Ujumbe unapokugusa Ukajisikia Ndani Yako Kuchukua Hatua Jenga Utulivu Kwanza Ujue Kama Kweli Umehamasika.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, jina lenye nguvu na uweza wa mambo yote, si lingine bali ni jina la Yesu Kristo. Siku nyingine tena Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona, ni fursa kwetu kwenda kumzalia matunda yaliyo mema, na kuweka alama njema katika maisha yetu ya kiroho na kimwili.
Karibu tushirikishane mambo machache ya kujengana kiroho katika safari yetu ya maisha ya wokovu. Yapo mambo mengi ambayo huwa tunahamasika sana yanapogusa mioyo yetu, hakuna mtu anayetusukuma kuhamasika. Ila kutokana na uzito wa ujumbe husika, na ukweli wa maneno tuliyoambiwa, tunajikuta tunajiona tunapaswa kubadilika na kuchukua hatua stahiki.
Wengi wetu mhamasiko ule, huwa unadumu muda ule ule tulioambiwa au muda tuliposoma ujumbe fulani. Ila baada ya muda mfupi kuisha tunaona hilo jambo tulilosikia au tulilosoma, tunaliona halina maana tena kufanyiwa kazi kama tulivyojiambia tutafanya.
Unaweza kuona watu wengi wanaweza kusikia mahubiri wakaokoka haraka haraka, ila baada kuondoka eneo la mkutano. Wanaenda kudumu ndani ya wokovu wiki moja tu, anaona maamzi aliyochukua ya kuokoka sio sahihi. Utashangaa imekuwaje, ila huo ndio ukweli kwamba ameona kuokoka ni utumwa. Maana hapati tena ule uhuru wake aliozoea kuwa nao siku zake za kutenda dhambi.
Unaweza kuona pia katika maisha yetu ya kawaida, mtu anaweza kupata semina ya ujasiriamali, mtu yule akatoka pale ana hamasa kubwa sana ya kufanya jambo fulani alilopata wazo kichwani. Ila mtu yule anaanza kidogo tu, anakutana na changamoto mbili tatu, anaona bora kuachana na jambo hilo.
Unaweza kuona pia katika usomaji wa NENO la MUNGU, ambalo ndio lengo langu kuu la kuandika ujumbe huu. Wengi sana ukiwaeleza habari za kusoma NENO la MUNGU, watahamasika sana sana na usipokuwa haraka kuwasikiliza mnaweza kugombana nao. Ila baada ya muda fulani ile hamasa yao inakata, na ukimuuliza kwanini husomi tena biblia atakupa sababu nyingi mno mpaka utashangaa.
Moja ya sababu hizo ni nakuwa bize sana, sina muda mzuri wa kusoma NENO la MUNGU, sielewi ninaposoma biblia. Tukirudi upande wa pili wa huyu mtu unakuta yupo mitandao ya kijamii, anachati na watu wasap, anasoma jumbe mbalimbali mitandaoni ila inapofika kusoma biblia yupo bize.
Mwingine anaweza asiwe na sababu hizo zote, akawa hajisikii tu kusoma NENO la MUNGU, hana sababu ya kukueleza sana kwanini hasomi. Ila ndani yake hana msukumo wowote wa kutaka kujifunza Neno la Mungu, hili ni tatizo ambalo anapaswa kulikataa mwenyewe kwa maombi.
Leo nataka tuliangalie sana hili la kuhamasika alafu baadaye mtu anarudia maisha yake ya awali. Kitu kinachotufanya tushindwe kuendelea mbele ni kuchukua maamzi bila kuhesabu gharama ya lile tunalolitaka kulifanya au kulianzisha. Unapoanza jambo lolote unapaswa kukaa chini uhesabu gharama, ikiwezekana pata picha kubwa ya mbele. Ukishaipata anza kuona namna gani utapambana na changamoto utakazokutana nazo, na jua njia zipi sahihi za wewe kupitia pale utakapoona njia zingine zimezibwa.
Unapopiga hesabu hizo, inakufanya uwe imara kifikra, uwe mtu ambaye utaweza kusimamia maamzi yako bila kuyumbishwa na mtu mwingine yeyote. Lakini ukikurupuka kuanza jambo bila kuhesabu gharama matokeo yake huwa sio mazuri sana kama hukijipanga.
Huenda unasoma ujumbe huu na upo miongoni mwa watu walioanza kusoma NENO la MUNGU, lakini uliishia njiani maana yake hukuweza kuendelea mbele. Unapaswa kukaa chini tena ujue sababu gani haswa iliyokufanya usisome Neno la Mungu, ambalo ni taa/tochi ya maisha yako kiroho na kimwili.
Huenda umesoma ujumbe huu ukasikia msukumo ndani yako wa kuanza kusoma biblia, na unatamani kuungana na wenzako wanaosoma Neno la Mungu kila siku kupitia group la Wasap. Nakushauri ukae chini kwanza uhesabu gharama, vizuri sana kuchukua hatua sasa bila kusuburi kesho, ila usipokaa chini ujiulize kama kweli umemaanisha kufanya kile ulichoamua, utajikuta utarudi nyuma tena.
Sio rahisi ukajua kila changamoto utakayokutana nayo, ila utapokaa chini ukajitafakari, inakupa nguvu wewe kuwa na maamzi, na ujasiri wa kusonga mbele hata unapokutana na changamoto. Maana tayari ulishaiandaa akili yako kukabiliana na vizuizi utakavyokutana navyo mbele ya safari.
Tabia ya kususa susa kwa mtu anapokutana na changamoto fulani, mara nyingi mtu huyu ana utoto ndani yake, na hajajipanga vizuri japo ana nia kabisa ya kufanikiwa kwa kile amekianzisha. Watu hawa wanahitaji sana kuwa na watu watakaoelewana nao vizuri, ili wawasaidie kufikia malengo yao.
Kila mtu anahamasika maeneo fulani katika maisha yake, ila nakusihi sana uwe na muda wa kutulia, ili uipe nafasi akili yako ujue kama kweli upo Tayari au ulihamasika tu hapo, na ikaishia ivyo. Hili sio kusoma NENO la MUNGU tu, hata katika maisha yako ya kawaida, uwe mwangalifu sana unapo hamasika ndani yako.
Nakukaribisha sana wewe unayependa kuungana na wenzako wanaosoma NENO la MUNGU kila siku, umehamasika na umefikiri vizuri, na umeona ni jambo zuri, na la mhimu sana katika maisha yako. Unachotakiwa kuwa nacho ni simu yenye Application ya Wasap, kisha unanitumia sms WASAP yenye jina lako kamili kwenda0759808081. Narudia tena hakikisha upo tayari kusoma NENO la MUNGU kila siku, maana nitakusimamia kuhakikisha unafanya hivyo kweli.
Leo tupo katikakitabu cha 2 Nyakati 8,tunaenda kusoma sura hii na kushirikishana TAFAKARI zetu kwa yale tuliyojifunza. Usipange kukosa hii, tenga muda wako mapema usome sura hii, kisha upate muda wa kutafakari yale uliyosoma.
Nakushukuru sana kwa muda wako, nikutakie siku njema iliyozungukwa na ulinzi wa Mungu.
Ndugu yako katika Kristo,
Facebook; Chapeo Ya wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.