Huwezi Kusamehe Kirahisi Ikiwa Neno La Mungu Halimo Ndani Yako.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tunamrudishia yeye kwa wema wake mkuu kwetu, si wote walitamani kufika leo wamefika, mimi na wewe ni nani kama si Mungu?

Kuna watu wanaumiza mioyo yetu, unaumizwa kiasi kwamba unasikia ndani yako unapata shida na kujiuliza kwanini mtu huyu anifanyie hivi na vile.

Hakuna fundi mwenye moyo mgumu usiosikia maumivu ya kutendewa jambo baya, hata huyo unayemwona anaitwa jambazi sugu au ana roho ngumu au mbaya. Vipo vitu akifanyiwa vitaumiza moyo wake na vitaondoa usingizi wake.

Kuumia kupo pale pale, haijalishi wewe ni nani ila utofauti unakuja namna ya kuumia na jinsi tunavyoweza kubeba vitu moyoni na kuviachilia. Yupo mtu ukimfanyia jambo baya, ataumia tu kwa muda mfupi na kulipuuza hilo jambo na kuliachilia kabisa moyoni mwake kama vile hajakosewa na mtu. Yupo pia akikosewa leo anaweza kuteseka kila siku na jambo lile lile, na sio kama anafanya makusudi la hasha hana uwezo wa kuachilia hilo.

Kuna watu wamebeba wenzao moyoni kiasi kwamba akisikia mwenzake aliyemkosea amepatwa na tatizo fulani baya. Atafurahi sana, tena anaweza kufanya hata sherehe kwa furaha aliyonayo moyoni. Sawa huenda ukapata nafuu na kushangalia unaposikia Goliati ameuawa na Daudi kwa jinsi alivyokuwa analitukana jina la Mungu wenu na kuwatesa taifa lenu. Hiyo inakuwa vita ya Mungu sasa si yako tena, ila ninachozungumza hapa ni ile kushindwa kumwachilia aliyekukosea.

Pamoja na Daudi kutafutwa na Sauli kutaka kumuua, siku amesikia Sauli amekufa aliomboleza kwa manjozi mengi sana. Hakukumbuka tena yale mateso aliyokutana nayo nyuma kwa kutaka kuondolewa uhai wake na sauli, heshima yake ilikuwa kwa mfalme Sauli pamoja na mabaya aliyomfanyia.

Haingii akilini mtu kukuambia mwombee adui yako, au omba juu ya wale wanaokutendea mabaya. Sawa na mtu amekufanyia jambo baya siku ya jana alafu leo upige magoti umwombee kwa Mungu. Nakwambia pasipo Neno la Mungu ndani yako huwezi, tena unaweza kumkuta anapigwa na vibaka ukatamani kuungana na vibaka wale.

Neno la Mungu linakupa uwezo wa kuwaombea wengine, haijalishi wewe hujahusika na kosa lile utaenda mbele za Mungu kuomba toba juu yao. Ukijua kosa lile linaweza kuwaletea madhara kanisa nzima na sio mkosaji mmoja, huwezi kuwa na ujasiri wa kufurahia watu wanavyoanguka dhambini. Huwezi kufurahia kwa sababu Neno la Mungu li ndani yako, linakukumbusha wajibu wako.

Usimshangae mtu anayeshindwa kusamehe mtu aliyemkosea miaka mitatu iliyopita, chunguza kiwango chake cha kiroho kama hutamkuta ni mchanga kiroho. Utamkuta ni mtu asiyependa kujifunza Neno la Mungu, utamkuta ni mtu asiyependa kumwomba Mungu.

Hatusomi Neno la Mungu ili kuwa na uwezo tu wa kuwajibu watu maswali yanayohusu imani yetu. Tunasoma Neno la Mungu litusaidie namna ya kuweza kuwasemehe wanaotuumiza mioyo yetu, mkristo wa kweli hawezi kwenda mbele za Mungu kuomba Mungu ampe kitu fulani wakati bado hajamsamehe aliyemkosea.
Bila kuambiwa na mchungaji unakosea yeye mwenyewe atajua amekosea kanuni, kusamehe ni agizo la Mungu ili apate kutusamehe na sisi makosa yetu.

Kila mmoja anakosea kwa kiwango chake, unaweza kuwa unafikiri unawatendea watu mema kumbe unawaumiza na kuwafanya waumie ndani ya mioyo yao. Unafanya kosa labda kwa sababu ya kutojua kwako kama hilo unalofanya halimpi Mungu utukufu wala hao unaowafanyia.

Tusipokuwa na moyo wa kuachilia wale wanaotukosea hatuwezi kusema tuna mahusiano mazuri na Mungu wetu. Wakati unasikia wenzako wanajazwa na Roho Mtakatifu, wewe utakuwa umejaza mtu moyoni na kukuzuia kabisa kukutana na Mungu wako.

Haijalishi umri wako kwenye wokovu, ikiwa unasema huwezi kumsamehe fulani kwa kosa alilokufanyia. Huo ukristo wako una kasoro kubwa sana, unapaswa kupata msaada wa haraka sana. Kusamehe ni agizo la kila mwamini, hebu fikiria tangu umemshikilia mwenzako moyoni umewahi kupata zawadi gani.

Uwe mwelewa hapa, umemkopesha mtu pesa zako hajakurudishia na umefanya kila jitihada la kurudisha pesa zako. Ila ukaja kuona anakusumbua tu, tafsiri ya kumsamehe sio kwamba uendelee kumpa pesa zako hata kama ile ya mwanzo hajakurudishia. Maana yake kwamba umejua ni mtu wa namna gani, na umejua huwezi kufanya naye kazi, na umejua hazimiki pesa za watu. Kwako unabaki na funzo hilo na siku nyingine ili asikukwaze huwezi kumpa pesa yako, na rafiki yako mwingine akitaka kumpa pesa utamsaidia mawazo asifanye kosa ulilofanya wewe. Ila moyoni mwako unakuwa huna kinyongo naye wala chuki yeyote na yeye…hiyo ndio kusamehe.

Biblia inatuambia tusiwe wajinga, sasa wewe kwa kuwa nimesema usamehe, utasema kwa hiyo aliyenizulumu pesa zangu. Akija kuniomba nimkopeshe tena la hasha hapo utakuwa hujatumia akili, nazungumza kusamehe.

Labda kupitishe kwenye hili andiko alafu nimalize;
Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [ Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.] MK.11:25‭-‬26 SUV.

Bila shaka umenielewa kwa kile nimekufundisha, tunapata ujasiri wa kuwaombea na kuwatakia mema wanaotukosea kwa sababu Neno la Mungu li ndani yetu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com