Mgandamizo mmoja Juu Ya Mgandamizo Mwingine.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, habari njema kwako ni kwamba umechaguliwa kuingia siku ya leo miongoni mwa matrilionea wa watu duniani kote. Tulikuwa wengi sana kwenye kinyang’anyiro hichi ila waliobahatika kushinda ni mimi na wewe, ambapo tumepata nafasi nyingine tena ya kwenda kumzalia Bwana matunda mema.

Tunapita maeneo mengi sana ya maisha yetu, kila kukicha kuna kitu kimoja ulichovuka wewe leo kuna mwenzeko amenaswa nacho. Ni kama vile kuachiana kijiti, leo unapitia kwenye Changamoto fulani, ukivuka wewe ni kama inahamia kwa mwingine. Vivyo hivyo ikitoka kwa huyo inatafuta mwingine, ndio maana unakutana na ndugu/rafiki yako anapita kwenye jambo ulilopita wewe wiki/miezi michache iliyopita. Unamwambia jipe moyo na mimi nimewahi kupitia hilo, ila ulishinda hiyo Changamoto.

Ninaposema mgandamizo juu ya mgandamizo, nadhani utakuwa unanielewa hichi kiswahili nilichotumia hapa. Ikiwa hujanielewa namaanisha nini, namaanisha upo kwenye tatizo moja bado halijamalizika hilo ulilokuwa unapitia, linakuja lingine jipya kabisa juu yake.

Unapokutwa na hali kama hizi uwe na uhakika huu, hilo jaribu ni saizi yako kabisa, hakuna jaribu atakaloruhusu Mungu lije kwako kama anajua huwezi kulihimili hilo jaribu. Haijalishi kuna majaribu yamepandana manne kwa wakati mmoja bila lingine kumalizika.

Unasema mtumishi mbona unanidanganya, andiko gani hilo linasema jaribu ulilonalo sasa ni saizi yako, wakati wewe unapata maumivu kiasi kwamba umefika wakati unaona giza mbele. Nataka kukuhakikishia kuwa lipo andiko ndani ya biblia yako ambayo unayo hapo ndani au uliyonayo kwenye smartphone/tablet yako.

TUSOME: Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili. 1 Wakorintho 10:13 SUV.

Bila shaka umesoma huo mstari na kuona kweli upo, sasa nataka kukuambia nini hapa juu ya tatizo juu ya tatizo au Changamoto juu ya changamoto au jaribu juu ya jaribu lingine. Kadri unavyozidi kupanda viwango vya ukuaji wa kiroho ndivyo unavyozidi kupandisha viwango vya majaribu juu yako.

Shetani hawezi kukupiga na jaribu la mtu aliyeokoka jana na wewe una mwaka ndani ya wokovu, wakati mwingine anajiona angepatwa na jambo ulilopatwa wewe angeshakufa. Wewe naye unaona analopitia mwingine mbona dogo sana au ukaona analopitia mwingine ni afadhali la kwako.

Labda hujanielewa vizuri, ngoja nikupeleke hospital utanipata Vizuri; bila shaka umewahi kuingia hospital ya mkoa wako au mkoa mwingine. Uliingia ukijiona wewe una shida sana, ukakutana na mwenzako anaumwa sana mpaka ukajiona wewe huumwi kabisa. Wakati mwingine homa inaweza kukata hata kabla hujafika kwa daktari, hii ni kwa kuona wenzako wenye matatizo makubwa zaidi yako.

Unapopatwa na jambo lolote sio mpango wa Mungu umwache, bali ni tumaini kwako utaendelea kumshikilia YESU wako. Unapopigwa na jaribu alafu ukakubali kurudi nyuma ni furah a kwa shetani kufanikiwa mbinu yake ya kukugusa kidogo ukahama njia ya kweli, ukaingia njia ya upotevuni.

Stamina zetu zinaletwa na Neno la Mungu, neno la Mungu ndio linatupa nguvu ya kutomtenda Mungu dhambi pale tunapojikuta tupo mazingira magumu ya kutushawishi tutende dhambi. Pia neno la Mungu linatukumbusha kuomba kila wakati tusije tukaingia majaribuni.

