Unaowaamini Watafanya Vizuri Zaidi Wanaweza Kutumika Kukuvunja Moyo Pale Watakapofanya Kinyume Na Matarajio Yako.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku ya leo umeianzaje ndugu, umeianza na kugombana na watu waliokukosea jana au umeamka na hamu ya kuitafuta amani. Vigumu kumtafakari Mungu tukiwa ndani ya hasira na kutosamehe waliotukosea, kwa hiyo nakusihi sana utafute amani ndani ya moyo wako kwa kuwaachilia wote waliokukosea.

Kila mmoja ana watu wake anaotarajia wawe vizuri zaidi katika mambo ya Mungu, anapokuta kinyume chake, inaweza kumletea shida ambayo asipokuwa makini. Shida ile inaweza kumfanya aanze kuchukulia mambo ya Mungu kawaida kawaida.

Kukua kiroho kuna hatua nyingi sana, unaweza kukutana na changamoto kadhaa katika safari yako. Usijue kuwa zina mchango mkubwa sana wa kukuvunja moyo wa kushindwa kusonga mbele Zaidi.

Kila mmoja amejifunza sana kwa watu mbalimbali wanaosema, fuatana na watu waliofanikiwa nawe utafanikiwa, huu usemi ni ukweli sehemu kubwa sana. Ila shida itakuja pale wale waliofanikiwa wakawa wanafanya vitu kwa kawaida sana, na wengine wakawa wanafanya vitu kwa bidii sana.

Hapa unapaswa kuwa na kipimo cha marafiki hawa waliofanikiwa, sio kila aliyefanikiwa anaweza kuwa mfano wa kuigwa kwako. Wengine wanaweza kutumika kukuvunja moyo usijue kama ni wao wametumika katika hilo.

Wengi wetu tunatamani kufikia kiwango fulani kiroho, tunapoambiwa tunapaswa kuwa wasomaji wa Neno la Mungu, alafu ukakutana na mtu unayemwamini katika mambo ya Mungu. Akawa hasomi Neno la Mungu kama ulivyotegemea, usipokuwa makini anaweza kuwa mlango wa wewe kuvunjika moyo.

Kuna rafiki yangu mmoja anampenda Mungu sana, na yupo makini sana kusoma NENO la MUNGU, na anafuatilia kwa makini sana mafundisho ya NENO la Mungu. Akanifuata na kuniuliza swali ngumu kidogo, akaniuliza mtumishi naomba unisaidie, huyu si mchungaji?(akamtaja jina) Mbona haonyeshi kuwa yeye ni mchungaji kwa jinsi anavyotoa TAFAKARI yake ya Neno la Mungu?

Kwa kuwa namwelewa sana ni mtu makini, alinifanya nitafakari kwa dakika kadhaa kwanini hili jambo limemuumiza kiasi kile, na kumfanya ashindwe kuvumilia mpaka akaniuliza. Nia yake haikuwa mbaya nia yake ilionyesha ameshangazwa sana na jambo ambalo hakulitegemea kuliona kwa mchungaji yule.

Nilichoweza kumwambia ni kwamba, asijifunze kwa wale wasioendana na matarajio yake hata kama anawaamini wangefanya vizuri zaidi kutokana na ngazi fulani walizonazo. Bali ajifunze kwa wale wanaoendana na matarajio yake katika kukua kwake kiroho, yaani ajifunze kwa waliofanikiwa kwenye eneo analotaka kufanikiwa.

Huenda huyu ndugu ametuwakilisha wengi sana ambao tuna maswali mengi kuhusu hili, ila nikuambie tu kitu hiki nilichoanza nacho mwanzo. Ulikuwa na matarajio fulani kwa mtu unayeamini ana hatua fulani kiroho alafu ukakutana na kinyume chake, isikufanye wewe ukaacha kuendelea kuwa na bidii ya kumtafuta Mungu.

Hiyo changamoto itazame kama moja ya fundisho lako la kuelewa baadhi ya mambo, sivyo yalivyo kama ulivyotarajia yawe. Zaidi endelea kuweka juhudi kwa kuhamisha watu wengine wa kujifunza kwao.

Suala la kumjua Mungu katika viwango fulani unavyotaka wewe kufikia, linahitaji sana bidii yako iliyoambatana na nidhamu yako binafsi. Vinginevyo utasema ngoja niwe mtu wa kusoma Neno la Mungu kila siku, utaanza kweli vizuri tena kwa bidii. Lakini baada ya siku kadhaa mbele utaishia njiani, ukiulizwa sababu haswa ya msingi iliyokufanya uache kusoma Neno la Mungu unakuwa huna.

Haijalishi kuna watu unawaamini sana na unawajua wana viwango fulani vya kumjua Mungu, kama hawana kitu ambacho unataka kujifunza kwao. Bora kuondoa wazo la kujifunza kwao usije ukamkosea Mungu wako, kwa kitu ambacho kilikuwa hakina ulazima sana kungangana nacho.

Fahamu hili litakusaidia sana, jifunze kwa wale wanaoendana na malengo yako, nimekuambia hata kama kuna watu ulikuwa unajua kabisa unaweza kujifunza kwao. Ukienda kwao kwa undani ukakosa cha kujifunza hilo lisiwe sababu ya kukuvunja wewe moyo, heshima yao kwako iendelee vilevile. Ila tafuta mtu mwingine wa kujifunza zaidi kile unachokitaka kiwe kwako kwa ubora zaidi.

Endelea kuongeza viwango vyako vya kusoma NENO la MUNGU, kwa kupata muda zaidi wa kutulia mbele za Mungu kwa kufakari yale uliyojifunza. Utajikuta una hatua kubwa sana kiroho ambapo utaanza kuona baadhi ya maeneo katika maisha yako yanabadilika na kuwa imara zaidi.

Tunaendelea kujifunza Neno la Mungu, leo tupo katika kitabu cha *2 Nyakati 12*, pata muda mzuri wa kusoma Neno la Mungu. Hakuna majuto ya kupoteza muda wako katika hili, Zaidi ipo faida kwa waliomaanisha katika hili.

Nakushuru sana kwa muda wako, nakutakia wakati mwema, kumbuka kujifunza ni kila siku ya maisha yako yote.

Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.