Jitengenezee Kanuni Za Kujibana Mwenyewe Na Zikubali Hizo Kanuni Ulizojitengezea Kabla Hujaanza Kuzitendea Kazi.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, habari za leo ndugu yangu, ni siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa nafasi tuendelee kumzalia matunda yaliyo mema. Vyema kila mmoja akaitumia siku hii vizuri kuzalisha kitu chema ambacho kitakuwa alama nzuri katika maisha yake.

Ukiamua kufanya jambo katika maisha yako, vyema ukajitengenezea utaratibu mzuri ambao hutoweza kuuvunja kamwe. Utaratibu huo unaweza kutokana na kanuni/sheria ulizopewa/ulizopangiwa ili uzifuate, kama unakubaliana na mtoa kanuni, iwe katika kundi, au iwe katika familia, au iwe katika ofisi. Unapaswa kuzijua hizo kanuni, ukishaona upo tayari kuendana nazo, unachotakiwa kufanya ni kurudi kwako binafsi kujiwekea mikakati yako ili uweze kuzifuata kanuni/sheria hizo zilizowekwa.

Mungu anaheshimu sana mapatano yenu yenye nia ya kumletea utukufu yeye, usipoyakubali yale mapatano mliyowekeana. Hutoweza kufika mbali utaona yale mapatano yamekuwa kama adhabu kwako, wakati ni kwa ajili ya faida yako.

Unaweza kuujua umhimu wa kuamka asubuhi na mapema, na ukapata somo la faida za kuamka mapema. Labda tuseme mmepatana kila siku mtakuwa mnaamka saa kumi na moja kamili alfajiri, mnapopanga wawili au zaidi. Itategemea sana wewe umelikubali na kulifanyia kazi kweli au unaweza ukapuuzia kwa sababu kila mmoja anaishi kivyake hata usipoamka hawataweza kukuona.

Umeona hapo kanuni/mapatano yenu yanategemea sana wewe, mnaweza kukuambiliana jambo fulani, wenzako wakalifanyia kazi na wewe ukalishindwa kwa sababu hukujiwekea nidhamu ya kulitimiza lile jambo.

Wakati bado mtoto mzazi wako alikufundisha namna ya kula, alihakikisha anakusimamia upata chakula, lakini baadaye ulivyopata akili ulikuwa unadai mwenyewe chakula kwa kujua umhimu wa kula. Huku ukijua ukivunja kanuni ya kutokula, unakufa, kwa hiyo uwe unapenda au hupendi itakubidi ule chakula kuondoa njaa.

Hiyo ni kula, sasa yapo mambo mengine usipoyafanya hayawezi kuonyesha madhara yake haraka. Haya mambo ndio wengi wetu tunapuuzia kuyatenda, tukijua hata usipofanya hakuna akayekusumbua. Na wakati mwingine unaenda mbali zaidi kusema unajuana na Mungu wako.

Labda tuseme tumejiwekea utaratibu wa ibada za kila wiki, tuseme labda utaratibu wetu wa kusali ni siku ya jumapili. Wote tukakubaliana tutakuwa tunasali jumapili, itaenda hivyo kizazi hadi kizazi. Sasa hapo baada ya kukubaliana unaweza ukarudi nyuma ukaacha kwenda ibadani, na hakuna atakayekuja kukulazimisha utoke nyumbani kwako, zaidi watakuja kukuuliza vipi ndugu mbona hatukuoni kanisani siku hizi.

Tunapaswa kulielewa hili ili tuweze kufanikiwa kwenye jambo husika, ili upate hitaji la moyo wako unapaswa kufuata kanuni ya kulipata hilo jambo. Ili uende mkoa mwingine utapaswa kusafiri kuelekea mkoa husika, haijalishi usafiri ukaotumia ila utapaswa kufanya hivyo.

