Tumia Muda Wako Wa Amani Kulijaza Neno La Mungu Litakufaa Wakati Ambao Huwezi Kufanya Hivyo.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona tena. Kila mmoja wetu anayo nafasi ya kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Nikukaribishe katika somo hili la leo ambalo naenda kukumbusha baadhi ya mambo machache sana, kadri Roho Mtakatifu atakavyoniongoza kukupa yale aliyotaraji uyapate kupitia ujumbe huu.

Tumekuwa tukitumia muda wetu vibaya na kujipa faraja kuwa tupo na mambo mengi sana, kiasi kwamba hatuwezi kupata muda kusoma Neno la Mungu. Kujipa faraja hii imetufanya tuendelee kutokusoma kabisa Neno la Mungu.

Tunapofika wakati ambao akili zetu zimefika mwisho ndio huwa tunaanza kutangatanga kutafuta msaada wa Mungu. Sio ule msaada wa maombi ya kulala, sio ule msaada wa maombi ya kuombea chakula ule. Ni msaada ambao huoni ufuate njia ipi, na kila mmoja anakupa maoni yake.

Ndugu yangu zipo nyakati kama hizi, najua umewahi kukutana nazo au bado hujakutana nazo. Ila zipo nyakati ambazo unahitaji kuchukua maamzi sahihi wewe kama wewe, hata kama umesikiliza ushauri wa wengi, mwisho wa yote unapaswa kubaki na Mungu wako.

Hapa ndipo unaweza kukuta wengi wetu tunafanya maamzi yasiyofaa, maamzi ambayo baadaye hugeuka majuto. Majuto ambayo yanakuwa tayari yana matokeo hasi.

Wakati tungekuwa na ujazo mzuri wa Neno la Mungu, tungekuwa na wazo jema la kufuata, haitajalisha ulisikiliza sauti za watu wangapi. Lipo wazo moja katika hayo yote ulipaswa kulifuata.

Unapotenga muda wako wakati una utulivu wa moyo wako, unajipa maandilizi mazuri ya wakati usioujua maneno yale kukufaa vizuri.

Ninachoweza kukushauri kuanzia Leo, ni kutoa muda wako kila siku, nasema kila siku kwa sababu hatujui tutakutwa na Nyakati zipi mbaya ambazo hatutaweza kusoma Neno la Mungu.

Ukilipuuza hili matokeo yake ni mabaya sana, sikutishi kwa sababu labda nipate kitu fulani kwako. Nakupa uhalisia wa maisha halisi ya mkristo, sifaidi chochote kwako zaidi kukupa maelekezo alafu uamue mwenyewe kuyafuata au kuyaacha.

Labda nikutolee mfano huu utanielewa zaidi; hapa nilipo naandika ujumbe huu nikiwa ndani ya gari natoka Singida naelekea Arusha, sio naenda kustarehe huko niendako, naenda msibani. Hapo hapo kuna mdogo wangu nimemwacha amelazwa tangu jana, Na muda niliolala ni saa sita na nimeamka saa kumi alfajiri.

Unaweza kuona ni kiasi gani wakati kama huu nisingeweza kukuandikia ujumbe huu, maana nina kila sababu ya kujipa ili kuepuka hili.

Kukuambia haya sio kukuonyesha jinsi gani nina matatizo, nataka kukuthibitishia haya ninayokuandikia yana ukweli au nakupa hadithi za kale. Nakueleza vitu halisi ambavyo vitakuwa msaada mkubwa sana katika maisha yako.

Unaweza usifanye yote unayopaswa kufanya, Ila utakuwa umejisaidia mwenyewe kuwa na stamina za kukabiliana na changamoto ambazo huwa zinakuja bila taarifa.

Jitahidi sana kusoma Neno la Mungu, litakufaa sana sana wakati wa tabu yako. Wakati ambao kila mtu atakuwa anakushauri kwa jambo moja, wakati ambao kila mtu atakuwa anajua hata kama hajui.

Naamini umepata kitu cha kukusaidia katika safari yako ya kujifunza Neno la Mungu, fanyia kazi yale uliyojifunza.

Nashukuru sana kwa muda wako,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com