NIMESOMA SANA BIBLIA IMETOSHA.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, habari za leo ndugu yangu katika Kristo, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona.

Kukua kiroho ni kama mtu aliyekula leo vizuri na kesho tena akala vizuri, alipoanza kunawiri afya yake, akaona haina haja tena kula vizuri. Bila shaka mtu yule afya yake itaanza kuwa mbovu kwa sababu suala la kula vizuri linapaswa kuwa la kila siku.

Huwezi kula leo chakula vizuri alafu matokeo ya kula vizuri yalipoanza kuonekana, ukaona uachane na kula vizuri. Hapo utakuwa unakaribisha matatizo mengine, maana unapaswa kula vizuri zaidi pale unapopaswa kufanya hivyo.

Kula vizuri ni kuujengea mwili wako afya njema, inakusaidia wewe kuepuka magonjwa mengine ambayo husababishwa na kula ovyo, au kutokula kabisa vyakula fulani.

Lazima tukue kwenye akili zetu na kutoruhusu uzembe wa aina yeyote ututawala ndani mwetu, itatusaidia sana kukataa mawazo hasi yanayoweza kutupotosha ili tuache kile tulianza nacho.

Nayasema haya si kana kwamba nataka nikufundishe mambo ya kula chakula kizuri, japo ni vizuri pia ukazingatia hilo ili kuwa na afya njema. Lengo langu haswa kukuandikia haya, ni kuona baadhi yetu huwa tunaanza kuridhika na hatua ndogo sana tunazofikia katika maisha yetu.

Wengi wetu akishaona amesoma biblia kwa mfululizo wa vitabu kadhaa labda akafika kiwango cha kumalizaAgano jipya au Agano la kale,anaona imetosha hana haja tena ya kuendelea kutenga muda kwa ajili ya NENO.

Tabia hii imeendelea kuwaingia hata yule ambaye alijitoa akasoma labdaMwanzo, Kutoka, Walawi, Hesabu, na kumbukumbu. Anaona amesoma sana biblia haina haja ya kuendelea kusoma NENO tena.

Ikiwa tuliona kuwa huwezi kula leo vizuri baada ya muda fulani ukaona matokeo ya kula vizuri, matokeo yale mazuri hayawezi kukufanya ukasitisha kula vizuri. Zaidi utaongeza bidii zaidi ya kula vizuri na kuepuka vyakula vinavyoweza kukuletea matokeo yasiyo mazuri.

Sawa na mtu anayefanya mazoezi ya mwili, hawezi kufanya sana leo alafu kesho akasema imetosha maisha yangu yote, mazoezi niliyofanya jana yatanisaidia kuniletea uimara wa mwili wangu. Ni kitu ambacho kinapaswa kuwa mwendelezo wa kila siku, ndio maana tunasema kuujenga mwili kiroho au kimwili ni suala la kila siku.

Bila shaka unaanza kunielewa ninachomaanisha hapa, huwezi kusoma biblia mpaka hatua fulani ukaona huhitaji tena kusoma NENO la MUNGU, huko ni kujidanganya ndugu yangu. Lazima ufike wakati ukue kiufahamu, usiwe mtu wa kufikiri kawaida kawaida ukaishia hapo, fikiri kwa viwango vya utu uzima.

Kwanini urudi nyuma kwa ridhiko ndogo kiasi hicho, kwanini uone hujisikii kula tena chakula cha roho yako. Kuna shida ambayo umeiruhusu mwenyewe ikutawale, shida yenyewe imekuja kwa kuingiza mawazo potofu.

Tuache kujidanganya, tuache kujazwa maneno hasi na watu ambao wao wanasubiri siku za jpili ndio wanashika biblia zao, kwa mwendo huo hatutafikia lengo ambalo tulilianzisha. Kujijua wewe kama wewe kwanini unasoma biblia, itakuongezea nguvu za wewe kusonga mbele.

Tusipoambiana ukweli kwa sababu sisi tumeokoka, tutapotezana kabisa, tunapokosea eneo fulani lazima tuwekane sawa bila kujali ukweli huo unagusa kiasi gani mioyo yetu. Shida yetu tunapenda kuzungukana pembeni na kuanza kusema kwa wengine wakati tatizo linaendelea kubaki pale pale.

Nimeamua kukunyokea wewe mhusika, sijataka kuzunguka pembeni, nimekuja moja kwa moja kwako kukuambia hivi, tabia ya kuridhika na mafanikio madogo uache. Hata kama ungemaliza kusoma biblia nzima, bado utapaswa kutenga muda wa kusoma kwa umakini mwingine zaidi kwa sababu bado hujahitimu WOKOVU.

Kuna vitu utajisahau na kuanza kuenenda ndivyo sivyo, ila kupitia utaratibu wako wa kujisomea NENO la MUNGU kila wakati, litakusaidia kujua ulipo bado unaenenda sawa au umeacha njia iliyo sahihi.

Shika hili sana, na acha kabisa kuridhika ridhika, kufanya hivyo unajipelekea kujidumbukiza shimoni mwenyewe. Pigana vita vya imani mpaka unaondoka hapa dunia, tunastafu kazi/utumishi baada ya muda fulani. Ila hatustafu WOKOVU, hili ni jambo la maisha yako yote hapa duniani.

Kila siku yako mpya unayopewa kibali na Bwana, iwe siku yako ya kuendelea kukua kiroho, usibaki palepale kwa kujiona umefika viwango vikubwa uhitaji tena kujifunza. Utapoteana vibaya hutaaamini kilichokutokea, umeamua kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo, amua haswa.

Bidii yako ya kumtafuta Mungu, na kuyaishi yale anayokuelekeza uyaishi, lazima utavuna matunda ya utii wako.

Baada ya kusoma haya, labda umejisikia na wewe kuwa pamoja na wenzako wanaojifunza NENO la MUNGU kila sikuWASAP GROUP,unakaribishwa sanaikiwa umeokoka kwa sharti hili moja. Lazima uwe na nia/kiu ya kusoma NENO la MUNGU kila siku na kutushirikisha kile ulichojifunza.

Unaona hilo sio shida kwako, nikikukaribishe sana kwa kundikia ujumbe wenye majina yako kamili kwenda wasap namba hiyo chini nitakayoitoa. Angalizo, tumia wasap na si sms ya kawaida.

Leo tupo katika kitabu cha 1 Nyakati 25, tunaenda kusoma na kushirikishana TAFAKARI zetu kwa yale tuliyojifunza.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu.
www.chapeotz.com
+255759808081.