Wengi wetu wameshindwa kusoma NENO la MUNGU, kwa kushindwa kujiwekea utaratibu ambao unawabana wao binafsi. Ndio maana wengi wanaanza vizuri lakini baadaye wanapofika katikati ya safari wanakosa ile kiu ya kuendelea mbele.

Tumepewa uhuru wa kuchagua kumfuata Yesu Kristo au kumfuata shetani, hakuna sehemu inayotupa kibali cha mtu akikataa kuokoka chukua panga umkatekate. Tumepewa wajibu wa kuhubiri habari njema za Yesu Kristo, ili asiyeokoka aokoke, tena kwa kuamua mwenyewe binafsi, kwa hiari yake.

Kusoma Neno la Mungu ipo vilevile, kazi yangu ni kukumbusha na kukuambia umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Una uhuru wa kuchagua kusoma Neno la Mungu kila siku au kutosoma kabisa. Na kusoma biblia kila siku kunakutegemea sana wewe jinsi utakavyojiwekea kanuni za kukubana, ili uwe na mpango huo wa kila siku.

Haitatokea tu ukawa na muda wa kutosha sana ambao umejitenga kwa ajili ya kusoma NENO la MUNGU, bali wewe mwenyewe utamua ni muda gani utakuwa unasoma Neno la Mungu na kulitafakari. Hakuna atakayekushikia fimbo kama ilivyokuwa upo mtoto mdogo, usipokula chakula unachapwa na wakati mwingine kulazimishwa.

Unaweza kutengeneza sababu za wewe kuwa msomaji wa Neno la Mungu, na unaweza kutengeneza sababu za kutokusoma Neno la Mungu. Hii itakutegemea sana wewe jinsi ulivyojiwekea kanuni zako, ambazo zinakufanya uwe na msimamo wa kuweza kujisimamia mwenyewe bila kutegemea kusukumwa na mtu yeyote.

Unaweza kuwafanya wengine kukuimarisha zaidi kwa jinsi wanavyokuwa na bidii ya kusoma NENO la MUNGU. Unavyowatazama na kuwaona jinsi wanavyoweka bidii katika hilo, wanakuwa sehemu ya kukutia moyo na kujiona kumbe haupo peke yako. Kumbuka mapatano yako, hii itakusukuma popote ulipo kutafuta sehemu iliyotulia ili usome Neno la Mungu. Utajishangaa kwa hili, na usipotimiza patano hilo utaona maumivu makali sana ambayo yatakusuma kesho ufanye vizuri.

Huenda hunielewi sana hili linalolizungumzia hapa, lakini nakuhimiza uelewe kwamba kanuni ni mchango mkubwa sana kukusaidia kufikia malengo yako. Bila kujiwekea kanuni hutoweza kufika kirahisi unapotaka kufika.

Jiwekee muda wa kusoma Neno la Mungu, kama ni saa moja asubuhi/usiku iwe hivyo kila siku, kama ni saa kumi jioni iwe hivyo kila siku. Muda wowote ule utakaopanga, uwe ndio alarm kwako kukusaidia kukusukuma utimize ahadi yako. Haitajalishi unajisikia kusoma biblia au hujisikii kabisa kusoma biblia, utajisikuma kwa sababu umejiwekea kanuni/sheria ya kufanya hivyo.

Nakusihi sana ungeuze NENO LA MUNGU ni sehemu ya maisha yako, popote ulipo kuwa mtu ambaye hawezi kumaliza siku bila kushika biblia apitie maandiko Matakatifu. Kuwa mwathirika ambaye bila kusoma Neno la Mungu huwezi kuendelea kuishi tena. Nimetumia neno mwathirika kwa maana nzuri, huenda ukanielewa zaidi ninachokisema hapa.

Nisiwe na mengi sana ukasahau hata nilichokumbia, nikukumbushe kwamba leo tupo katika kitabu cha *2 Nyakati 16*. Tenga muda wako kwa ajili ya kusoma sura ya leo, hakuna kupoteza muda katika hili bali ni kuvuna faida.

Nashukuru sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com