Mafanikio Ya Kiroho Unayoyaona Leo Kwa Mtu Mwingine Hayajatokea Ghafla.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena nzuri kabisa Bwana wetu ametupa kibali kingine tena cha kwenda kumzalia matunda mema. Kwa sisi tuliomjua yeye na kumkiri kuwa Bwana na Mwokozi wetu. Kila mmoja anapaswa kumshukuru Mungu kwa neema hii ya kuiona siku ya leo tukiwa hai, sio jambo rahisi kabisa.
Kila mmoja anayempenda Mungu na kumtumikia, hutamani kufikia hatua fulani kiroho. Hili linaweza kuwa hitaji la wengi sana, ambapo hitaji hili husababisha wengine kuanza kufanya vituko, na wengine huanza kulazimisha waonekane.
Hali hii inaweza kuwa imeletwa na kuwaona watumishi wengine wakiwa viwango fulani vya juu kiroho, au imeletwa na marafiki zetu waliotutangulia kuujua wokovu, au imeletwa na watu ambao wameokoka muda sio mrefu wakiwa wametukuta tayari sisi tupo ndani ya wokovu.
Tunapoona makundi ya watu wa namna hii, tunaona wao kama wana upendeleo fulani mkubwa, ila ukipata muda wa kuwauliza gharama waliyotoa mbele za Mungu kwa ajili ya kuutafuta uso wake, ni gharama kubwa na imechukua muda mrefu sana.
Haya yote tunaacha kufikiri na kuona imetokea tu kwa bahati mtu yule kuwa hapo alipo, lakini mapito na mateso aliyopita mtumishi yule katika utumishi wake. Huenda kikombe chake usingeweza kukinywea hata kidogo.
Kikombe alichokinywea Daudi kabla hajawa mfalme, kilikuwa ni kizito mno japo Mungu alimteua kusimama katika kiti cha kifalme badala ya Sauli. Japo Saul alijua Mungu ameshamwondolea nafasi yake kwake na kumtupia roho mbaya, aliona nafasi ile inaenda kuchukuliwa na Daudi.
Vita vikali vilianza pale tu alipoimbiwa nyimbo za ushindi kwa Goliati, vita vile vilikuwa kuitafuta roho ya Daudi iangamizwe. Ilikuwa ni vita kali sana, mapito yake yalikuwa ni magumu, pamoja na Mungu kumpaka Daudi mafuta kwa ajili ya kazi yake, ilikuwa haijamwondolea kile kilichompata.
Tunamsoma pia Yusuph, ambaye alipita vipindi tofautitofauti vya kuumiza moyo wake, japo Mungu alimwonyesha atakuwa mtu mkubwa katika kizazi chake.
Baada ya mapito yale mazito, tunaona huduma zao Mungu akiziinua kwa viwango vya juu sana, kumbe ilikuwa ni kipindi chao cha kuandaliwa. Mungu kukuchagua wewe umtumikie, haiondoi vipindi vya kuchekwa, haiondoi vipindi vya kutafutwa uawe, haiondoi kipindi cha kukataliwa.
Yapo madarasa utapitishwa ili kuimarisha, yanaweza kuonekana ni mateso makubwa kwako, yanaweza kuonekana ni maumivu makali kwako. Unapaswa kuvumilia na kutunza agano lako na Mungu, kutunza maisha yako ya wokovu yasipotee/yasiharibike.
Haya tunayajua kwa Kusoma Neno la Mungu, tunaposoma neno la Mungu tunapata kufunguliwa maeneo mbalimbali katika maisha yetu ya kiroho. Pale tunapoona mambo yamekuwa magumu katika huduma zetu, neno la Mungu linatupa mwanga tunachopaswa kufanya wakati huo.
Daudi asingekuwa na Neno la Mungu ndani yake, angempiga Saul, maana alikuwa ana uwezo huo wa kumuua adui yake. Lakini alikuwa anajua wakati wake wa kuitwa mfalme katika hali ya nje ilikuwa bado, japo alishapakwa mafuta na Samweli.
Sijui kama unanielewa hapa, nazungumzia mafanikio ya mtu, ambaye unaweza kuona labda yeye ana bahati sana kuliko wewe. Nakupitisha kidogo maeneo machache upate kujua kuwa kila jambo lina majira yake ya kuinuliwa na kukalishwa katika kiti chake.
Ikiwa Mungu amekuchagua kuwa mtumishi wake, usiwe na haraka sana ya kuanza kugombania nafasi aliyokupa. Anajua ni wakati gani atakudhihirisha kwa watu wote kuwa wewe ni mchungaji, mwinjilisti, nabii, mtume.
Haijalishi umeimba alafu ukafukuzwa mbele ya madhabahu/jukwaa, uwe na moyo wa ushujaa kujua kwamba. Kuuzwa utumwani kwa Yusuf, haikuwa mwisho wake, ujue kwamba kufungwa gerezani kwa Yusuf haikumzua yeye kuwa waziri mkuu.
Unasoma Neno la Mungu, lakini huelewi sana kama wengine unavyowaona wanasoma na kuelewa vizuri sana. Usivunjike moyo, endelea kuongeza bidii haswa utafika hatua ambayo utaona ulipo sio ulivyoanza.
Unatamani kufundisha Neno la Mungu, lakini ukianza kuelezea maandiko unaona kabisa kuna maeneo unakwama. Hiyo isikuvunje moyo, endelea kuongeza juhudi zaidi ya kusoma maandiko na kupata muda wa kutafakari yale uliyojifunza.
Mafanikio yanayoletwa na Mungu, yana hatua zake, haijalishi amekuandaa kuwa mtumishi wake. Kuna maeneo lazima akuandae vizuri ili jina lake likatukuzwe zaidi ya ulivyomuua Goliati wa Gati.
Usiache kusoma Neno la Mungu kwa kuona mafanikio kidogo sana katika usomaji wako, iwe furaha, iwe huzuni, Neno la Mungu liwe chakula chako cha kila siku zote za uhai wako. Usivunjwe moyo na asiyejua uhusiano wako na Mungu ukoje, asiyejua Yesu Kristo alikuokoa katika mazingira gani.
Uwe makini sana unapoianza safari ya kumtegemea Mungu, safari hii ina vita na mateso mengi. Maana neno linasema mateso ya mwenye haki ni mengi, kwa sababu anayetafutwa sio wewe, ni ule uhusiano wako na Mungu utafutwa upate kuharibiwa.
Mpaka hapo naamini kuna kitu umekipata ambacho Mungu alikikusudia ukipate kupitia ujumbe huu. Huenda katika maneno haya yote hujaona yakigusa sana maisha yako, ila upo mstari mmoja tu ndio umeona ukibeba kila kitu. Chukua hilo hilo maana ni la kwako, fanyia kazi ili uendelee kuimarisha wokovu wako.
Neno la Mungu linatupa ujasiri maeneo mengi sana katika maisha yetu, kila mmoja wetu akilijua hili tutapona mengi na kuimarisha mahusiano yetu na Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako,
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com