Usilikubali Wazo Lolote Linalokuzuia Kusoma Neno La Mungu Likapata Kibali Ndani Yako.
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, habari za leo ndugu katika Kristo, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona. Kila mmoja wetu anapaswa kuitumia vyema siku ya leo, kwa kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.
Tunakazana kuzungumza kuhusu kusoma neno la Mungu, sio kana kwamba watu hawajui kusoma, na sio kana kwamba hawatamani kusoma NENO. Ule msukumo wa ndani unaoambatana na nidhamu ya mtu binafsi unakuwa hakuna kabisa.
Hili jambo la kusoma neno la Mungu, limesemwa sana na watumishi wa Mungu, nimekuwa nasikiliza watumishi mbalimbali. Ndani ya mafundisho/mahubiri yao, lazima kuna msisitizo wa kusoma Neno la Mungu.
Ikiwa watumishi wa Mungu wanatuhimiza hili jambo, changamoto huwa inatokea wapi mpaka tushindwe kusoma Neno la Mungu. Shida ipo kwenye marafiki tunaozungukwa nao, marafiki hawa wana mchango mkubwa sana kumrudisha nyuma aliyeamua kuanza kusoma Neno la Mungu.
Unajiuliza anarudishwaje nyuma, kurudishwa nyuma ni rahisi sana kwa mtu ambaye hajajipanga yeye mwenyewe binafsi. Ni rahisi kurudishwa nyuma na wengine wasiopenda Kusoma Neno la Mungu, kwa kukosa nidhamu binafsi.
Unaweza usiwaone wakikuzuia kusoma Neno la Mungu moja kwa moja, ila kwa kuwa hujajiwekea utaratibu mzuri na nidhamu binafsi. Unajikuta ulianza vizuri kusoma lakini wazo lingine likakujia, mbona hawa hawasomi NENO na maisha yao yanaendelea vizuri.
Hebu wewe fikiri katika familia yako nzima labda unayetenga muda wa kusoma Neno la Mungu, ni wewe tu. Tena sio kwamba wote hawajamjua Kristo, wanamjua na wanaenda kanisani vizuri sana, sasa hapa unapaswa kujipanga. Maana unaweza kukutana na kejeli za kila aina, unaweza kukutana na kuzuiliwa kushindwa kuendelea na juhudi zako.
Ukiwa ndani ya ndoa, shetani anaweza kumtumia mke/mume wako asiyependa kusoma Neno la Mungu, kukuzuia au kukupinga usiendelee na utaratibu wako. Ukiwa unaishi na wazazi/walezi wako, wanaweza kutumika kama ukuta kwako, kukuzuia usiwe na ratiba ya kusoma neno la Mungu. Unaweza kuambiwa muda wote unautumia kusoma NENO tu, unashindwa kufanya kazi zingine, kumbe huwa humalizi hata nusu saa.
Hivyo vyote ni vita vya kukufanya usiwe mshindi kwa kile ulichoamua kukifanya, ndio maana unapata misukosuko kama hiyo. Unafika muda unaona kuna haja gani kuendelea kusoma Neno la Mungu, wakati kila siku unakutana na maneno mabaya ya kukuumiza moyo wako.
Neno la Mungu halitufanyi tuwe wajinga, bali linatufanya kuwa werefu zaidi kiroho na kimwili, kwa sababu hiyo unapaswa kuwa mwangalifu sana na ratiba zako. Tenga muda wako maalum wa wewe kusoma neno la Mungu, muda ambao hauingiliani na ratiba ya mtu mwingine.
Tumia maarifa unayoyapata ndani ya Neno la Mungu kuyaishi kwa vitendo, yaani watu walivyokujua jana ukiwa na tabia fulani mbaya wakushangae leo kwa mwenendo wako mzuri. Hapa utawafanya wanaokupigia kelele za kukuzuia wasiendelee kufanya hivyo tena, wabaki na maneno yao ya pembeni.
Jambo lingine kuepuka kugombana na wengine, tenga muda wako wa kusoma Neno la Mungu baada ya kumaliza shughuli zako, au tumia muda wako wa asubuhi sana kabla ya kuanza shughuli zako, au tumia muda wako wa mapumziko kusoma Neno la Mungu. Hapa hakuna atakayekuzuia au kukukera.
Hizo zote zinazokupa ni mbinu za kukuwezesha kuwa mshindi katika usomaji wako wa Neno la Mungu, wengi wanarudi nyuma kwa kuruhusu mawazo mabaya ya kukatisha tamaa. Kwa sababu ya kutoweka msingi imara, wanajikuta wanaacha kabisa na kusahau kama waliwahi kuwa na utaratibu wa kusoma Maandiko Matakatifu.
Kuanzia leo wazo lolote litakalokujia ili kukuvunja moyo uache kusoma Neno la Mungu, usilikubali kamwe. Zaidi lichukulie jambo hilo kama changamoto kwako ya kukuimarisha zaidi katika ukuaji wako wa kiroho.
Usiwe mtu wa kukubali kirahisi madhaifu yawe sehemu ya kukuzuia usifanikiwe, yapa madhaifu yako sababu ya wewe kufanikiwa zaidi. Kwa kuweka juhudi kubwa zaidi ya kusoma Neno la Mungu.
Ulikuwa mbioni kuacha kusoma Neno la Mungu, kuanzia leo rudi kwa upya. Na wewe ambaye ulikuwa unasitasita kuanza, anza sasa kusoma biblia yako, hutojuta kwanini ulitoa muda wako kusoma Neno la Mungu.
Nashukuru sana na nakutakia siku njema.
Tuendelee kuwa pamoja,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com