Kufanikiwa Hatua Moja Isikupumbaze Ukaacha Kwenda Hatua Nyingine Zaidi.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, aliyeshinda kifo na mauti, aliyebeba dhambi zetu zote, aliyejitishwa kila aina ya mateso yetu. Kupitia msalaba wake Yesu Kristo, umetufanya kuwa huru kwelikweli, ametutoa gizani, na sasa tunaitwa wana wa nuru.

Karibu tuendelee kushirikishana maneno yenye kukujenga kiroho ili uendelee kukua zaidi ya hapo ulipo, hatua uliyonayo sasa inapaswa kuimarishwa zaidi, na kusogea hatua nyingine zaidi kiroho. Na si kudumaa eneo hilohilo kila mwaka, vyema viwango vyako vya kiroho viendelee kuongezeka siku hadi siku, jinsi unavyozidi kumjua Mungu.

Unapofanikiwa hatua moja ifurahie ila isiwe kitanzi kwako, kushindwa kusogea hatua ya pili, na hatua ya tatu, na hatua zingine mbele zaidi jinsi Mungu atakavyokujalia uzima wake. Lakini kama utapiga hatua moja ukabaki kujisifu nayo bila kuongeza bidii ya kwenda hatua ya pili. Mwisho wake unaweza kujikuta umeipoteza hata hiyo hatua moja uliyokuwa nayo, kwa uzembe ambao ulipaswa kuepukana nao mapema.

Ukweli inatupasa kufurahia hatua zetu tunazofanikiwa kuzifikia kwa bidii zetu, ila hizo hatua zisipokuwa chachu za sisi kusonga mbele zaidi. Itazidi kuhesabika uharibifu kwa sababu hatusogei mbele wala hatukui zaidi.

Tuseme labda una mtoto wako uliyemzaa, alivyoanza kujitegemea kukaa mwenyewe bila kushikiliwa, hiyo hatua uliifurahia sana, ilivyofika hatua ya kutambaa ndio ilikufanya uibue furaha nyingine zaidi. Sasa shida ikaja pale mtoto wako atakapozidi kutambaa tu bila kuanza kusimama wala kutembea kwa miguu yake. Badala ya furaha ile ya mwanzo kuendelea ilipotea kabisa, na kugeuka mzigo mzito kwako.

Nazungumza kusogea hatua, wengi sana tumepotea eneo hili katika maisha yetu ya kimwili na kiroho. Wengi walivyofika viwango fulani kiroho walijiona wamemaliza kila kitu na kuacha kumtafuta Mungu kwa bidii, badala yake wamezidi kupoa zaidi kiroho, na kusahaulika kama waliwahi kuwa wa moto zaidi.

Nafikiri nazungumza kitu ambacho unakielewa katika mazingira yako ya kila siku unayoishi, kama huelewi vizuri, naomba Roho Mtakatifu akusaidie sasa uelewe ujumbe huu unakutaka uchukue hatua gani. Mungu anapotuambia iweni hodari na moyo wa ushujaa, uhodari wetu hauwi siku moja tu bali unapaswa kuwa zaidi na zaidi.

Nasema hivi, askari imara ni yule anayejiimarisha zaidi kimazoezi kila siku, hata kama anaelewa jana alishinda vita vikubwa. Hiyo haiwezi kumfanya apumzike tu na kuwa mlegevu kimwili, atahakikisha anajimarisha zaidi kiulinzi.

Nilikutolea mfano wa mtoto anavyokua na unavyoweza kufurahia ukuaji wake, umeona kila hatua anayoendelea kukua mtoto utaifurahia. Ila shida inakuja pale atakapokwama kwenye hatua fulani, kama alikuwa anatamka mama kwa shida fulani, na katika kupata shida kule inaweza iligeuka kichekesho. Mbaya ni pale atakapoendelea kutamka mama kwa shida bila kubadilika, hapo badala ya kicheko itabadilika huzuni utakopogundua mtoto ana matatizo ya kuongea.

Hebu na wewe ujenge tabia ya kutamani kukua zaidi, utamani kuongezeka viwango vyako zaidi vya kiroho. Usibaki tu na hatua za jana, tamani kuongeza hatua nyingine zaidi ya kumjua Mungu. Usomaji wako wa Neno la Mungu uonekane tofauti na jana, maana yake uelewa wako uzidi zaidi na zaidi ya ulivyoanza mwanzo.

Usipokuwa na kiu ya kusogea zaidi hatua zingine, utajikuta unakosa hamu ya kuendelea mbele zaidi, utajikuta unaanza kutamani kuacha ile safari uliyoamua kuianzisha. Usiruhusu uzembe huu ukuvamia alafu mwisho ukupoteze kabisa.

Tamani kila siku kujiona wa tofauti katika usomaji wako wa Neno la Mungu, tamani kuona matunda zaidi ya unavyoendelea mbele kusoma Neno la Mungu, tamani kuona viwango vyako vikiimarishwa kila unaposoma sura mpya ya kitabu. Kutamani huku kuna kupa uzito zaidi wa kwenda mbele zaidi ya wengine, inakufanya ujitafute mwenyewe bila kutafutwa na mtu.

Tunaweza kukupigia kelele za kila aina kama hutaki kusogea hatua nyingine, tutakulazimisha na utasogea kidogo tu, alafu unarudia yaleyale uliyopigiwa kelele. Inahitaji juhudi zako, watu watajitahidi kukusaidia lakini usipokuwa na mwitikio wako binafsi wa kuufanya msaada ule kusogea hatua fulani, utabaki vilevile kila siku.

Furaha yako izidi kuwa zaidi pale unapofika hatua fulani, iwe chachu yako kufika hatua nyingine zaidi, mafanikio yako isiwe shimo lako la kukuzika usijulikane tena. Hii italetwa na juhudi zako za kila siku kujitahidi kusogea hatua nyingine mbele.

Nakukaribisha sana tujifunze NENO la MUNGU kwa pamoja, unapenda kuungana na wenzako wanaojifunza Neno la Mungu kila siku, utawapataCHAPEO YA WOKOVU wasap GROUP,ni wewe kuamua kweli kutoka ndani ya moyo wako kujifunza Neno la Mungu. Kuungana nao tuma jina lako kamili kwenda0759808081(tumia wasap tu kunitumia ujumbe wako).

Leo tunaenda kujifunza Neno la Mungu kutoka kitabu cha 2Nyakati 9, tunaenda kushirikishana mambo mhimu tuliyojifunza katika sura hii. Nikuombe sana uliweke mstari wa mbele hili suala la kusoma Neno la Mungu, pata muda wako wa kusoma NENO la MUNGU, utaona mafanikio makubwa sana KIROHO.

Nakushukuru sana kwa muda wako, nikutakie wakati mwema.

Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.