Usiache Kusoma Neno La Mungu kwa Kisingizio Chochote Kile.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za leo ndugu yangu, bila shaka umeipokea siku ya leo kwa furaha kutimiza mipango yako uliyopanga uitimize siku ya leo. Na wewe ambaye uliyetegemea siku ya leo iwe ya namna fulani lakini mipango yako imevurugika, usivunjike moyo endelea kuweka juhudi zaidi na zaidi utafanikiwa.

Leo nikukumbushe jambo la msingi sana, kama kinavyosema kichwa cha somo hapo chini ya SOMA NENO UKUE KIROHO, kinachosema;
Usiache Kusoma Neno La Mungu kwa Kisingizio Chochote Kile.

Tuna mambo mengi yanayoweza kutukwamisha siku ikaisha bila kusoma Neno la Mungu, ila mambo hayo hayawezi kutufanya tukaacha kabisa kujifunza Neno la Mungu. Fahamu hili litakusaidia sana, unapokwamishwa na jambo fulani siku hiyo sio tiketi ya wewe kuacha kabisa kujifunza Neno la Mungu.

Hatari sana umepatwa na changamoto leo, ukaifanya hiyo changamoto ndio tiketi yako ya kuachana kabisa na mpango wa kujifunza NENO la MUNGU. Epuka hili ndugu, kukwama sio kuacha, kukosa chakula leo ukalala njaa sio fursa kwako ya kutokula kabisa, utakufa nakwambia kama utaacha kula.

Unapopata changamoto leo, iache ipite lakini mpango wako wa kujifunza Neno la Mungu uwe palepale. Usije ukajipumzisha moja kwa moja, kwa kuona inaleta amani kutojishughulisha na kusoma NENO la MUNGU.

Unapokwama leo, haitakuwa hivyo kila siku, na kukwama kwenyewe inaweza kuletwa na kutojiandaa mapema. Kama upo kwenye gari, unaweza kusoma NENO la MUNGU kwenye kiti chako, unaweza kuamua kusoma kwa njia ya kusikiliza audio au ukasoma kawaida. Maana tablet/smartphone zetu zina uwezo wa hivyo vitu, kwanini tusitumie hiyo fursa kumtukuza Mungu kila eneo.

Narudia tena changamoto ya leo, isiwe tiketi yako ya kuacha kusoma neno la Mungu kila siku, umekutwa na shida leo ambayo inakukosesha utulivu. Acha ipite hiyo alafu wewe endelea na zoezi lako, sio inapita na wewe unaendelea kuketi hapo hapo kwenye sababu iliyopita.

Sawa na ulikuwa upo safari na basi, mlipofika katikati ya safari gari lenu likaharibika njiani, kilichofuata ni mafundi kuanza kulitengeneza huku wewe ukiwa umekaa unasubiri. Baada ya muda konda akakupa taarifa kuwa gari lipo tayari mnaweza kuendelea na safari, alafu itokee wewe ukasema nimechoka ngoja niendelee kupumzika hapa barabarani. Nakwambia wenzako watarudi kwenye gari na kuendelea na safari lakini wewe utaachwa hapo barabarani.

Kuzuia usipatwa na changamoto huwezi, maana tupo dunia iliyojaa kila kikwazo, leo unaweza kuwa unacheka sana kwa furaha uliyonayo. Ila ikafika kesho ukalia sana kwa kupatwa jambo ambalo litaumiza moyo wako. Ni sisi kujipanga na kuelewa katika safari tunakutana na mengi, na kukutana huko kusitufanye sisi tukaacha yale yanayotuimarisha mahusiano yetu na Mungu.

Haijalishi kitakutokea nini katika safari yako ya usomaji Neno la Mungu, hakikisha huondolewi na hilo kwazo katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Acha huo upepo upite ila wewe hakikisha mpango wako upo palepale wa kujifunza Neno la Mungu.

Mwanamke anapewa likizo ya miezi mitatu kazini pale anapojifungua mtoto, baada ya hapo anapaswa kuendelea na kazi. Sio kupata mtoto ndio iwe sababu ya kuacha kazi, kazi haiachwi kwa kuzaa mtoto, wala huachi kwa kupata ujauzito ndio iwe mwisho wa mambo yako mengine. Kila jambo lina nafasi yake kwa wakati wake, unapaswa kuwa mkomavu katika hili.

Najaribu kukupitisha maeneo mbalimbali ili upate kunielewa kwa hichi ninachokueleza hapa. Ifanye biblia ni silaha yako, uzuri wake ni kwamba biblia ya kawaida ambayo haipo kwenye simu haitumii umeme. Unaweza kuwa nayo kwenye mkoba/begi lako mahali popote pale.

Jenga mkakati ambao hauna mwisho wake ukiwa hai, siku zote ziwe za kujifunza Neno la Mungu, haijalishi ni kijana au mzeee ilimradi bado upo dunia na bado hujaitwa marehemu. Vyema biblia yako ikawa chakula chako kikuu cha kiroho, na usipokipata ona madhara makubwa sana mbele yako.

Kwa wale ambao tupo pamoja, leo tupo katika kitabu cha 2 Nyakati 17, tenga muda wako wa kutosha kusoma sura hii na kupata muda mwingine mzuri wa kutafakari yale uliyosoma.

Mungu akubariki sana kwa muda wako uliotoa kusoma ujumbe huu, nakutakia siku njema.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com