Fungua Moyo Wako Ili Uweze Kupokea Ukweli Wa Neno La Mungu.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona. Hatuna budi kumshukuru Mungu wetu kwa fadhili zake, ni neema tu sisi kuifikia leo, hakuna aliyelipia hii pumzi.
Unaposoma Neno la Mungu kuna vitu vinaweza kukuzuia kabisa usiweze kuelewa vizuri, moja ya kitu hicho ni kutofungua moyo wako uweze kuupokea ukweli wa Neno la Mungu.
Tunaweza kujiwekea mipaka ya mafundisho mbalimbali kutoka kwa watumishi, kutokana na sababu zetu ambazo tunaziona kwetu, inaweza kuwa kutokana na mapokeo yetu. Ila Neno la Mungu halina kipimo cha kuchota wala kuchukua, unapaswa kulikubali hata kama linapingana na ulivyoaminishwa.
Usipolikubali Neno la Mungu, utakuwa unapingana nalo sehemu nyingi sana, Neno la Mungu litakuelekeza hivi, wewe utasema niliambiwa hivi. Sasa hapo unakuwa unasoma kitu ambacho unapingana nacho huku unataka kumjua zaidi Mungu.
Ikiwa umedhamiria kweli kujifunza Neno la Mungu, hebu maanisha kweli, usiwe nusunusu, NENO linakuambia SAMEHE ALIYEKUKOSA, wewe unaanza kupima kosa la kusamehe na la kutosamehe. Unaanza kuona biblia haitendi haki kukuambia usamehe mtu aliyekufanyia kitu kibaya. Umesahau kabisa hapo hapo biblia inakuambia kisasi ni juu ya Bwana, ila wewe unataka ulipize kisasi.
Sijui kama unanipata vizuri hapa, nasema na wewe unayejifunza NENO LA MUNGU, unapaswa kufungua moyo wako kupokea kila fundisho lililo ndani ya biblia. Nimekwambia tangu mwanzo unaweza kuchuja mafundisho mengine ila sio Neno la Mungu, fahamu hili likusaidia maeneo mengi sana.
Ukijiweka sawa katika kusoma NENO, utaona ukipokea mambo mengi sana ambayo awali hukujua kama Mungu anasema hivyo. Ila hapohapo unaweza kusoma, na usijue umhimu wa Neno hilo kutokana na vile ulivyowekewa misingi huko nyuma.
Ruhusu moyo wako kupokea NENO LA MUNGU, haijalishi NENO lile litaenda kinyume na dini yako, ikiwa nia yako ni kwenda kuishi maisha ya umilele baada ya haya. Unapaswa kusikiliza Neno la Mungu linasemaje, najua umewahi kusoma huu mstari, hebu usome tena;
*Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi. Ezekieli 12 : 2 SUV.*
Kumbe upo uwezekano wa mtu kuwa na masikio yanayomwezesha kusikia lakini asiweze kusikia, kumbe upo uwezekano wa mtu kuwa na macho ya kuona ila akawa haoni japo anatazama.
Yesu akawaambia wanafunzi wake hivi, soma kwa umakini maana unaweza kusema haya nayatunga tu kichwani;
REJEA; *Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie. MTHAYO. 13:13-17 SUV.*
Ndugu yangu yakupasa kujichunguza kwa makini sana, tunaweza kwenda pamoja hapa katika kusoma neno la Mungu. Kumbe ukawa huelewi kabisa unachosoma, sio kwa sababu nyingine, ni ile mipaka uliyomwekea Roho Mtakatifu kutokana na mapokeo ya dini/dhehebu lako.
Utashangaa biblia ni hii hii, wenzako wanafunguliwa kwa namna ya pekee sana ila wewe umebaki vilevile. Ndio maana usishangae ambaye hajaokoka, akashindwa kuelewa Neno la Mungu linasema nini japo ameweza kulisoma.
Biblia imetuweka wazi kabisa, na hapa ikasema hivi;
*Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo. 2 TIM. 4:3-4 SUV.*
Hebu jiulize ni kwanini Neno la Mungu linasema hivi, ila wewe hutaki unataka kusikia fundisho lingine linalokupa faraja uendelee kudumu katika baya. Sio hali ya kawaida kabisa, nimejaribu kukupitisha katika maandiko, uelewe vizuri uzito wa hili ninalokuambia hapa.
Ningeandika tu bila kukupa maandiko yeyote huenda ungesema ninajisemea tu, Roho Mtakatifu ameliona hilo ndio maana anakuletea msisitizo wa maandiko Matakatifu.
Fungua moyo wako sasa uweze kusoma neno la Mungu, na uweze kuelewa kile unasoma, na kibadilisha mwenendo wako wa maisha yako. Ni ajabu sana kuikataa kweli ya Neno la Mungu, ukaikubali kweli ya mafundisho ya wanadamu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kwa ajili ya kusoma ujumbe huu, nikutakie wakati mwema.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com