Jua Ahadi Zako Ili Uweze Kuzifuata Na Kuziishi.

Asifiwe Yesu Kristo, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona tena. Tuna nafasi nzuri sana ya kufanya mambo yanayompendeza Mungu na kuweka misingi mizuri juu ya maisha yetu.

Tunapaswa kuishi kama wana Mungu waliokolewa kwa damu ya Yesu Kristo, hatupaswi kuishi kama watumwa wasio na uhuru ndani ya nchi yao. Uhuru wetu unaletwa na sisi wenyewe kujua kuwa tumekombolewa kwa damu ya thamani.

Tumeshindwa kutunza thamani ya wokovu wetu ndani ya maisha yetu, kwa kutojua kwetu thamani kubwa iliyotumika kutukomboa. Tunakuwa kama wafungwa wasioweza kuyatimiza malengo yao kwa kufungwa kwao.

Ulivyookoka ulifunguliwa katika kifungo cha dhambi, baada ya hapo ukawekwa huru, na hiyo huru unapaswa kujua haki zako za msingi ili usiendelee kuishi kama upo utumwani/gerezani.

Unaweza kuendelea kuishi kama mtumwa kwa mtazamo hasi ulionao ulipokuwa utumwani. Hii ipo na inatutesa tulio wengi sana, inasababishwa sana na kutojua kwetu neno la Mungu.

Kuokoka tu haitoshi kukufanya ujue Neno la Mungu kama hutochukua hatua ya kulisoma, unaweza kuendelea kuwa katika kifungo fulani kwa kutojua neno la Mungu juu ya hilo linalokutesa.

Unaweza kuwa unateswa na kumbukumbu mbaya kwa sababu ya kukosa Neno la Mungu ndani yako, ungejua Mungu anasemaje juu ya hilo jambo usingepata shida. Usingehifadhi uchungu mwingi ndani yako huku umeokoka, uchungu mwingine unadumu ndani yetu kwa kukosa maarifa sahihi ya neno la Mungu.

Ndio maana unaona mtu anaokoka ila tabia zake zipo palepale, huwezi kumtofautisha kabla hajaokoka na huwezi kumtofautisha baada ya kuokoka. Maana zipo tabia kwa mtu zinaondolewa taratibu kadri anavyozidi kulijaza Neno la Mungu moyoni mwake.

Ili tuufurahie wokovu wetu, tunapaswa kuzijua ahadi za Mungu juu ya maisha yetu, tunapaswa kusoma Neno la Mungu kwa bidii sana. Vinginevyo tutaendelea kufungwa na mapokeo potofu tukijua ndivyo tunavyopaswa kuishi wokovu, kumbe sivyo tunavyopaswa kuenenda.

Wengi hatuonekani magerezani, ila yapo magereza yaliyo ndani ya fikra zetu. Fikra zetu zimefungwa kwa kushindwa kujua kama tupo huru. Ni sawa na kuku aliyekuwa amefungwa kamba mguuni, akija kufunguliwa anabaki vilevile ametulia mpaka anakaposhtuliwa.

Kuku aliyefungwa muda mrefu huwezi kumfanyia mashindano ya kumkimbiza, kama hutomfungua mapema ajue kuwa yupo huru. Ndivyo ilivyo kwetu tunaokolewa, kuujua uhuru wetu ni pale tunapojua Yesu Kristo ametusamehe dhambi zetu. Haitoshi tu kujua tupo huru, tunapaswa kujua haki zetu baada ya kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu.

Ukijua kwanini kusoma Neno la Mungu ni mhimu sana katika maisha yako, hutochoka kutenga ratiba yako ya kutulia mbele za Mungu kujua ahadi zake juu ya maisha yako. Hutojisikia kupungukiwa kitu kwa kutoa muda wako kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu, zaidi utajisikia kuongezewa vitu vingi katika maisha yako.

Siku hizi ukiingia nyumba za kulala wageni unakutana na biblia mezani, kama hakuna unaweza kuomba ukapatiwa. Siku hizi biblia zipo ndani ya smartphone/tablet zetu, popote ulipo unaweza kutafuta sehemu iliyotulia ukajipatia maarifa yako. Hakuna kisingizio cha nilishindwa kubeba biblia kutokana na safari niliyokuwa nayo.

Tafuta ahadi zako na kusudi la wewe kuzaliwa ndani ya biblia yako, jenga tabia hii maisha yako yote, yaani hakuna kustafu. Labda itokee macho yako yakakosa nguvu kutokana na uzee, lakini bado kuna miwani zinazokuwezesha usome bila usumbufu. Labda ifike nyakati ambazo biblia imesema ni mbaya, ambazo mwili wako hujewezi tena kutokana na udhaifu wa uzee.

Tukiwa bado wenye nguvu za kumzalia Mungu matunda, tunapaswa kuzijua ahadi za Mungu na kuzitendea kazi tukiwa bado wenye nguvu za kutosha. Uzee wako uwe ni hitimisho ya mambo yote uliyoyatenda ujanani, huu wakati ujana uwe ni wa kutenda kazi ya Bwana kwa kadri Mungu alivyokupa nafasi.

Utajuaje ahadi za Bwana juu ya maisha yako? Ni kwa kusoma Neno la Mungu, na kuyatenda yale mema unayojifunza ndani ya biblia.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Endelea kufuatilia masomo mengine mazuri zaidi ya kukujenga,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com