Jitafakari Bidii Yako Ya Usomaji Neno La Mungu Ikoje hadi sasa.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, nafasi nyingine tena tumeipewa na Mungu wetu tukaitumie vyema kumzalia matunda yaliyomema. Haijalishi nyakati gani tunapitia, tunapaswa kulitukuza jina la Yesu Kristo maana yeye hutupa kushinda siku zote.
Leo tuangalie eneo mhimu sana ambalo wengi wetu hulisahau na kuliona la kawaida, wakati lina faida kubwa sana kwa mtu yeyote anayetamani kusogea hatua fulani kimaendeleo. Yawe maendeleo ya kimwili au kiroho, kwa anayejua safari anayoendea inahitaji uwe umejipanga kisawasawa, hawezi kutembea kizembe kizembe.
Jambo lolote linapoanzishwa na mtu, huanza kwa kasi kubwa sana, kasi hii huleta matumaini mazuri ya kufikia malengo yale aliyoyatarajia. Lakini siku zinavyozidi kwenda mtu huyu anavyozidi kukutana na pongezi za kile anachofanya, wengi wao huanza kulewa sifa na wachache wao huitumia fursa ile kujiimarisha zaidi.
Wengine pia wanapokutana na changamoto za maisha katikati ya safari yao, huanza kujisikia kuchoka na kutamani kuacha kabisa kile alichokianzisha. Na wachache katika hao huona changamoto ni moja ya sehemu ya maisha, na wanazichukulia changamoto zile kama darasa kwao la kufanikiwa zaidi lile wanaloliendea mbele yao.
Kila mmoja mmoja anajua namna anavyoyatazama mambo, unaweza kuteswa sana na jambo lakini mwenzako anaona ni kitu cha kawaida. Ambacho kinapita tu kama mambo mengine yaliyopita, sio kana kwamba huyu anavyoyaangalia haya mambo kirahisi, yeye hapitii hiyo hali la hasha! Anapitia sema jinsi anavyoyatazama mambo ndio inamsaidia yeye kusonga mbele bila tatizo.
Safari yeyote ya mafanikio ya KIMWILI au KIROHO ina changamoto zake kubwa tu, usipojua namna ya kukabiliana na changamoto hizo. Nakwambia utavunjika moyo wa kusonga mbele, hasahasa safari ya mtoto wa MUNGU, ina vipingamizi vingi sana maana shetani hataki ufanikiwe. Kufanikiwa kwako utamharibia kazi zake nyingi kwa watu wake anaowatumikisha.
Ndio maana vita kubwa ya shetani anahakikisha anakuzuia usisome NENO la MUNGU, unaweza kujitahidi kusoma lakini ukawa huoni kitu unachopata kwenye biblia. Lakini kwa mtu aliyedhamiria atahakikisha anaondoa kila udhaifu kwa maombi, atahakikisha anamshirikisha Roho Mtakatifu ahusike katika kumsaidia kuelewa NENO la MUNGU.
Baada ya kufahamu hayo, tuje sasa kwenye kutenga muda mwingine wa kujitafakari wewe mwenyewe, ulipo katika usomaji wako wa NENO la MUNGU unapanda juu au unashuka chini.
Naomba usipuuze hili ni mhimu sana sana, lazima ukae chini ujiulize ile kasi yako ya mwanzo ya usomaji wa Neno la Mungu bado ipo palepale ama imepungua. Kama ipo palepale je unaona mabadiliko ndani yako? Kama unaona mabadiliko je unapanda viwango zaidi au unazidi kushuka viwango.
Imekuwa kawaida kabisa kumwona mtu anakuwa na bidii kubwa ya usomaji NENO la MUNGU, ila ukija kumrudia baada ya muda fulani. Unakutana naye akiwa hana tena ile bidii aliyokuwa nayo mwanzo, na kama ana bidii basi utamkuta anafanya kwa mazoea yasiyo na mabadiliko yeyote, kuonyesha huyu mtu anabadilika siku hadi siku jinsi anavyozidi kukua KIROHO.
Vizuri sana ukajijengea utaratibu wa kujitathimini wewe mwenyewe, unapojitathimini inakupa nafasi ya kujijua ulipo unahitaji kuongeza bidii wapi, na utajua upunguze vitu gani ambavyo vinakukwamisha usifikie malengo yako.
Kukua kiroho hupaswi kuendelea kubaki vilevile miaka nenda rudi, tuposemaSOMA NENO UKUE KIROHO, tunatazamia jinsi tulivyokuona mwezi ulivyopita ukiwa viwango fulani KIROHO tusikuone upo vilevile mwezi huu. Jambo lingine zaidi usionekane unashuka bali uonekane unapanda juu kiwango cha kumjua Mungu zaidi.
Itakuwa haina maana unasoma NENO la MUNGU kila siku, mpaka sasa bado huwezi kusamehe, hapo lazima ujiulize una shida gani ili uifanyie kazi haraka.
Tenga muda wako kujitafakari wewe mwenyewe, najua umezoea kutafakari Neno la Mungu kila siku, leo nakutaka ujitafakari wewe mwenyewe. Utashangaa unaona vitu vingi sana vya kujirekebisha wewe kama wewe.
Kukaa chini kwako na kujitafakari, unaweza kujikuta huwa unampa Mungu muda mdogo sana wa kulisoma NENO lake na kulifakari. Utakapojua hilo kuna vitu utaviona huwa vinakula muda wako lakini havina maana sana kwako. Utapogundua vitu vinavyokula muda wako, utaviacha na kuviondoa kwako, kufanya hivyo utakuwa umesogea hatua kubwa sana kwako KIROHO.
Usipuuze vitu vidogovidogo vinavyokula muda wako mwingi, hivyo vitu ndio vinakuzuia wewe uwe na muda mdogo wa kushindwa kutafakari NENO la MUNGU kwa kina. Utakapoamua kuondokana/kuepukana navyo, utakuwa umefanya kitu cha msingi sana kukuwezesha wewe kusogea zaidi hatua ya mbele.
Bila shaka umeona jinsi gani kutenga muda wako wa kujithamini ulivyo na faida kubwa, usiache kufanya hivyo. Umejifunza hili na umeona linafaa sana kwako, anza kulifanyia kazi leo hii.
Kama bado hujajiunga na group la wasap Chapeo Ya Wokovu unakaribishwe sana, kama umeamua kuwa miongoni mwa marafiki wenye nia moja ya kujifunza NENO la MUNGU. Hakikisha huna visingizio vya kukufanya usisome NENO la MUNGU, upo tayari kujiunga andika ujumbe wako wenye majina yako kamili kwenda +255759808081(tumia wasap tu).
Leo tupo katika kitabu cha *2 Nyakati 4*, hii ni kwa wale ambao tupo pamoja katika kusoma NENO la MUNGU kila siku.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.