Rahisi Kusema Ngumu Kuweka Vitendo.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona tena. Bila shaka tunapaswa kutoa muda wetu mzuri kumzalia Mungu matunda yaliyo mema.
Tumekuwa waongeaji wazuri sana, waongeaji wa vitu vingi ambavyo ukija kwenye matendo unakutana na sifuri. Tunafika kipindi tunaongea mpaka tunapitiliza, na jamii inayotuzunguka inatusikiliza na kufika kipindi inatuona ni waongo tu.
Ongea ni nzuri, ikiwa ongea ile itaambatana na matendo ya kile tunazungumza. Tuelewe pia sio kana kwamba kila tunachokizungumza kitaweza kufanyika vile tulifikiri. Ila kujaribu kufanya na kuweka bidii kwa kile tulichoanzisha, inatuweka kwenye imani nzuri ya kuaminika na Wengine jinsi vile tunavyojituma kufanya.
Tunakuwa na maneno kiasi kwamba tumekuwa kero kwa wengine, maana wakitazama jana uliahidi kitu fulani lakini hukukitimiza. Wakirudi nyuma zaidi wanaona msururu wa matukio mengi uliyowahi kuahidi lakini hukutekeleza, na bado unaendelea kuahidi mengi zaidi.
Huenda hujawahi kuahidi kumtendea mwingine kitu, ila huwa unajiahidi wewe mwenyewe kufanya jambo fulani. Ila baada ya kujiahidi kufanya hicho kitu, ulianza kwa hatua fulani ndogo ukaacha au hukuanza kabisa zaidi ya maneno.
Biblia inatuambia imani bila matendo imekufa, kama unaamini ukifanya jambo fulani utafanikiwa. Alafu ukawa hufanyi hicho kitu, huko ni kujidanganya maana hicho kitu hakitatokea kwako kwa miujiza, kwa sababu kinakuhitaji uchukue hatua.
Tunaongea sana kuhusu kusoma Neno la Mungu, tunajiahidi kiasi kwamba mpaka tumeanza kuona aibu kuendelea kujiahidi. Maana tulivyokuwa tunaanza huu mwaka, wengi sana waliahidi kusoma Neno la Mungu. Lakini walivyoanza kusoma haikuchukua hata mwezi mmoja wakarudi kwenye hali zao zilezile za awali. Wengine hawakuanza kabisa mpaka leo, wameshia tu kwenye maneno mengi na leo tupo mwezi March.
Utaendelea kuimba huu wimbo wa nitasoma Neno la Mungu kesho, mpaka mwaka utaisha unaendelea kuimba vivyo hivyo. Lazima uamue kuweka uvivu pembeni na kuweka matendo yaliyoambatana na bidii, na nidhamu ya hali ya juu sana. Hakuna siku utaamka una nafasi ya kutosha sana, kila siku inakuja na changamoto zake tofauti tofauti.
Tusipoweka umakini kwa kile tunachokihitaji, tutajikuta miaka inazidi kwenda bila matokeo yeyote kwa kile unachokitamani kuwa nacho. Mhimu sana kulijua hili katika maisha yetu ya wokovu, itatusaidia kuwa na bidii kwenye mambo ya Mungu.
Tuache mbwembwe za uongo, ninaposema mbwembwe najua utakuwa unanielewa. Kama hunielewi tuneweza kuipa tafsiri hii kutokana na somo letu leo, ni hali ya mtu kujisemea maneno mengi, lakini ukija kwenye matendo hakuna anachokiishi hata kimoja. Tunaweza kuita ni uzuri wa maneno ila utendaji wake ni sifuri.
Tutawezaje sasa kujisimamia wenyewe kwenye hili la kusoma Neno la Mungu kila siku, ni sisi wenyewe kuamua. Hakuna mtu atakuja kukushikia fimbo kwa hili, ni wewe na serikali yako kichwani.
Jambo lingine ambalo napenda kukumbusha, punguza maneno weka matendo, hapa ni kwa jambo lolote lile. Ongea yako iwe kidogo sana, ila utendaji wako uwe mwingi sana. Hii itakupa hatua kubwa sana katika maisha yako ya kiroho na kimwili.
Usikubali kuwa mtu ambaye hata yeye mwenyewe anashindwa kutimiza haja za moyo wake. Alafu anataka kutimiza haja za wengine, ni jambo ambalo litakuwa gumu sana kwake.
Ujumbe wa Leo umekufundisha kuacha maneno mengi na kuweka vitendo, naamini kipo kitu umekipata cha kukusaidia kuanza upya kujifunza Neno la Mungu. Kitumie hicho ulichokipata ili kikusaidie kufikia lengo lako.
Nakushuru sana kwa muda wako, nikutakie wakati mwema.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com