Pamoja na kuomba hatuachi kujaribiwa na mwovu shetani, anapotujaribu akutane na mizizi ya imani iliyojichimbia chini sana. Kiasi kwamba anapogusa matawi yetu mti hauwezi kukauka kwa sababu uimara wa mti ule haupo katika matawi yale, bali uimara upo kwenye mizizi. Matawi ni biashari zetu, matawi ni kazi zetu, matawi ni watoto wetu, matawi ni mume/mke wako, matawi ni wazazi/walezi wako.

Yanapoguswa matawi yako ujue lazima utafadhaika sana ila ukiwa una akiba ya kutosha ya Neno la Mungu, utapita salama bila madhara yeyote ya roho yako. Mahusiano yako na Mungu hayatapotezwa na jambo lolote maana unaye mtetezi wako yu hai.

Nakueleza haya ili ukumbuke Kusudi lako la kumtafuta Mungu kwa bidii sana hata nyakati zile ngumu unazokutana nazo za bandika bandua. Kwa sababu ukiacha kumtumainia Mungu unatafuta kuondolewa kwenye mstari wa kiMungu.

Mizigo yako mtwishe Bwana, usikae nayo kama ndio sehemu ya maisha yako wakati unaye BABA wa kukusaidia mwanaye. Hebu tujikumbushe mistari hii upate kuinua kiwango chako cha imani;

TUSOME=>> Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. 1 PET. 5:6‭-‬8 SUV.

Haleluya, hiyo ndio raha ya mtu anayejua haki zake kupitia Neno la Mungu, ndio maana tunasisitizana usimwache Yesu Kristo wakati wa kipindi kigumu. Maana shida yako anaiweza pamoja na unaona giza mbele, ukimwita yeye atakuonyesha njia ya kupita.

Kusoma Neno la Mungu hakukupi tu kujua maandiko mengi, kunakupa kujua mambo ya msingi ya kukusaidia katika uhalisia wa nyanja zote za maisha yako. Hakuna kitu kigumu kwako kisicho na suluhisho, shika hili siku zote za m aisha yako.

Utashangaza sana kama kila siku unaingia kanisani, alafu akaja mtu akakuambia umelogwa, na ili upone unapaswa kwenda kutibiwa na mganga fulani wa kienyeji. Huo sio ukomavu wa kiroho, neno la Mungu linakusaidia kutosikiliza hayo mashauri kwa sababu unajua madhara ya kuchanganya miungu mingine.

Bidii yako iongezeke zaidi ya kumtafuta Mungu wako, usirudishwe nyuma kiimani kwa changamoto yeyote ile. Kazia hapo hapo uone mkono wa MUNGU ukikutoa ulipokwamia ili uendelee na safari yako ya wokovu.

Acha matatizo yabebane kama mawe ya Singida na Mwanza, uwe na uhakika utashinda hayo unayopitia sasa. Maumivu ni makali kwa sababu una moyo wa nyama, ila yupo mwenye kupoza maumivu hayo, si mwingine bali ni Roho Mtakatifu aliye ndani yako.

Mpaka hapo nina uhakika umejifunza jinsi gani unaweza kushusha mizigo yako inapokuzidia. Nia ya somo hili ni kukujulisha kuwa usiache wokovu kwa sababu ya mambo yanayokuandama. Wakati wa kuongeza bidii zaidi ya kumtafuta Mungu, ni wakati ambao unapita pagumu, neno moja utakalotamka kwa Mungu lina nguvu kuliko maneno mengi ukiwa kwenye amani.

Nilitaka kumaliza ila kuna Neno limenijia kwa nguvu sana hapa, nami nisilibane ngoja niliachilie kwako;
Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. Zaburi 27:4 SUV.

Mungu akubariki sana kwa muda wako, nimalize kwa kusema kwamba, hata sasa yeye ni Ebenezer.

Kujifunza kila siku ni wajibu wetu, usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com