Usikubali Kuachwa Nyuma Na Wenzako Mlioanza Nao Safari Pamoja.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za leo ndugu yangu, siku nyingine tena Mungu ametupa kibali cha kuiona. Najua sio wote waliofikia leo, ila mimi na wewe tumeiona siku ya leo, vyema tukaitumia siku hii vizuri kumzalia Mungu matunda yaliyo safi.

Yapo makundi ya watu unaweza kuambatana nayo, yasiwe makundi mazuri yanayokufikisha mahali pazuri, bali yakawa sababisho la wewe kupotea kabisa. Pia yapo makundi mazuri ya watu unaweza kuambatana nayo, yakawa sababisho la wewe kufikia malengo yako mazuri.

Leo nataka tuzungumzie sana kundi la watu wazuri ambao wanasafiri kwa lengo moja la kufanikiwa jambo fulani, ambalo hilo jambo lina manufaa kwa wote mlio ndani ya safari hiyo.

Unapo chagua kufuatana na kundi la watu wanaosoma NENO la MUNGU, usikubali kuachwa nyuma hatua nyingi sana, vyema ukapaza sauti pale unapotaka kukwama ili wasikuache sana.

Unapoachwa nyuma bila sababu ya msingi sana, unaruhusu uzembe kukuvaa, utapowaona wamekuacha hatua nyingi mbele, na ukawa unawaona kwa mbali sana. Kitakachofuata kwako ni kuacha kufuatana nao baada ya kuona huwezi kuwakimbilia kutokana na umbali waliokuacha nao.

Kuzuia tabia hii ya uvivu wa kutosoma NENO la MUNGU, jitahidi sana uwe mstari wa mbele, ukiona mbele panakushinda sana, kuwa katikati, ili wa mbele, na wa nyuma, na wa katikati, na wa pembeni, wawe ndio nguzo yako.

Haijalishi wao wana mwendo wa kasi sana kuliko wewe, tumia mwendo wao kukufikisha kwenye malengo yako, kukufikisha kwako ni jinsi wanavyokuvuta mbele maeneo mbalimbali. Ukiwa huelewi sehemu watakusaidia, ukiwa unaona jambo fulani ni kwazo kwako, utaona wao wanaendelea kusonga mbele pamoja na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo njiani.

Usikubali wakuache, usinyamaze kimya unapokwama, sema shida iliyokukwamisha, unaposema tu kuna eneo unafungua mlango mwingine wa kutokea.

Tunajua kuanzisha jambo jipya katika maisha yako, sio jambo rahisi kabisa ila kumbuka yupo atutiaye nguvu, hebu we fikiria tangu uzaliwe hujawahi kuwa na utaratibu wa kujisomea Neno la Mungu kila siku. Ulichozoea kwako ni kwenda na biblia siku za ibada tu, tena wakati mwingine unatokea kazini moja kwa moja unasahau kubeba biblia.

Alafu leo hii anatokea mtu anakwambia unapaswa kusoma NENO la MUNGU kila siku, ukiangalia jamii inayokuzunguka, haina tabia ya kufanya hicho unachoambiwa. Lazima fikiri vizuri ili usije ukaanza alafu ukaishia njiani, maana kelele za kushindwa zitakuwa nyingi kuliko za kushinda.

Pamoja na hizo kelele nyingi za kushindwa, nilikuambia kundi ulioamua kuambatana nalo kwa ajili ya zoezi hili la kila siku, kundi hili litakufanya uwe na nguvu za kuendelea kusoma NENO la MUNGU kila siku. Kila utapojihisi kuchoka, utakapowatazama wao, utajisikia ukipata nguvu za kuendelea mbele.

Shida itakuja pale utakaporuhusu hali yeyote ya uzembe kwa kujiona umetosheka na huna haja tena ya kuambatana nao, nakwambia ukijitahidi sana ni zile siku za mwanzoni wakati bado una kumbukumbu za zoezi mliokuwa mnalifanya. Baada ya hapo unaweza kurudi kulekule pa zamani wakati unashika biblia siku za ibada tu.

Unaweza kusema hakuna ulazima wa kuwa na marafiki wenye nia moja, je wakati unasema hivyo umeweza kusoma biblia yako kila siku au umesema hivyo ila husomi kabisa biblia yako, unasubiri mpaka siku za ibada.

Kama hujaweza kusoma NENO la MUNGU, basi unahitajika kuachana na makundi yasiyoweza kukusukuma kusoma Neno la Mungu. Kila mmoja anatamani kufikia eneo fulani katika maisha yake, sasa unapotumia muda mwingi kuwasikiliza wale wasio na lengo moja na wewe, inakupa wakati Mungu kwako kufanikiwa.

Usitazame nyuma idadi iliyoshindwa alafu ukavutiwa nao, na wewe kubaki nyuma kama wao, tazama mbele walioshinda hata kama idadi yao ni ndogo, haohao katika udogo wao, na wewe tamani kuwa miongoni mwao.

Walioshindwa wasiwe faraja kwako, bali walioshinda ndio wawe nguzo yako ya kuelekea ushindi wako. Tunasoma habari za Ayubu zinatutia moyo kwa sababu alishinda majaribu, na si kwa sababu alishindwa majaribu.

Ninapokuambia usikubali kutengana na kundi la washindi, nakwambia kitu halisi. Maana walioshindwa hawana maneno mazuri ya kukufanya na wewe ushinde, lazima watakujaza maneno hasi ya kila namna ya wewe kutoweza kufanikiwa.

Chagua leo kuambatana na kundi wasiokubali kurudishwa nyuma kwa hali yeyote ile, kataa kuwasikiliza na kuambatana na kundi lililokata tamaa. Bali uwe sababu ya waliokata tamaa kuinuka tena baada ya kukuona wewe umefanikiwa kwa lile waliosema haliwezekani.

Unaweza kuungana na wenzako wanaohimizana kusoma NENO la MUNGU kila siku kama ulikuwa bado hujaungana nao, kundi hili la watu wanaojifunza Neno la Mungu lipo kwa njia ya WASAP GROUP. Ili uweze kuwa nao pamoja, ni lazima uwe umedhamiria kweli kusoma Neno la Mungu bila kutanguliza visingizio. Unapenda kuwa miongoni mwa kundi hili, tuma sms yenye jina lako kamili kwenda 0759808081, tumia wasap tu kutuma ujumbe wako.

Leo tupo katika kitabu cha *2 Nyakati 7*, ambapo tunaenda kusoma sura hii na kupata muda wa kutafakari na kushirikishana yale tuliyojifunza katika sura hii. Hii inakufanya kuwa na kumbukumbu nzuri kwa yale uliyojifunza, vilevile inakufanya uelewa wako kuwa mpana zaidi kwa kusoma TAFAKARI mbalimbali za wengine.

Nakushuru sana kwa muda wako.

Ndugu yako katika Kristo,
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.