Eleweka Kwa Kile Unachokifanya.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona leo. Ipo sababu ya mimi na wewe kumshukuru Mungu wetu kwa nafasi hii njema kabisa.

Nimekuwa nikisisitiza sana kwa jambo lolote unalofanya au unalotaka kufanya, unahitaji nidhamu kubwa sana ili usije ukaishia njiani. Unapoamua kuanza biashara yako eneo fulani uwe umefanya uchunguzi wa kutosha kuepuka kuhama hama.

Wateja wana tabia moja, unapofungua biashara yako eneo fulani hutawaona siku hiyo hiyo. Ila kadri wanavyozidi kuiona bidhaa yako unayoitoa na kuwa na uhakika nayo, wanaanza kujenga imani na wewe.

Unapoeleweka eneo lolote lile kwenye maisha yako, kuna watu unawapa urahisi, hata akili yako unaipa nafasi ya kukusukuma kufanya vizuri zaidi na kuongeza bidii kwa kile unachokifanya. Maana unakuwa na bidii kufanya kwa sababu unajua kuna wateja wako wanakusubiri ufungue ofisi yako uwape huduma.

Unapoeleweka kwa kile unachofanya, inakuwa kama tabia yako ya kufanya kile unafanya. Hata kama siku hiyo umeamka hujisikii kabisa kufanya, utajikuta unajisukuma kufanya kwa sababu unajua kwenye kufanya kuna kitu unaingiza.

Shida inakuja pale unapolipuka leo alafu baada ya siku mbili tatu unapotea, hutofanikiwa kwa kile unachofanya ndugu. Hata kufikia malengo yako uliyojipangia mwaka huu inakuwa shida maana hufanyi vitu kwa mwendelezo.

Tunaweza kukulinganisha na mtu aliyeanza kujiwekea akiba, labda mwezi huu anafanya hivyo na mwezi mwingine. Baadaye anaishia hapo, bila shaka mtu huyu mpaka mwaka unaisha atakuwa amejiwekea akiba ya miezi miwili. Ambapo ukimfuatilia vizuri atakuwa amekitumia hata kile kiasi alichoanza kujiwekea kama akiba.

Wengi ndio tunachofanya, mtu anaanza kwa fujo kweli kuamka asubuhi na mapema, baada ya mwezi mmoja tu. Anaacha kabisa kuamka mapema, na kuingiza sababu nyingi za kumfanya aendeleze uvivu wake.

Ndivyo ilivyo kwa usomaji wa Neno la Mungu, wengi wamekuwa wakihamasika na kuanza kusoma Neno la Mungu. Wanafanya hivyo kwa muda mchache sana, baadaye wanabadilisha uamzi wao kwa kuacha kabisa kusoma.

Badala yake wengi tumekuwa mafundi wa mdomoni, tunaongea tu na kubaki kubeba biblia siku za ibada. Lakini hatuelewi kabisa kilichopo ndani, tumebakiwa na ile ya kumfuatishia mistari michache anayosoma mbele ya madhabahu.

Huwa nikikaa chini kutafakari idadi ya watu waliojiunga Chapeo Ya Wokovu kusoma Neno la Mungu, kwa hesabu ya haraka sana walioingia na kutoka hawapungui watu 500 na kuendelea. Hii ni hesabu ya chini sana, walikuja wengi sana kwa fujo na mbwembwe nyingi sana, lakini baada ya muda mfupi waliishilia mitini.

Miaka inaenda sana, kama utani lakini ndio kweli, tunasoma sura moja mpaka tunamaliza kitabu husika. Tunaingia kitabu kingine vivyo hivyo kwa kusoma sura moja kwa siku, tumeenda kwa mpangilio huo tukamaliza agano jipya. Mpaka leo ninapokuandikia ujumbe huu tupo agano la kale kwenye kitabu cha EZRA, maana yake tumeanzia kitabu cha Mwanzo mpaka leo tupo kitabu cha EZRA. Usifikiri tunaruka ruka ndio maana tumefika hapa tulipo, ni hatua kwa hatua imetufikisha hapa.

Walioanza safari hii kwa kuweka nidhamu, leo hii huwezi kumwondoa kwenye mpango huu, fanya ufanyalo huwezi kumwondoa kwenye hili. Maana mwanzoni aliona kama adhabu ila leo hii anaona kama ni sehemu ya maisha yake yote, asiposoma neno la Mungu siku hiyo ni sawa na mtu aliyekosa chakula cha mwili.

Wale waliojitoa kusoma Neno la Mungu kila siku ndio tunasema ni watu wanaoeleweka kwa kile wanachofanya. Iwe masika, iwe kiangazi utamkuta anafanya kile kile, labda cha zaidi utakachomkuta amekibadilisha ni kukiboresha zaidi na kukifanya vizuri zaidi hicho anachofanya.

Leo tumeelewana mimi na wewe tusome NENO LA MUNGU ili tukue kiroho, uamzi huu uwe endelevu siku zote za maisha yetu. Uwe ni uamzi ambao watu wengine watakimbizana huko na huko wakirudi watatukuta tunaendelea na mpango wetu. Marafiki zetu waanze na sisi alafu watukimbie, wakirudi watukute tunaendelea na mpango wetu wa kusoma Neno la Mungu.

Watachokikuta kimebadilika sana kwetu ni ule uelewa na ufahamu wetu kukua zaidi ya pale walivyotuacha. Huu ndio mpango wa mtu aliyedhamiria kweli kufanya jambo, sio mtu wa kulipuka kwa msimu alafu anapotea kama hajawahi kuwepo.

Kuna vitu hata wewe unapenda kuvifuatilia kwa sababu vina mwendelezo wake kwa siku, unapenda kuangalia kitu fulani kwenye TV yako kwa sababu unajua ikifika muda fulani kipindi kinaanza. Kwanini isiwe wewe watu wakusubiri kwa sababu wanajua muda fulani utawaletea kitu kizuri.

Kwanini mwili wako usiwe na alarm inayokukumbusha muda huu ni wa kitu fulani unapaswa kufanya. Hata kama umechoka utakuwa unasikia kelele ndani yako mpaka unajikuta unafanya ndipo unajisikia vizuri. Ndio ilivyo kufanya kitu ulichokipanga kufanya, mwisho wake baada ya kukifanya unajisikia vizuri.

We chukulia ulivyokuwa unajilazimisha kuamka ili ufanye jambo fulani, uliamka kwa shida sana na kuona kama mateso. Ila baada ya kuamka na kukifanya kile ulichopanga ile huzuni ndani yako inaondoka kabisa na kujisikia amani moyoni, na kujiona wewe ni mshindi.

Jipangie utaratibu wa kujisomea biblia yako, nakueleza kitu ninachofanya mwenyewe, sikuelezi hadithi za zamani ambazo babu zetu walifanya. Lazima ueleweke katika hili, una masaa 24 kwa siku, ukiamua kabisa kutoka ndani ya moyo wako huwezi kukosa saa moja ya kutulia. Vinginevyo kama unakosa hata hiyo saa moja, muda wako mwingi utakuwa unautumia kwa vitu visivyofaa.

Bila shaka umenielewa kiasi fulani kuhusu kueleweka kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu, hata kama hujanipata sana. Chukua hatua kwa kile kidogo kimegusa moyo wako moja kwa moja, acha kulipuka na kupotea.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com