Kinachokusukuma Kufanya Jambo Kila Siku Bila Kuruhusu Uzembe Ni Kipi?
Bwana Yesu asifiwe wana wa Mungu, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona ili tuendelee kumtukuza yeye na kumletea sifa na utukufu. Ni fursa kwetu kuendelea kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.
Kabla hatujaendelea mbele na somo letu la leo, nichukue nafasi hii kukushuru wewe ambaye tumekuwa pamoja kwa muda sasa ukifuatilia kurasa hizi za kila siku. Ambapo leo tupo sehem ya 144, sio jambo rahisi sana kuandika hizi jumbe, na sio jambo rahisi kwako kusoma jumbe hizi kila siku.
Inahitaji sana nidhamu yako kutenga muda wako kusoma hizi kurasa zenye mwendelezo wa kila siku isipokuwa jpili mara nyingi huwa siandiki. Naamini umekuwa mstari wa mbele sana kusoma hizi jumbe na kupata vitu vya tofauti tofauti vya kukusaidia katika usomaji wako wa Neno la Mungu.
Kinachonifanya niendelee kuandika hizi jumbe ni kwa ajili yako wewe unayefuatilia kila SIKU, najua wapo wengi ambao wanaishia kusoma tu kichwa cha somo. Huenda ni uvivu ndio unamfanya asijue kilichoandikwa, au huenda ni kubanwa na majukum, au huenda hapendezwi sana na jumbe hizi, au huenda mimi mwenyewe huwa simbariki moyo wake. Moja wapo kati hayo yanaweza kuwa majibu au lisiwepo jibu kati ya hayo, ila kwa kuwa wote ni binadamu tunajua ubinadamu wetu, na tunaweza kujua mapungufu yetu yalivyo.
Kinachonisukuma kuandika zaidi bila kuchoka, ni kwa ajili ya mtu mmoja tu anayetoa muda wake kufuatilia hizi jumbe. Asipoona ujumbe ukiwa hewani, anaweza kuumia sana moyoni mwake, huyu ndiye namlenga mimi. Ndiye anayenifanya niwe na msukumo wa kuandika ujumbe mpya wa kumpa mbinu mbalimbali za kuweza kuwa imara katika fungu alilochagua la kusoma Neno la Mungu.
Huenda mtu mwenyewe ninayemsema wa kufuatilia hizi jumbe anaweza akawa ni wewe, hongera sana ndugu yangu katika Kristo. Nikuambie ukweli wewe ndiye unanifanya niwe na msukumo ndani yangu kukuandikia ujumbe, sio nyakati zote najisikia vizuri sana kukuandikia ujumbe mpya. Kupitia maombi yako natiwa nguvu za kushinda madhaifu ya mwili, changamoto ndogo ndogo ninazokutana nazo nazishinda kwa ajili ya maneno yako mazuri unayotamka juu yangu.
Unaweza kujiuliza labda ukiacha wewe kusoma ndio utakuwa mwisho wangu kuandika? La hasha najua atakuwa amezaliwa mwingine tena wa kufuatilia jumbe hizi. Huyo ndiye ataendelea kunipa hamasa na kiu ya kumpa kile Mungu amenijalia nimpe, kwa hiyo kuacha kwako kufuatilia jumbe hizi hakuwezi kunikwamisha kuendelea kuandika.
Kinachonisukuma haswa kuandika ni hicho, japo nimekumegea kipande kimoja na si vyote, ili ujue zipo sababu zinamfanya mtu kufanya jambo. Siwezi kukushirikisha yote ila kwa hii moja unaweza ukaona ni jinsi gani unaweza kuijua na ya kwako, ili uweze kuwa mshindi kwa jambo unalolifanya.
Hata kwa wale wachekeshaji unaowaona wanakupa kucheka pindi unapowasikiliza/unapowatazama. Si mara zote wanakuwa wanajisikia kufanya hilo jambo, kuna kitu huwa kinawasukuma hata pale wanapokuwa hawajisikii kabisa kufanya, wanafanya.
Muda mwingine unaamka siku hujisikii kabisa kula chakula, sio kwamba hupendi kula na si kwamba huna njaa, unaamka tu hujisikii kula. Ila kinachokusukuma ukale ni yale matokeo ya kutokula, matokeo hayo yanaweza kuwa ni kupata matatizo ya tumbo au kupoteza maisha.
Haijalishi kuna kitu unakipenda sana ipo siku utaamka hujisikii kabisa kukifanya, je ukipatwa na hali kama hiyo utafanyaje ili uendelee kukifanya kama utaratibu wako ulivyo. Lazima uwe na sababu moja tu kwanini ufanye na wakati hujisikii kufanya, hiyo sababu inaweza ikawa ndogo sana lakini ikakupa nguvu za wewe kufanya.
Nikirudi kwenye mzizi wa makala hii, ni kukuuliza unafanya nini pale unapojikuta hujisikii kabisa kusoma Neno la Mungu. Elewa kutojisikia kwako sio kwamba umebanwa sana na kazi la hasha hujabanwa ila unajisikia kuchoka tu.
Unapokutana na hali kama hii, kaa chini utulie, jiulize kwanini unasoma Neno la Mungu, ipi faida unaipata ndani ya Neno la Mungu. Labda tuseme katika kuwaza kote huko umeona sababu zote hazina uzito kama ulivyochoka wewe, daka sababu hii moja; ona kuna mtu anakufutilia kila siku kujua umejifunza nini ili umshirikishe na yeye apate kusogea hatua moja kwenda nyingine.
Naona unawaza sasa nijue kuna mtu ananifuatili ili iweje, si kila mtu anapaswa kuwa na bidii ya kumjua Mungu!! Basi tufanye hivi, kuna mtu amebakisha dakika moja ya kuishi baada ya hapo atachukua uamzi mbaya wa kujiua, na mtu pekee wa kumwokoa ni wewe. Mtu huyu amefikia uamzi huu kwa kukata tamaa na kuona hakuna maana ya kuishi tena, anasubiri useme Neno moja tu aishi.
Neno lenyewe ambalo unapaswa kumwambia ni wakati ambao wewe umechoka na wala hujisikii kufanya lolote zaidi ya kulala. Kulala kwako kutakuwa kumeua mtu mmoja ambaye alisubiri neno lako liwe la maamzi yake ya mwisho kutokatisha uhai wake.
Sijui kama unanielewa hapa, nataka uwe na picha ya kubwa ya jambo lolote unalofanya. Usifikiri kusoma Neno la Mungu ni zoezi ambalo halipendwi na watu wengi, kila mmoja ukimuuliza atakuambia anapenda sana kusoma Neno la Mungu. Lazima ataanza *lakini* sina muda, lakini lakini… zitakuwa nyingi na hazina msaada wala faida.
Kuanzia sasa tengeneza sababu za msingi kwanini usome Neno la Mungu, kama ilivyo katika maisha ya kawaida, huwezi kutoka bila nguo hata kama umechelewa sana kazini na wewe ndio mwenye funguo za ofisi.
Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia uweze kuondoa sababu za kila siku kukufanya usisome Neno la Mungu, kitumie hicho ulichokipata ili uwe imara katika usomaji wako wa Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako,
Usiache kufuatilia ukurasa wetu kwa masomo mazuri zaidi,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com