Chagua Mtu Wa Kujifunza Mambo Mazuri Kwake.
Haleluya, nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema Mungu ametupa kibali cha kuiona. Kila mmoja wetu anapaswa kuweka alama njema katika siku ya leo.
Tunaendelea kushirikishana mbinu mbalimbali za namna ya kukua kiroho, kwa kusoma NENO la MUNGU, na kuyaishi yale tunayojifunza. Unaposoma Neno la Mungu, bila kusukumwa na mtu yeyote utakuwa mtu wa maombi, utakuwa mtu wa shukrani, utakuwa mtu wa ibada, utakuwa mtoaji, utakuwa mtu unayeweza kusamehe na kuachilia vitu vilivyokuumiza.
Kuna vitu vingi sana unavivuna kutokana na usomaji wako wa Neno la Mungu, usione kusoma biblia labda ni kwa ajili ya kukusaidia maisha ya kiroho tu la hasha! Neno la Mungu linakujenga mpaka maisha yako ya kimwili, unakuwa imara kiasi kwamba watu wanaokuzunguka watashindwa kukuelewa jinsi unavyoendesha maisha yako.
Leo nataka kukumbusha jambo la msingi sana katika kukua kwako kiroho, katika maisha kila mmoja ana mtu anayeweza kuambatana naye. Kila mmoja ana rafiki yake ambaye yupo tayari kusimama badala yake na yule rafiki yake asijue kama kuna mtu anampenda, na kumfuatilia kwa karibu kiasi kile.
Nguvu hii ya urafiki inaweza kuletwa na vitu vingi, unaweza kumpenda mtu kwa jinsi anavyoendesha maisha yake kimwili/kiroho, unaweza kumpenda mtu kwa jinsi anavyoendesha biashara zake. Unaweza kumpenda mtu jinsi anavyoishi na mke/mume wake, na watoto wake.
Unaweza kumpenda mwalimu kwa ufundishaji wake, unaweza kumpenda mtumishi wa Mungu jinsi anavyohubiri NENO la MUNGU. Kumpenda huku mtu sio lazima yeye ajue kama unampenda na kumfuatilia sana.
Upendo wa mtu huyu unayemfuatilia kwa karibu, unakufanya ndani yako uanze kuibua vitu vilivyokuwa vimelala kwako. Mtu huyu anaweza kukuonya kwa njia ya mazungumzo yake ukamwelewa haraka sana kuliko mtu yeyote. Haijilishi mliokuwa mnamsikiliza mpo wangapi ilimradi wewe unamkubali na kumwelewa, utakuwa na vitu vingi vya kufanyia kazi.
Kumkubali mtu fulani haikufanyi usijufunze kwa wengine, hii inakupa wewe nafasi ya wewe kuwa imara katika kile unachoona kinaendana na vitu fulani unavyopenda kuwa navyo au kuviishi.
Nikupe faida kadhaa za kuwa na mtu unayependa kusoma makala zake au vitabu vyake au kusikiliza mafundisho yake; faida moja wapo atakuhamasisha kufanya vizuri zaidi ya ulivyokuwa unafanya awali, faida ya pili utakuwa mtu wa kupenda kubadilika haraka kutokana na makosa uliyokuwa unafanya bila wewe kujielewa.
Kuna vitu unaweza kuwa unafanya usijielewe kama unakosea, ila wewe ukawa unajiona upo sahihi, kadri unavyozidi kujifunza kwa wengine. Inakupa nafasi ya kujua hatua zipi uchukue ili uweze kuepukana na jambo fulani ama hatua zipi uchukue uweze kufanikiwa katika safari yako uliyoianza.
Katika usomaji wako wa Neno la Mungu, chagua mtu wa kumfuatilia kwa Karibu sana, mtu huyu awe na sifa ya bidii na sio mvivu, mtu ambaye hazuiliwi na sababu ndogondogo za kushindwa kusoma NENO la MUNGU.
Utakapompata atakuwa anakujibu maswali yako mengi sana ya changamoto unazokutana nazo kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu. Pale mlipokwamishwa mahali na jambo fulani, utakapomkuta yeye amepata muda wa kusoma Neno la Mungu alafu wewe ulishindwa kufanya hivyo, utaondoka na hatua kubwa sana kiroho.
Wakati mwingine watu wanaweza kuwa wanasingizia hawana muda wa kusoma NENO la MUNGU kutokana na kubanwa sana na shughuli. Lakini wamesahau kuwa huwa wana muda fulani wanauchezea bila wao kujua, ila kupitia mtu uliyemchagua kumfuatilia wewe. Utajikuta unapata muda mwingi sana wa kutulia mbele za MUNGU kwa ajili ya kusoma neno lake.
Chagua leo rafiki yako wa kiroho anayependa kusoma NENO la MUNGU, usipate shida ya kuanza kujiuliza utamwambiaje au utamfikiaje. Hilo lisikupe shida, nilikueleza mwanzo sio lazima yeye ajue kama unamfuatilia, cha mhimu kuwa karibu naye kwa njia unayoona ni rahisi kwako.
Nakuhakikishia hutaona hasara bali utaona mafanikio katika hili, na ile tabia ya kuanza kusoma NENO la MUNGU na kuishia njiani, utaona ikikoma kabisa. Hakikisha unalifanya hili zoezi kazi, la kuchagua mtu wa kumfuatilia, yeye anafanyaje mpaka afanikiwe kusoma NENO la MUNGU kila siku.
Wapo marafiki wengine wengi wanapatikana CHAPEO YA WOKOVU wasap GROUP, kama unapenda kuungana nao na una nia ya kweli kusoma NENO la MUNGU. Hakikisha simu yako ina uwezo wa wasap, kisha tuma ujumbe wako wenyejina lako kamilisio moja, kwenda +255759808081.
Leo tupo katika kitabu cha *2 Nyakati 5,* hii ni kwa wale waliopo wasap group, tunaenda kusoma hii sura na kushirikishana yale tuliyojifunza katika sura hii.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.