HATUA MOJA NI BORA SANA.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona siku hii njema. Hakuna aliyetoa rushwa ili aione leo, bali kwa neema tu tumekuchaguliwa kuifikia leo tena. Tunapaswa kuitumia leo kutenda mema na kujirekebisha pale tulipoenda kinyume na Mungu wetu.

Tabia ya kudharau hatua ndogo katika kufikia lile jambo ambalo mtu analihitaji kulifikia katika maisha yake, imepelekea wengi wetu kusubiri muda mrefu ili wajiandae vizuri. Matokeo yake maandalizi yale hajawahi kuzaa matunda ambapo mpaka leo bado wanasubiri kuanza na hatua kubwa kuliko ndogo.

Heri kuwa na subira huku ukiendelea kufanya kidogokidogo kile ambacho unakitaka kiwe sehemu ya maisha yako, ni sawa na mtoto anatamani darasa la saba wakati hataki kuanza na darasa la kwanza. Wakati mwingine analazimika kuanza na darasa la awali(chekechea) ili kuandaliwa vizuri kuingia darasa la saba.

Tunafahamu sio mambo yote utapaswa kuanza na hatua ndogo, ila fahamu hatua ndogo ndio zinakutambulisha wewe ni mtu wa aina gani. Na una kiu kiasi gani ya utendaji wako katika kufikia malengo yako, utaona wengi waliofikia hatua fulani kubwa walianza na vitu vya chini sana. Ambapo vitu vile walifanya vizuri vikawapelekea kujulikana na wengi, na kupelekea kuwagusa wengine zaidi, katika kuwagusa kule ndipo kuliwafanya wao kufikia hatua kubwa.

Hili jambo tunaweza kuliangalia kimwili kabisa, tukaliona vizuri jinsi lilivyokaa. Bila shaka nafasi nyingi za viongozi wanaotuongoza, zilizaliwa na hatua ndogo sana kwenye nafasi walizowekwa, walifanya vizuri kwenye nafasi zao za awali mpaka kupelekea kupandishwa nafasi za juu zaidi.

Haitoshi kwa viongozi wetu wa serikali, tunaona hata kwenye biashara zetu tunazoanzisha kwa hatua ndogo, na kuzingatia mambo madogo madogo ambavyo wateja wanahitaji kutoka kwetu. Ndio wanaofanikiwa sana kwa uvumilivu wao kuliko wale wanaosubiri wawe na mitaji mikubwa.

Tunaweza kuona pia kwa wale ambao wanatamani kufikia katika uhuru wa kifedha, badala ya kusubiri wawe na nafasi kubwa ili wapate pesa nyingi. Wao huanza kujiwekea Akiba kidogokidogo kwa kile wanachopata kidogo, baada ya muda fulani watu hawa utawakuta katika hatua fulani kubwa sana.

Nimejaribu kukupitisha mbali kidogo ili unielewe vizuri faida ya kuanza na hicho ulichonacho, hapo ulipo unaweza kuanza na hatua ndogo sana kufika eneo unalohitaji kulifikia. Hatua hizi ndogo sio kana kwamba ni rahisirahisi sana ndio maana nazisisitiza sana kwako.

Hatua ndogo pia zina changamoto zake nyingi, ambapo unapaswa kuwa na uvumilivu ulioambatana na nidhamu kwa safari uliyoanzisha. Pasipo kuwa na nidhamu utaona hicho kidogo hakina sana maana kwako, maana hakina matokeo mazuri ya haraka kama ulivyotarajia wewe.

Wakristo wengi wanatamani kusoma NENO la MUNGU, ila kinachowakwamisha na kukata tamaa mapema. Anaona akianza kusoma NENO leo akutane haraka haraka na yale aliyoambiwa, kumbe anahitaji nidhamu na bidii katika kutenga muda wake kila siku kuyapitia maandiko Matakatifu.

Tuseme labda ulikuwa unafanya mambo yasiyompendeza Mungu, ukaambiwa kwa Mungu kuna kila kitu, ukaamua kwenda mbele za Mungu kuomba haraka haraka akusaidie ila haupo tayari kulikiri jina lake wala kuacha dhambi. Utaonekana kituko kwa kusahau kila kitu kina kanuni zake, mtoto anaanza kutambaa ndipo utamwona anaanza kusimama kwa kusaidiwa, mwisho anaanza kutembea kwa kujitegemea mwenyewe.

Nayasema haya kwa sababu ninafuraha mbele za Mungu, tulianza kusoma kitabu cha 1 Nyakati sura 1 mpaka leo tunaenda kuhitimisha sura 29. Tulianza kwa hatua ndogo sana ambazo kwa mtu ambaye anahitaji mafanikio ya haraka haraka asingeona tunachofanya.

Hatua hizi ndizo zimetufanya tuanze kitabu cha Mwanzo, taratibu taratibu tumejikuta tumefikia kitabu cha 1 Nyakati. Usifikiri labda tumeruka vitabu vingine ndio maana tumefikia hapa tulipo leo la hasha! Tumeenda hatua kwa hatua, hizo hatua zikatufikisha hapa leo.

Usione shida kuanza kusoma NENO la MUNGU, usiangalie kesho ambayo unafikiri utakuwa na nafasi ya kutosha sana, angalia hapo ulipo utakuwa na dakika hata 30 za wewe kutulia mbele za Mungu ukasoma NENO lake. Anza na hizo dakika chache, taratibu unavyoendelea utaona hili zoezi linakuingia na linaanza kuwa tabia yako.

Acha kujidanganya utaanza kesho, kesho haijawahi kufika, acha kuanza kusoma NENO la MUNGU alafu unaachia njiani. Dhamiria kutoka ndani ya moyo wako bila kusukumwa, ukianza umeanza haijalishi mazingira yakoje utafanya tu kwa sababu umeamua kweli.

Nikualike siku ya leo CHAPEO YA WOKOVU wasap group, tukajifunze NENO la MUNGU kwa pamoja. Ambapo leo tunaenda kusoma kitabu cha 1 Nyakati 29. NENO LA MUNGU ni kwa faida ya maisha yako mwenyewe.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.