Muda Tunao Wa Kutosha Ila Tunaupoteza Kwa Vitu Visivyo Na Matunda Mbele Za Mungu.

Tumekuwa na malalamiko mengi sana juu ya muda wetu, kila mmoja amekuwa na sababu hii ya kukosa muda mwingine wa kusoma Neno la Mungu. Kuna ukweli kabisa wapo watu wanakosa muda wa kusoma Neno la Mungu, kukosa kwao muda sio kwamba yale wanayofanya yanawaletea faida kwao, na sio kwamba wanamzalia Bwana matunda.

Nimekuwa najifuatilia mimi mwenyewe kwa umakini kujua huwa muda wangu mwingi naupoteza wapi, mpaka nishindwe kuwa imara kwa baadhi ya mambo ninayofanya kwa ajili ya kumletea Mungu utukufu. Nilichokuja kugundua ni sehemu ndogo sana na zinazotumia muda wangu bila kujielewa umeishaje.

Moja ya sehemu ambazo zinakula muda wa mtu, ni kuwa kwenye m akundi mengi ya Wasap yasiyo na faida yeyote zaidi ya kuchati na kujaziana sms ambazo ukija kukaa chini ukazitasimini. Unakuta katika sms 1000, mbili tu ndio zina ujumbe wa kujenga.

Sehemu nyingine ya kupoteza muda wako mwingi ni marafiki unaokuwa nao kazini, mtaani, shuleni/chuoni na nyumbani. Yaani mnaanza kuongea kuanzia asubuhi mpaka jioni, mnachoongea hakieleweki na wala hakina lengo la kukusogeza hatua fulani kiroho au kimwili.

Wengi wanaona wapo bize sana na kukosa muda kwa sababu hii, anakutana na rafiki yake anaongea weee na kukumbusha habari za mwaka 1990. Mara wazungumzie mwingine vibaya, mara wahame kwenye mada hii, mara waingie kwa mtu fulani kumchambua, mara akipita mtu barabarani au eneo waliloketi wanageuza mada na kuanza kumwongelea mpita njia.

Jua linachoea mtu huyu amefanya kazi zake labda kwa masaa mawili au matatu tu, ila haya masaa mengine tisa ya mchana/jua ameyatumia kwa mambo yasiyo na manufaa kabisa mbele za Mungu.

Upo wakati wa kubadilishana mawazo na marafiki na ndugu, hichi ni kipindi kizuri sana unapotoa muda wako wakukaa na familia yako au marafiki zako ambao hamkuonana siku nyingi au wale mnaofanya nao huduma au kazi. Je mazungumzo yenu yanawajenga na kuwaletea faida au mnaongea tu na kujazana maneno ya ovyo ovyo.

Labda tuchukulie mnaongea na kujadili vitu vya msingi vyenye faida kwenu, je una muda maalum wa kuongea nao na kumpa Mungu muda wako au umkianza stori mpaka mnasahau hata kama huwa kuna ibada kanisani. Au mnasahau kabisa kuna kupata muda wa kusoma maandiko Matakatifu kabla siku haijaisha.

Lazima ukae chini ujiulize muda wako mwingi unautumia kweli kuzalisha na unautumia kumtumikia Mungu, au wewe unasukuma siku ilimradi imeisha. Haiwezekani mtu akawa bize masaa 24 kuanzia JANUARY mpaka leo APRIL, ubize ambao hawezi kufanya Chochote cha Mungu.

Lazima kuna sehemu inakula muda wako, kama sio kijiweni ni kwenye magroup ya wasap na huko facebook au instagram. Fuatilia utaona mwenyewe, ingekuwa upo bize kiasi hicho basi tuna imani unaingiza fedha kwa kila lisaa limoja au dakika. Hata watu wa hivyo wana muda wao mzuri wa kumpa Mungu wao.

Chunguza eneo linalokula muda wako mpaka ushindwe kusoma Neno la Mungu, kaa chini taratibu utaona mapungufu mengi sana kwako. Utashangaa una masaa manne kwa siku huwa unayapoteza bure kabisa bila kuingiza kitu chochote kichwani.

Kama una groups za wasap nyingi sana, na ukiangalia kati ya hizo groups 10, saba tu ndio zina faida kwako. Jiondoe haraka sana hizo tatu, hata kama ni hili group unaona halina maana yeyote kwako, unaweza kujiondoa. Sababu kubwa ni wewe kupata muda wako na Mungu katika kulisoma Neno lake.

Labda upo group la kazi zako mhimu unaweza kuliacha, group la familia halina shida, group la kanisani kwenu mnalopeana taarifa za msingi halina shida, group la biashara/kijasiriamali linalokupa maarifa mazuri hilo nalo unaweza kuliacha. Sasa hapa uwe mwangalifu, hakikisha kila group ambalo upo unanufaika kweli, na kwenye mitandao mengine ya kijamii tenga muda wako maalum wa kuingia na kujifunza vitu maalum unavyotaka kwa marafiki/kurasa unazopenda kupata taarifa au maarifa.

Ukishachuja magroup, nenda moja kwa moja kwenye marafiki zako unaoshinda nao, angalia muda mchache wa kuwa nao kisha agana nao. Muda mwingine unaoweza kuupoteza ni kushinda kwenye TV kuangalia Movies mbalimbali, hapa napo ondoka upesi.

Ukishamaliza hii operation safisha, nakwambia utakuwa na masaa mengi ya kufanya mambo yako, na utakuwa na masaa ya kutosha kufanya ibada kanisani, na utakuwa na muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu. Wengi huwa wanafikiri kwenda kwenye vipindi vya kanisani/semina/mikutano kujifunza maneno ya Mungu ni kupoteza muda, ila wamesahau muda wanaotumia kufanya mambo yasiyo na faida kwao.

Binafsi nimefanya hilo zoezi la kujiondoa kwenye magroup yote yasiyo na faida kwangu, haijalishi nilikuwa napata habari moja nzuri na muhimu sana. Kama habari kumi zote ni za kipuuzi, siwezi kuvumilia hiyo moja nzuri bora kujiondoa kabisa.

Msimamo wa maisha yako ni bora kuliko kwenda kwa mkumbo ilimradi siku imeenda, jenga nidhamu ya maisha yako. Tuna kipindi kifupi sana cha ujana, na tukiwa wenye nguvu, tusipozitumia vizuri hizi nguvu, zitakuja nyakati mbaya ambazo mwili wako unakuwa huna uwezo wa kufanya chochote zaidi ya kuamshwa na kulishwa.

Umejifunza mengi sana, chukua moja tu unaloona limeugusa sana moyo wako. Hilo ndilo la kwako, usiishie kusikitika na kusema kweli, weka katika matendo yale yote unayoona yatakuletea faida.

Mungu akubariki sana kwa muda wako mzuri ulionipa wa kujifunza pamoja.

Usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.