Simamia Uamzi Wako Uliochagua Kujifunza Neno La Mungu.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, zawadi nyingine tena ya siku njema Bwana ametupa kibali cha kuiona. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa wema na fadhili zake zinazodumu milele.

Baada ya salamu hizo, nikuombe unipe muda mchache nikushirikishe mambo yatakayokusaidia katika safari yako ya wokovu. Najua una haraka ila nikuombe tuende sambasamba tujifunze kwa pamoja.

Tunapolianza jambo huwa tunalianza kwa juhudi na kasi kubwa sana, wakati mwingine tunakuwa na moto kiasi kwamba tunaona hata wale tuliowakuta wanafanya. Tunawaona wanakosea sana kwa jinsi wanavyofanya kwa uzembe, huenda ikawa ni kweli kabisa wanafanya kwa uzembe. Lakini unaweza kuwaona na uzembe wao vilevile, wakaendelea kudumu walipo na wewe uliye na kasi ya kwenda mbele zaidi, ukafika njiani ukakwamia hapo.

Tunapokaukiwa na kiu ndani yetu, huwa tunaanza kujipa faraja ambazo zinaendelea kutudumaza akili zetu, kiasi kwamba mtu anajikuta amebaki palepale. Na wengine kupotelea kabisa katika kupumzika kwao, ni sawa na mtu aliyeomba likizo kazini watu wakijua atakaa muda fulani atarudi ila anaenda moja kwa moja.

Tuenaelewa kabisa upo uamzi huwa tunafanya sio sahihi kabisa, ila upo uamzi tunaweza kufanya sahihi na tukamtukuza Mungu wetu. Huu ndio uamzi ninaouzungumza mimi hapa leo, uamzi sahihi ndio mada yangu kuu katika somo hili, tuendelee kuwa pamoja.

Mtu anakwambia unajua mtumishi kwa sasa sina nafasi nzuri, naomba unipe muda wa siku mbili tatu hivi, nitakuwa vizuri katika kusoma Neno la Mungu. Zinafika hizo siku alizosema humwoni akitokea, anaweza akaja na lingine jipya au akikuonea aibu atakaa huko huko moja kwa moja. Maana yake ile safari ya kujifunza Neno la Mungu ndio imeishia hapo.

Mtu mwingine alivyoanza mwaka huu 2017, alijiwekea kabisa uamzi wa kusoma Neno la Mungu, alianza vizuri kweli kusoma Neno la Mungu. Lakini hakuchukua hata mwezi mmoja, leo ukimuuliza bado unaendelea na zoezi lako la kusoma Neno la Mungu? Atakupa sababu nyingi sana za kushindwa kwake. Ambazo zote zinaweza zisiwe na uzito wowote isipokuwa moja atakuambia sina muda au ninasoma lakini sielewi, sawa haelewi mi sijakataa. Ataachaje kutokuelewa wakati anawaza kwenda kuchati kwenye magroup ya wasap tena ya umbea, ataachaje kutokuelewa wakati anawaza kuwahi facebook/instargram asipitwe na yanayoendelea huko.

Unapochukua maamzi yeyote unapaswa kuhakikisha umejipanga kisawakisawa, kujipanga kwenyewe kunapaswa kuanzia ndani yako. Unapojipanga kwa jambo fulani alafu ukakubaliana na wewe mwenyewe pasipo kusukumwa na mtu yeyote, itakufanya kujisukuma hata pale unapojisikia kuchoka.

Jambo lolote uliloamua kulifanya linalindwa na wewe mwenyewe, kila mmoja anakazana kufikia malengo yake. Mara chache sana mtu atakukumbuka wewe wakati na yeye ana mzigo ndani yake wa kumjua Mungu wake.

Mbaya sana kufikia hatua tukajiona tulichukua uamzi usio sahihi kwa mambo ya Mungu, yanayojenga uhusiano wetu na Mungu wetu. Kusoma Neno la Mungu sio uamzi mbaya, ni jambo la msingi sana kwa kila mwamini Mwenye safari ya kwenda mbinguni.

Haiwezekani ukafika kipindi ukajiona ulifanya uamzi mbaya wa kusoma Neno la Mungu, alafu ukakubali ile hali. Ndugu hiyo ni roho ya ibilisi imekukalia ndani yako bila wewe kuwa na taarifa ya kuwa una mgeni ndani yako, ambaye anakufanya uwe mvivu kiasi kwamba unaona kujishughulisha na kusoma Neno la Mungu ni kupoteza muda wako.

Usahihi wa maamzi uliyochukua, haikupi nafasi ya wewe kutokukutana na changamoto ngumu, tena wakati mwingine unakutana na vikwazo ambavyo vinakufanya ukose utulivu kabisa. Lakini kwa kuwa tulifanya uamzi wa busara kufanya jambo linalotuletea kumjua tunayemtumikia, hatuna mashaka na uamzi wetu.

Jifunze sana kulisimami hili la kusoma Neno la Mungu, hakikisha huyumbishwi na jambo lolote. Umekutwa na changamoto fulani leo, hakikisha changamoto ile haiondoi hamu yako ya kusoma Neno la Mungu. Kukosa hamu ya kusoma Neno la Mungu, ujue kabisa una shida ya kiroho, unahitaji kuingia kwenye maombi umwambie Bwana arejeshe furaha ya wokovu wako.

Lazima uwe mtu wa kujihoji mara kwa mara, inawezekana vipi unakosa kabisa kiu ya kusoma Neno la Mungu. Na wewe umeokoka na unasema unampenda Yesu Kristo, unampenda vipi wakati yapo mambo huna msukumo wowote kuyafanya. Ukisikia suala ya kusoma Neno la Mungu unajisikia vibaya, hiyo kujisikia vibaya inatoka wapi ndugu yangu.

Kuna wakati tunajiona tupo salama kumbe hatupo salama, haiwezekani huna hamu na mambo ya Mungu alafu unafurahia tu hiyo hali. Lazima uingie magotini umweleze Mungu, nimeokoka mwaka wa tano sasa, sipo na ile bidii yangu kama nilivyoanza WOKOVU siku za mwanzo. Hapo inaonyesha huyu mtu sasa anahitaji msaada kwa Baba yake aliye juu, maana amefika hatua za kujihoji yeye mwenyewe.

Acha kukomaa na hali mbaya iliyo chukua uamzi wako mzuri, kataa haraka sana hiyo hali hasi. Unahitaji sana kumjua Mungu wako ili akusaidie kumaliza safari hii salama, kabla ya kuondoka hapa duniani yapo mambo ya msingi tunapaswa kuyafanya. Tutayafanyaje kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ikiwa tumekaa mbali na Neno la Mungu.

Jifunze hili leo la kusimamia uamzi wako, ulifanya busara kuanza kusoma Neno la Mungu. Usikubali kukandamizwa na changamoto za maisha, acha changamoto ziwe sehemu yake, na wewe simama sehemu yako.

Nikushukuru kwa uvumilivu wako, nilikuomba unipe muda mchache, bila shaka nimeutumia vyema muda ulionipa kukupa kitu cha kukusaidia.

Nakutakia siku njema yenye ulinzi wa Mungu.
Usiache kutembelea mtandao wetu kwa masomo mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com