katika sura hii. Nikuombe sana wewe ambaye unapendezwa kuwa nasi katika hii safari, uamue kweli kujitoa kwa kutenga muda wako wa kusoma NENO LA MUNGU.
Nakutakia maamzi mema ambayo hutokuja kujuta maishani mwako.
Samson Ernest.
+255759808081.