Usifikirie Sana Hatua Ndogo Unazopiga Fikiria Safari Iliyo Mbele Yako.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za leo mwana wa Mungu, siku nyingine tena Bwana ametuzawadia. Nasi ni miongoni mwa watu waliochaguliwa kuwepo siku ya Leo, tunamrudishia Mungu wetu sifa na utukufu.

Karibu tushirikishane habari njema za kukusaidia kusonga mbele katika usomaji wako wa Neno la Mungu, kupitia makala hii unaenda kuondoka na kitu cha kukuvuta mbele na si kukurudisha nyuma.

Kila mmoja wetu ameanza kuelewa kuwa hatua moja katika kuyaendea mafanikio, sio ya kudharau hata kidogo. Kama umekuwa ukifuatilia jumbe zangu, umeona nikielezea sana kuanza na hatua ndogo zitakufikisha mahali pa kubwa sana.

Tumeliona hili likizaa matunda mazuri kwa wachache wetu, na limeonekana ni jambo la mateso kwa wengi wetu. Maana mtu alitarajia akianza kusoma NENO la MUNGU, atakutana na raha siku zote, kwa kutokutana na changamoto zozote za maisha. Badala yake changamoto zimemkumba na ameona aachane kwanza na habari za kusoma NENO la MUNGU mpaka pale atakapokuwa huru.

Tunavyofikiria kusoma NENO la MUNGU huenda tunafikiri tofauti sana ndio maana tunaona tujipe sababu za kushindwa kuendelea. Lakini tungejua umhimu wa Neno la Mungu kama tunavyojua umhimu wa kula chakula cha mwili, tungekuwa mbali sana.

Mtu anaweza kukuambia asubuhi sina pesa ya kununulia chakula, ila mpaka kufikia jioni utamkuta ameipata hiyo pesa ya kununua chakula. Ataumiza kichwa na atafanya kila linalowezekana ili asilale njaa, ikitokea amelala njaa kesho yake asubuhi sana utamwona ameamka na wazo jipya la namna ya kupata pesa za kununulia chakula.

Kwa mazoea ya kawaida unaweza usilione hili kama lina uzito mkubwa sana, ni sawa na wakati ule ulikuwa unaumiza kichwa sana ukiishiwa kalamu ya kuandikia. Lakini leo hii hilo halikupi shida kwa sababu tayari umejijenga kimaisha na sio mwanafunzi tena.

Umeona ni jinsi gani kuna vitu huwa tunavipuuzia pale vinapoleta ugumu, ila vipo vitu vingine huwa tunahakikisha tunavipata kwa gharama yeyote ile hata kama hatuoni mlango mzuri wa kutokea.

Tunapoanza safari kwa hatua ndogo tunazoanza nazo, tunapaswa kuziheshimu hizo hatua kwa kuhakikisha tunafikia kusudi tulilolifuata. Tunapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu na kufikiri zaidi kama mtu anayetafuta njia ya kupata chakula cha mwili.

Anayetafuta pesa ya kununua chakula hafikiri njaa inavyouma, anafikiri jinsi gani ataokoa uhai wake. Mtu huyu yupo tayari kufanya kibarua chochote aokoe uhai wake na familia yake, haijalishi hiyo kazi ni ngumu na ina ukubwa kiasi gani, ataifanya tu.

Ikiwa tunaweza kupigania miili yetu kiasi hichi, kwa kujua madhara ya kutokula ni kujisababishia matatizo. Iweje leo hatuoni umhimu wa kulisha utu wetu wa ndani Neno la Mungu, tungejua madhara yanayopatikana kwa kutokuwa na NENO la MUNGU mioyoni mwetu. Lazima tungetafuta kila njia ya kuhakikisha tumepata muda wa kusoma Neno la Mungu.

Shida haipo kwenye kusoma biblia sura moja kila siku, shida ipo kwenye uelewa wetu, hebu we fikiria umewahi kununua mchele kilo 10 ukazipika zote wakati mmoja alafu upo peke yako? Kitu ambacho hujawahi! Itakulazimu kupika kidogo kidogo kutokana na hitaji lako mwisho unajikuta umezimaliza hizo kilo 10.

Utakapoacha kufikiria kusoma NENO la MUNGU hatua kwa hatua ni mateso, ukaanza kufikiria faida inayopatikana kwenye hatua zako za usomaji Neno la Mungu kila siku. Kuna hatua kubwa sana utakuwa umevuka na hutokubali kukwamishwa na jambo lolote mbele yako.

Kuanzia sasa anza kufikiria faida inayopatikana kwa usomaji wako wa Neno la Mungu, anza kujua umhimu wa kulitafakari Neno la Mungu. Umeshajua huwezi kumaliza biblia yote siku moja alafu ukasema umeshiba NENO huhitaji tena. Tumeona anayetafuta chakula akipata kilo 10 za mchele hawezi kuzipika siku moja zote zikaisha, hata zile kilo 10 atakapozimaliza hatasema imetosha kula, ataenda tena kuzitafuta zingine.

Hujakosea kabisa kuwa na tabia ya kila siku kusoma neno la Mungu, tabia hii unaifanya maeneo mengi sana ya maisha yako. Sema kwenye kusoma NENO la MUNGU ulikuwa bado hujajua vizuri namna ya kuiweka, ila kwa maneno haya utakuwa umeelewa vizuri.

Safari iliyo mbele yako hutoweza kuifikia kwa kudharau hatua hizi ndogo, na hatua hizi ndogo hazitakufikisha popote kama hutojua umhimu na madhara yatokanayo na kutosoma Neno la Mungu.

Umeshajua hatua hizi na utamani kuungana na ndugu zako katika Kristo, katika kusoma NENO la MUNGU kwa pamoja na una nia ya kweli. Unakaribishwa sanaCHAPEO YA WOKOVUwasap GROUP, hakikisha unafuata hatua hizi, andika jina lako kamili kwenda0759808081. Tumia njia ya wasap kunitumia ujumbe wako wa majina kamili na si njia nyingine.

Leo tunaenda kusoma na kutafakari Neno la Mungu katika kitabu cha *2 Nyakati 6,* unakaribishwa sana ndugu yangu.

Nakushukuru sana kwa muda wako, Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.